1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis ahimiza uwajibikaji wa pamoja wakati wa COP26

Admin.WagnerD29 Oktoba 2021

Kiongozi wa Kanisa Katoloki Duniani Papa Francis amesema mkutano ujao wa COP26 lazima utoe matumaini thabiti kwa vizazi vijavyo kwa kukubaliana juu ya hatua za kuchukua ili kuulinda ulimwengu.

https://p.dw.com/p/42Kxk
Vatikan I Papst Franziskus spricht das Angelusgebet
Picha: Giuseppe Lami/ZUMA Press/imago images

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi COP26 ukiwa unategemewa kuanza Oktoba 31 hadi Novemba 12 mjini Glasgow, Scotland, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis ametoa wito kwa mataifa yote kuwajibika katika kuulinda ulimwengu wetu.

 "Viongozi wa kisiasa lazima wavipe matumaini ya kweli vizazi vijavyo kwa kuchukua hatua thabiti zinazohitajika kupambana na mabadiliko ya tabianchi wakiwa katika mkutano wa COP26," amesema Papa Francis wakati akizungumza na shirika la habari la Uingereza BBC.

Naye Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema mkutano huo wa kilele una umuhimu mkubwa, lakini matokeo yake hayawezi kujulikana kwani majadiliano yanatagemewa kuwa magumu.

Papa Francis amekubali kuwa mkutano huo utakuwa mgumu, lakini pia unatoa fursa ya kupatikana makubaliano ya pamoja ya kuulinda ulimwengu. Ameongeza kuwa majanga ya aina hiyo huwa yanamlazimisha mwanadamu kufanya maamuzi magumu, kitu ambacho sio rahisi kufanya.

Papa Francis mwenye umri wa miaka 84, hatoweza kuhudhuria mkutano huo baada ya kufanyiwa upasuaji mapema mwaka huu. Lakini Vatican itatuma ujumbe utakaomwakilisha katika mkutano huo wa kilele wa COP26.

Mkutano huo wa kilele wa COP26 unatanguliwa na mkutano mwengine mjini Rome wa kundi la mataifa yaliyostawi kiuchumi, G20.

COP26 | Glasgow
COP26 | GlasgowPicha: Scott Heppell/picture alliance/AP

Johnson kuwashawishi viongozi wa G20

Na Johnson amesema atahudhuria mkutano wa G20 kwa lengo moja tu la kuwashawishi viongozi wa mataifa yenye chumi imara ulimwenguni kuchangia kifedha wakati wa mkutano ujao wa COP26 mjini Glasgow. Fedha hizo ni ahadi ambayo bado haikutimizwa iliyotolewa katika makubaliano ya Paris ya mwaka 2015, ya kukusanya dola bilioni 100 kuzisaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Aidha Waziri Mkuu huyo wa Uingereza pia atahimiza suala la kupunguza uzalishaji wa gesi chafu hasa miongoni mwa mataifa yanayotoa viwango vya juu vya gesi ya kaboni ikiwa ni pamoja na China, Marekani, India na Urusi. Suala lengine atakalolitilia mkazo kwenye mkutano wa G20 ni kuachana na matumizi ya makaa ya mawe.

Mataifa yanayounda kundi la G20 ndiyo yanayodhibiti asilimia 75 ya biashara ya dunia, na wananchi wake kwa pamoja wanajumuisha asilimia 60 ya idadi jumla ya watu ulimwenguni. Kutokana na ukubwa wake, mara nyingi kundi hili linalaumiwa kwamba huwa linashindwa kufanya maamuzi ya pamoja. Na kwa vile Uingereza hivi sasa imepoteza hadhi yake kutokana na mgogoro wa Brexit wa kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya, huwenda ushawishi wa Johnson usizae matunda anayoyatarajia.

Vyanzo: (rtre, ap)