Pacquiao atania kuhusu ′Pacquiao-Mayweather 2′ | Michezo | DW | 15.11.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Manila

Pacquiao atania kuhusu 'Pacquiao-Mayweather 2'

Nyota wa mchezo wa masumbwi duniani, Manny Pacquiao amewatania mashabiki wake kuhusu uwezekano wa mechi ya marudiano kati yake na nyota mwenzake Floyd Mayweather.

Huku akiwa anatabasamu, ameonekana akionyesha nguo yenye picha yake na Mayweather kwenye kipande cha ndani au "lining" ya nguo hiyo. 

Pacquiao mwenye umri wa miaka 37 Jumatatu hii aliweka picha hiyo kupitia ukurasa wake wa Facebook, ikimuonyesha yeye mwenyewe akiwa amevaa nguo hiyo na picha yake ikiwa upande wa kulia wa koti la nguo hiyo, na Mayweather upande wa kushoto. 

"Umependa koti langu" Pacquiao aliyechaguliwa kuwa Seneta kwenye bunge la Ufilipino aliandika maneno hayo chini ya picha hiyo.

Picha hiyo ya Pacquiao iliyoangaliwa na mashabiki 215,000 kwenye mtandao wa Facebook siku moja baada ya kuituma imeamsha gumzo kuhusu marudiano ya mechi kati yake na Mayweather "Pacquiao-Mayweather 2"...

Kwenye mechi ya awali, Pacquiao alisema yuko tayari kulipiza kisasi baada ya kupoteza kwenye mchezo huo na Mayweather katika mpambano uliotajwa kuingiza fedha nyingi zaidi katika historia ya ndondi.

Sio tu mimi, lakini hata mashabiki wangu wanataka kurudiwa kwa mechi hiyo, sasa kwa nini isiwe? tunaweza kuzungumza kuhusu hilo, hamna tatizo, amesema Pacquiao. Promota wa bondia huyo Bob Arum amesema wiki iliyopita kwamba mechi hiyo inaweza kurudiwa. Nina uhakika wa asilimia 75, aliliambia shirika la habari za michezo la nchini Marekani, ESPN.

Hata hivyo kambi ya Pacquiao imesema mazungumzo hayo ya kurudiwa kwa mchezo huo yatasubiri. "masumbwi hayako kichwani mwake kwa sasa", Aquiles Zonio, ambaye ni msimamizi wa masuala ya mawasiliano ya umma wa Pacquiao ameliambia shirika la habari la AFP. "Amejikita kwenye shughuli za bunge." 

"Ifikapo January, tutajua ni lini kutakuwa na pambano jingine na nani atapambana nae." alisema Zonio.

Mwandishi: Lilian Mtono/ AFPE
Mhariri: Daniel Gakuba.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com