1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Benedict wa 16 kuwasili Cuba

26 Machi 2012

Kiongozi wa Kanisa Katoliki , Papa Benedict wa 16, leo atawasili nchini Cuba akiwa katika ziara yake ya America ya Kusini. Papa anatarajiwa kukutana na kiongozi wa zamani wa nchi hiyo Fidel Castro pamoja Raul Castro.

https://p.dw.com/p/14S8o
Papa asubiriwa nchini Cuba
Papa asubiriwa nchini CubaPicha: picture-alliance/dpa

Raia wa Cuba bado wanaukumbuka vizuri ujio wa Papa John Paul wa Pili mwaka 1988. Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki aliwasaidia Wacuba kupata upya kibali cha kusherehekea sikukuu ya Krismasi. Hadi leo, hiyo ndiyo sikukuu pekee ya kidini inayosherehekewa nchini Cuba. Papa John Paul wa Pili aliimarisha uhusiano baina ya kanisa na serikali na kuwatetea takriban wafungwa 100 wa kisiasa mbele ya kiongozi wa zamani wa Cuba, Fidel Castro.

Papa Benedict wa 16 anazuru Cuba akiwa kama mjumbe wa huruma. Akiwa nchini humo, Papa atasherehekea kumbukumbu ya miaka 400 tangu kugunduliwa kwa sanamu la bikira Maria katika mji wa El Cobre.

Kanisa Katoliki lapewa nafasi zaidi

Benedict atakutana pia na kiongozi wa Cuba, Raul Castro, pamoja na Fidel Castro, aliyeachia madaraka kwa sababu za kiafya. Raul Castro anaelezwa kuwa kiongozi aliyeleta mfumo mzuri katika taasisi mbalimbali. Hivyo sasa Cuba iko katika mchakato wa mabadiliko ya kiuchumi na kisisasa.

Papa John Paul wa Pili alipotembelea Cuba mwaka 1988
Papa John Paul wa Pili alipotembelea Cuba mwaka 1988Picha: picture-alliance/dpa

Kanisa Katoliki la nchini Cuba linajitahidi kuchukua nafasi ya muhimu katika masuala ya kijamii. Jambo hilo lilikuwa limeshindikana kwa miongo mingi. Lakini sasa Kanisa katoliki linapewa nafasi ya kuendesha shughuli za kidini na pia kuanzisha taasisi za elimu na kutangaza katika vyombo vya habari.

Upande wa upinzani watoa lawama

Serikali ya Cuba imeandaa vyombo vya usafiri wa umma vitakavyotumika kuanzia leo hadi kumalizika kwa ziara ya Papa Benedict siku ya Jumatano. Watumishi wa umma watakaopenda kuhudhuria misa zitakazoongozwa na Papa katika miji ya Santiago na Havanna hawatalazimika kufika kazini. Lawama zinazotolewa juu ya ziara ya Papa nchini Cuba ni chache sana ikilinganishwa na yale yaliyosemwa wakati Papa alipokuwa ziarani nchini Brazil na Mexico. Lawama zimetoka hasa kwa watu wenye mtazamo wa mrengo wa kushoto, ambao si wanachama wa chama cha kikommunisti kama vile kundi linalojiita "mtazamo makini." Watu hao wa upande wa upinzani wameeleza kwamba wanatamani Papa Benedict wa 16 azungumze wazi juu ya masuala ya haki za binadamu.

Rais wa Cuba, Raul Castro
Rais wa Cuba, Raul CastroPicha: dapd

Arturo López Levy, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kisiasa katika chuo kikuu cha Denver nchini Marekani, anaeleza kwamba Wacuba wengi walikuwa wakiusubiri kwa hamu ujio wa Papa. Watu wapatao 400 wanatarajiwa kufika Cuba kutoka nje ya nchi hiyo kwa ajili ya kumwona kiognozi huyo wa kidini.

Mwandishi: Rosa Muñoz Lima / Violeta Campos

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Saumu Yusuf