Papandreou aunda serikali mpya | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.06.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Papandreou aunda serikali mpya

Huku mgogoro wa kiuchumi ukizidi kugeuka kuwa wa kisiasa nchini Ugiriki, hivi leo Waziri Mkuu George Papandreou ameamua kutomrudisha aliyekuwa waziri wake wa fedha, George Papaconstantinou, katika wadhifa huo.

Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou

Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou

Kwa kila hali, George Papandreou, anajikuta katika wakati mgumu sana katika maisha yake ya kisiasa, na mwenyewe anakiri hilo, ingawa pia anajua kuwa ni wakati ambao anatakiwa kusimama imara zaidi kuthibitisha uwezo wake wa kuongoza.

"Haidhuru vita hivi viwe vigumu kiasi gani, tunapaswa kupambana. Nina imani na wabunge wetu. Nina imani na chama chetu. Nina imani na historia yetu. Munaweza kuniamini. Ninaweza kuwaamini. Lazima tuikwamue nchi yetu kutoka kwenye mgogoro huu." Alisema Papandreou akilihutubia Bunge hapo jana.

Katika kujenga upya imani baina ya serikali na bunge, kwa upande mmoja, na utawala na wananchi, kwa upande mwengine, leo Papandreou ameamua kumtoa kikoa waziri wake wa fedha, Papaconstantinou, ambaye sasa nafasi yake inachukuliwa na aliyekuwa waziri wa ulinzi, Evangelos Venizelos.

Amemuhamishia Papaconstantinou kwenye wizara ya mazingira, jambo ambalo wachambuzi wanasema ni sawa na kumshusha cheo.

Waziri mpya wa fedha wa Ugiriki, Evangelos Venizelos

Waziri mpya wa fedha wa Ugiriki, Evangelos Venizelos

Venizelos, mwanasiasa mkongwe, ambaye mwaka 2007 aligombania uongozi wa chama akipambana na Papandreou, amekabidhiwa pia wadhifa wa naibu waziri mkuu, sambamba na Theodoros Pangalos.

Waziri huyu mpya wa fedha anatokea kwenye mji wa kibiashara wa kaskazini wa Thessaloniki, na anatajwa kuwa ni mtaalamu wa masuala ya katiba na mzungumzaji mwenye kipaji. Aliwahi kuongoza kamati ya matayarisho ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2004.

Tangazo la kumteua Venizelos na wenzake limekuja siku moja tu baada ya wabunge wa chama cha Papandreou kumuacha mkono waziri mkuu huyo, wakimlaumu kwa namna anavyoushughulikia mgogoro wa kifedha na kushindwa kwake kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya pamoja na viongozi wa upinzani.

Wabunge wawili walijiuzulu kazi zao katika mkutano wa chama tawala uliotawaliwa na maneno makali, huku Papandreou akiungwa mkono na mawaziri wake muhimu.

Leo amemteua pia waziri mpya wa mambo ya nje, Stavros Lambrinidis, ambaye alikuwa kiongozi wa kundi la wabunge kwenye Bunge la Ulaya na mshirika wa muda mrefu wa Papandreou, wakati Papandreou alipoingia madarakani miaka kumi iliyopita.

Katika mabadiliko haya ya baraza la mawaziri, aliyekuwa naibu waziri wa ulinzi, Panos Beglitis, ambaye pia ni mshirika mwengine wa Papandreou, amepandishwa cheo na kuwa waziri kamili.

Askari wa kuzuia fujo wa Ugiriki wakiwadhibiti waandamanaji

Askari wa kuzuia fujo wa Ugiriki wakiwadhibiti waandamanaji

Mawaziri wawili muhimu ambao walisimamia mageuzi makubwa na magumu kwenye maeneo yao, waziri wa afya, Andreas Loverdos, na naibu waziri wa kazi, George Koutroumanis, wameongezewa majukumu zaidi, huku Koutroumanis sasa akiwa waziri kamili wa kazi.

Idadi kadhaa wa wapinzani wa Papandreou ndani ya chama wamepatiwa nafasi za unaibu waziri, huku akiwaacha washirika wengine muhimu, aliyewahi kuwa waziri wa fedha, Dimitris Droutsas, na wa mazingira, Tina Birbili.

Elias Mossialos, ambaye alikuwa profesa wa masuala ya sera za afya katika chuo cha Uingereza, London School of Economics, ameteuliwa kuwa msemaji wa serikali.

Kura ya imani kwa serikali hii mpya inatarajiwa hapo Jumapili, ambapo mawaziri wa eneo linalotumia sarafu ya Euro wanapanga kukutana kujaribu kutafuta msimamo wa pamoja juu ya kuikoa Ugiriki isizame kwenye mgogoro wake wa madeni.

Baadaye, serikali italazimika kuwasilisha bungeni mpango wake mpya wa mageuzi wenye thamani ya Euro bilioni 28 kufikia mwishoni mwa mwezi huu.

Mpango huo unashinikizwa na wakopeshaji wa kimataifa wa Ugiriki, kama sharti la kutoa misaada mipya, lakini makato mapya ya kodi yamewakasirisha maelfu ya Wagiriki ambao wamekuwa wakiandamana nje ya bunge la nchi hiyo kila siku.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE/Reuters
Mhariri: Othman Miraji

DW inapendekeza

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com