Papa Francis kutaka ushauri wa mabadiliko ya kimtazamo wa Imani | Masuala ya Jamii | DW | 03.12.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Papa Francis kutaka ushauri wa mabadiliko ya kimtazamo wa Imani

Baba Mtakatifu Francis, ametoa wito kwamba sasa umefika wakati wa kufanya mabadiliko ya kimtazamo ndani ya kanisa katoliki ulimwenguni, muhimu pia kanisa lijihusishe zaidi na kuwasaidia watu maskini,huo ndio umisionari

Papa Francis akitoa Baraka kwa waumini

Papa Francis akitoa Baraka kwa waumini

Kiongozi huyo wa kanisa katoliki duniani, alifafanua hayo katika waraka wa kichungaji kutoka Vatikani kwa mabaraza ya maaskofu Duniani, wenye kurasa 224 ambapo amejumuisha mambo aliyoyapa kipaumbele katika mahubiri yake ya miezi nane ya uongozi wake tangu alipochaguliwa, hasa akisisitiza umuhimu wa kufikiri namna ya kugusa imani za watu wenye hali duni kimaisha, na taswira yake kuhusu kanisa katoliki la siku zijazo.

Papa Francis kuomba mchango wa mawazo

Katika waraka huo wa kichungaji, Papa Francis amesema, ni jukumu lake kama askofu wa Roma kufungua milango ya kupokea mawazo chanya yatakayoleta manufaa zaidi katika huduma yake ya kichungaji na kupelekea matunda mema kwa waamini, kama Yesu Kristo mwenyewe alivyotaka iwe.

Waumini wa kanisa katoliki katika misa inayoendeshwa na Papa Roma.

Waumini wa kanisa katoliki katika misa inayoendeshwa na Papa Roma.

Katika waraka huo papa Francis anasema ,huu ni wakati wa kufanya mabadiliko ya kipapa ambapo haoni sababu ya ukiritimba wa viongozi wa kanisa, kujifungia ndani na kufuata yale ya vitabuni kinadharia pasipo kujikita kwa undani katika jamii ili kuweza kujua nini watu wanachohitaji kiimani katika maisha yao ya kila siku, na kushughulikia hayo kama wachungaji. Amefafanua kuwa ni lazima mapadri wa nyakati hizi wafanye kazi ya kimisionari kikamilifu, kwa kuwahudumia watu wenye shida mitaani.

Msimamo wa Kanisa

Baba mtakatifu amesema pia kwamba, hali ilivyo sasa ulimwenguni, maaskofu wanahitaji kusimamia waamini katika misimamo ya kikanisa yenye uhalisia, inayoendana na nyakati za sasa, ili kuweza kugusa matatizo ya waamini kwa njia nyepesi pasipo madaraja yanayofanya waamini kuwa mbali na viongozi wao wa kiimani.

Katika waraka wake baba Mtakatifu, amefafanua kutoweza kuwa na baadhi ya mabadiliko katika mfumo wa kanisa kama kuwa na mapadri wanawake na suala la utoaji mimba halitoweza kukubalika katika kanisa, ila katika hilo amesisitiza kwa upande wa viongozi kuweza kurekebisha mazingira yanayowapata wanawake, yanayowalazimu kufanya tendo la utoaji mimba, ili kupata suluhu ya tatizo hilo badala ya kuwanyoshea vidole.

Uhuru wa kuabudu

Katika mtazamo wake wa kimahusianao na watu wa imani nyingine, Papa Francis amesema, uhusiano kati ya kanisa Katoliki na Waislamu inabidi uimarike maradufu, kutokana na ongezeko la wahamiaji wa Kiislamu kwenye mataifa ya magharibi yenye asili ya kikristu, unaosababishwa na vita kwenye nchi zao. Amesisitiza kuwa wakristu wanapaswa kuguswa na kuheshimu hali hiyo ya wahamiaji, kama ambavyo wakristu wangetarajia kukubalika katika nchi zenye asili ya utamaduni wa Kiislamu. Pande hizo mbili zinapaswa kuheshimu uhuru wa wengine kuabudu katika imani yao pasipo ubaguzi kutokana na asili ya imani ya nchi husika.

Kimsingi baba mtakatifu Francis, amefungua milango ya kupokea mawazo

Maandamano ya kuingia kanisani viongozi wa kanisa katoliki huko Roma

Maandamano ya kuingia kanisani viongozi wa kanisa katoliki huko Roma

mbalimbali kutoka ngazi ya chini ya kanisa, ili kugusa kila nyanja hasa kwa wale wenye hali duni na wamekuwa hawana sauti kabisa katika jamii, ambapo ameangazia kufanya mabadiliko yatakayoponya roho za waumini waliokata tamaa kiimani. Papa Francis amesisitiza kuwa injili lazima ifurahiwe na isilale, hivyo ili kanisa liwe na mwamko wa kiimani halina budi kujikita katika matatizo ya ndani ya watu.

Mkuu wa idara ya masuala ya kijamii na mawasiliano wa Vatikan, Monsinyore Claudio Celli, amesema kiujumla mtindo wa kiuongozi wa papa francis una mvuto wa ndani sana kiimani kwa watu wakawaida, hata ukisikia lugha anayotumia ni ya kawaida na pia sauti yake ni ya kiimani zaidi.

Mwandishi: Diana Kago/AFP
Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com