Premier League yaendelea kupamba moto | Michezo | DW | 27.12.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Premier League yaendelea kupamba moto

Kuna muda mfupi sana wa kupumzika wakati ligi kuu ya England ikirejea tena kwa kishindo baada ya mechi za siku kuu ya Boxing. Kuna mechi tisa zitakazochezwa Jumapili katika ratiba ngumu

Ni kipindi kifupi mno cha mapumziko ambapo timu hucheza mechi tatu katika siku sita na kutumiwa kama mtihani kwa wachezaji. Mechi tatu za kesho zinazijumuisha timu zinazowinda kumaliza katika nafasi nne za kwanza na nafasi moja ya kufuzu katika Champions League.

Manchester United ambao kwa sasa wako katika nafasi ya tatu, watakuwa ugenini kwa nambari saba Tottenham wakati West Ham wakiwakaribisha Arsenal katika mchunao kati ya vilabu vya nafasi ya tano na sita. Mchuano wa kilele hata hivyo, utakuwa kati ya nambari nne Southampton, watakaowakaribisha viongozi wa ligi Chelsea.

Fußball Manchester City-Manager Manuel Pellegrini

Kocha wa Manchester City Manuel Pellegrini

Chelsea wanaongoza kwa pengo la points tatu dhidi ya mabingwa watetezi Manchester City baada ya timu zote mbili kupata ushindi rahisi hapo jana. Blues waliwazaba West Ham mabao mawili kwa bila wakati City wakishinda tatu moja dhidi ya West Brom.

Southampton iliizaba Crystal Palace mabao matatu kwa moja na kuiruka West Ham hadi nafasi ya nne. Kichapo hicho kimesababisha kocha wa Palace Neil Wanorck kufutwa kazi hii leo. Warnock ndiye kocha wa kwanza wa Premier League kutimuliwa msimu huu. Manchester City watakuwa na mchuano mwepesi dhidi ya wenyeji Burnely ambao wako katika nafasi ya 19.

Kiynang'anyiro cha nafasi nne za kwanza siyo pekee ambacho ni kikali kwenye msimamo wa ligi. Mambo ni magumu pia katika upande wa chini wa ligi ambapo timu sita zinapambana katika vita vya kuepuka kushushwa daraja.

Nne kati ya timu hizo zinakutana kesho wakati Leicester ikikabana koo na Hull nayo QPR ikiialika Crystal Palace. Leicester inashika mkia na points 10, tano nyuma ya Burnely na Crystal Palace juu yake. Katika mechi nyingine, Sunderland itakuwa ugenini dhidi ya Aston Villa, Stoke itacheza na West Brom, wakati Newcastle ikiialika Everton. Liverpool itaikaribisha Swansea siku ya Jumatatu ili kukunja jamvi la mechi za wikendi hii.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/reuters/dpa
Mhariri: Mohammed Dahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com