Ouattara ashinda uchaguzi wa Cote d′Ivoire | Matukio ya Afrika | DW | 28.10.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Ouattara ashinda uchaguzi wa Cote d'Ivoire

Rais wa Cote d'Ivoire Alassane Ouattara ameshinda kwa urahisi muhula mwingine wa uongozi katika uchaguzi ambao ni wa kwanza tangu uchaguzi uliozusha utata miaka mitano iliyopita

Kwa mujibu wa matokeo yaliyosomwa na Youssouf Bakayoko, mkuu wa tume ya uchaguzi, Ouattara alipata karibu asilimia 84 ya kura katika uchaguzi huo wa Jumapili, na kuushinda kabisa upinzani.

Alishinda kura nyingi katika majimbo yote isipokuwa moja tu kati ya 31 pamoja na mji mkubwa kabisa, Abidjan, na mji mkuu Yamoussoukro. Matokeo yanaonyesha alishinda kura zote isipokuwa 16 katika eneo lake la Kong, kaskazini mwa Cote d'Ivoire, ambako zaidi ya watu 14,000 walipiga kura. Ouattara alistahili kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura ili kuepuka duru ya pili. Bakayoko amesema matokeo hayo sasa yatawasilishwa kwa mahakama ya katiba ili kuidhinishwa.

Ouattara alipigiwa upatu mapema hata kabla ya kampeni kuanza. Wakati nchi ikisubiri matokeo rasmi hapo jana, rais huyo alisema uchaguzi huo umeiruhusu Cote d'Ivoire “kufungua ukurasa mpya na kuusahau mgogoro ambao nchi hiyo iliipitia” baada ya uchaguzi wa miaka mitano iliyopita.

Elfenbeinküste Wahlkampf Pascal Affi N'Guessan

Kiongozi wa upinzani Pascal Affi N’Guessan (kulia)

Katika kinyang'anyiro hicho, Ouattara alimpiku rais wa zamani Laurent Gbagbo katika duru ya pili lakini Gbagbo akakataa kujiuzulu, hali iliyosababisha machafuko yaliyowauwa zaidi ya watu 3,000 na kuendelea hadi kukakatwa kwa Gbagbo mnamo Aprili 11. Kesi ya Gbagbo ya makosa ya uhalifu dhidi ya binaadamu inatarajiwa kuanza mwezi ujao katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague ICC.

Mara hii Ouattara alipambana na upinzani uliogawika ambao ulishindwa kuwavutia wafuasi wengi. Alifanya kampeni kwa kuzingatia kuimarika uchumi wa nchi aliousimamia tangu alipochukua hatamu za uongozi Mei 2011, ijapokuwa wakosoaji wanasema wananchi wa kawaida wa Cote d'Ivoire hawajanufaika sana kutokana na ukuaji huo na kuwa maridhiano ya baada ya mgogoro uliokuwepo yamekuwa madogo mno.

Aliyemaliza katika nafasi ya pili na asilimia 9 ni Pascal Affi N'Guessan, mgombea wa chama cha kisiasa cha Gbagbo, Ivorian Popular Front. Kundi kubwa la chama hicho liliacha kumuunga mkono N'Guessan, likimwiita msaliti kwa Gbagbo na kubashiri kuwa kura hizo zingeibwa.

Idadi ya wapiga kura waliojitokeza ya zaidi ya asilimia 54 ilikuwa chini ya karibu asilimia 80 iliyosajiliwa katika duru ya kwanza ya mwaka wa 2010, ijapokuwa uchaguzi huo ulicheleweshwa kwa muda mrefu na kuwa wa ushindani mkali.

Rais wa Muungano wa Viongozi Wanawake wa Cote d'Ivoire na msemaji wa ujumbe wa waangalizi wa mashirika ya kiraia Mariam Dao Gabala anasema kupungua idadi hiyo huenda kuliashiria mazingira ya kisiasa yaliyobadilika pamoja na hofu ya uchaguzi kwa sababu ya kilichotokea mara ya mwisho.

Wakati wa kampeni, Ouattara aliapa kuyatatua matatizo kama vile ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana wakati akihimiza haki na maridhiano.

Mwandishi: Bruce Amani/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga

Matangazo

IJUE DW

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com