Papa ataka mazungumzo ya amani ya kijasiri | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Papa ataka mazungumzo ya amani ya kijasiri

Papa Francis amewataka viongozi wa Wapalestina na Israel wakate kiu ya amani ya watu wao kwa mazungumzo ya kijasiri wakati wa mkutano wa sala ya maombi ukiwakutanisha Wayahudi, Wakristo na Waislamu huko Vatican.

Papa Francis na Rais Mahmud Abbas wa Wapalestina (kushoto) na Rais Shimon Peres wa Israel (kulia) katika bustani za Vatican. (08.06.2014)

Papa Francis na Rais Mahmud Abbas wa Wapalestina (kushoto) na Rais Shimon Peres wa Israel (kulia) katika bustani za Vatican. (08.06.2014)

Papa Francis ametowa wito mzito Jumapili (09.06.2014)kwa Rais Shimon Peres wa Israel na mwenzake Mahmoud Abbas wa Wapalestina mwishoni mwa misa ya jioni ya saa mbili iliofanyika katika bustani za Vatican, mjumuiko ambao papa anataraji utauanzisha tena mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati.

Amesema juhudi za kutafuta amani zinahitaji ushujaa kuliko hata ule wa vita, unahitaji kusema ndio kwa kukutana na hapana kwa mzozo,ndio kwa kwa na mazungumzo na hapana kwa uhasama.

Papa alikuwa akizungumza baada ya marabi wa Kiyahudi, makadinali wa Kikristo na maimamu wa Kiislamu kukariri aya kutoka Agano la kale,agano jipya na Quran kwa lugha ya Kitaliana,Kingereza,Kiyahudi na Kiarabu katika tukio la kwanza lenye kujumuisha dini tafauti.

Katika hotuba yake nzito kwa lugha ya Kitaliana Papa Francis ametowa wito wa kuheshimiwa kwa makubaliano na kupinga vitendo vya uchokozi.Amesema yote hayo yanahitaji ushujaa, nguvu na un'gan'ganizi.

Wajibu kutafuta amani

Papa Francis akihutubia Vatican. (08.06.2014)

Papa Francis akihutubia Vatican. (08.06.2014)

Papa Francis ambaye alitowa mwaliko wa ghafla kwa viongozi hao wawili wakati wa ziara yake katika Ardhi Takatifu mwezi uliopita yaani Israel na Maeneo ya Wapalestina amesema kwamba juhudi za kutafuta amani ni hatua ya uwajibikaji mkubwa mbele ya ufahamu wetu na mbele ya watu wetu na kueleza kwamba mamilioni ya watu duniani kote wa imani za dini tafauti wanaiombea amani pamoja nao.

Huo ulikuwa mkutano wa kwanza wa hadhara kati ya marais hao wawili kufanyika baada ya zaidi ya mwaka mmoja na umefanyika ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja baada ya mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Marekani kusambaratika huku kila upande ukiilamu mwenzake.

Peres ambaye anatimiza miaka 90 na muda wake unamalizika mwezi ujao aliachana na hotuba aliyokuwa ameiandaa kwa Kingereza na Kihebrew kusema kwamba yeye ni mtu mzima aliayeshuhudia vita na kuonja amani na kwamba viongozi wote wanastahiki kuwapatia watoto mustakbali mwema.

Abbas ameomba Mungu awaletee amani ya haki na kamili kwa nchi yao na eneo hilo zima ili kwamba watu wa Mashariki ya Kati na dunia kwa jumla wafurahie matunda ya amani,utulivu na kuishi pamoja kwa maelewano.

Serikali ya muungano ya Wapalestina

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso.

Wakati huo huo Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barosso ameuambia mkutano wa usalama wa Israel makubaliano ya muungano wa Wapalestina na kundi la Hamas lazima yaungwe mkono.

Tamko lake hilo la jana limekuja siku chache tu baada serikali ya muungano ya Wapalestina yenye kuundwa na wataalmu huru wa kisiasa lakini inayoungwa mkono na Hamas kuapishwa hatua ambayo imekaribishwa na jumuiya ya kimataifa lakini imepingwa na Israel kama ni kikwazo kikuu cha amani.

Barroso amewaambia wajumbe katika mkutano huo unaofanyika kwenye mji wa mwambao wa Israel wa Herzliya kwamba kwa maslahi ya mustakbali wa makubaliano ya amani na uwakilishi halali wa serikali makubaliano ya usuluhishi baina ya Wapalestina yanapaswa kuungwa mkono.

Mwandishi : Mohamed Dahman

Reuters/AFP

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com