Oscar Pistorius aomba radhi kizimbani | Michezo | DW | 07.04.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Oscar Pistorius aomba radhi kizimbani

Huku akibubujikwa machozi, Oscar Pistorius alianza kutoa ushahidi katika kesi ya mauaji inayomkabili, kwa kuiomba msamaha familia ya mchumba wake ambaye alimpiga risasi na kumuuwa.

Mwanariadha huyo wa Olimpiki alieleza namna anavyosumbuka maishani tangu alipomuua Reeva Steenkamp mwaka jana na akaeleza namna anavyoandamwa na jinamizi ambalo humfanya kushtuka na kuamka usingizini kwa kunusa “harufu ya damu“.

Alisema kila siku anapoamka asubuhi, yeye huifikiria familia ya Steenkamp, na kuiombea kutokana na machungu aliyoisababishia. Alisema hakukusudia kuua, kwa sababu alikuwa akijaribu kumlinda mchumba wake.

Pistorius alimuua Steenkamp mwaka jana kwa kumpiga risasi kichwani, mkononi na nyonga kupita mlango wa choo nyumbani kwake. Waendesha mashitaka wanasema aliua makusudi baada ya kuzozana usiku wa Februari 14, 2013. Anakabiliwa na adhabu ya miaka 25 jela kama atapatikana na hatia ya kupanga mauwaji ya Steenkamp.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman