Ni ushindi wa wananchi asema kocha wa Cote D′Ivoire | Michezo | DW | 09.02.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Ni ushindi wa wananchi asema kocha wa Cote D'Ivoire

Kocha wa Tembo wa Cote D'Ivoire Herve Renard asema ushindi wa kombe la Afrika ni ushindi kwa wananchi. Rais wa Ghana awapa pole wachezaji wa kikosi cha nchi hiyo Black Stars.wa nchi hiyo .

Afrika Cup 2015 Elfenbeinküste vs. Algerien

Cote D'Ivoire mabingwa wa Afrika

Kwa mara nyingine tena , Tembo wa Cote D'Ivoire wamefanikiwa kuvishwa taji la ubingwa wa bara la Afrika mwaka 2015 nchini Guinea ya Ikweta jana Jumapili na kusababisha Ghana kurejea nyumbani mikono mitupu , kama ilivyotokea mwaka 1992 nchini Senegal ambapo timu hizo zilifikia fainali na Cote D'Ivoire iliibuka tena mshindi kwa mikwaju ya penalti 11-10.

Fußball Afrika Cup Elfenbeinküste vs. Ghana

Pambano kati ya Cote D'Ivoire na Ghana

Kocha wa Cote D'Ivoire Herve Renard amesema ushindi huu wa kombe la bara la Afrika ni ushindi kwa wananchi wa Cote D'Ivoire.Kocha huyo Mfaransa ambaye aliiongoza Zambia kupata ushindi wake wa kwanza wa kombe hilo kwa mikwaju ya penalti katika fainali dhidi ya Cote D'Ivoire mwaka 2012 amesema watu wa Cote D'Ivoire ndio washindi. Ushindi wa Renard na Cote D'Ivoire pamoja na Zambia unamfanya kocha huyo kuwa wa kwanza kushinda kombe hilo akiwa na timu tofauti za taifa barani humo.

Kabla ya pambano hilo lililokuwa la kuvutia shabiki wa Ghana Nana Fredua amesema mara hii ni Ghana itakayotoka kifua mbele.

"Hii ni kama marudio ya historia . Mwaka 1992 nchini Senegal pia tulipambana na Cote D'Ivoire , wakati huo walishinda. Mara hii hawatatuweza."

Afrika 2015 Africa Cup of Nations (Andre Ayew)

Nahodha wa Ghana Andre Ayew akilia kwa uchungu baada ya kushindwa

Baada ya Cote D'Ivoire kukosa penalti zao mbili za mwanzo , mshambuliaji Gervinho alikata taama ya kuishinda Ghana katika fainali mara hii ya kombe la Afrika. Baada ya kuwa nyuma kwa mabao mawili,nilikaa na kuupa mgongo mchezo huo ," amesema Gervinho alipozungumza na waandishi habari.

Pengine hatua hiyo ilituletea bahati." Iwe bahati ama ufundi , wenzake waliweza kufunga mikwaju yao nane ya penalti kabla ya juhudi za mlinda mlango wa Ghana Razak Braimah kupanguliwa na mlinda mlango mwenzake Boubacar Barry na kutayarisha nafasi ya ushindi, ambayo mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 35 aliitumia na kuandika ushindi wa pili wa Tembo hao wa Cote D'Ivoire. Nahodha wa Cote D'Ivoire Yaya Toure amesema yalikuwa ni maajabu.

"Ni kitu ambacho huwezi kuamini. Nimeusubiri sana ushindi huu. Niko karibu miaka nane katika timu ya taifa . Mara mbili nilishindwa katika fainali."

Fußball Afrika Cup 2015 Kongo vs. Elfenbeinküste 4.2.2015

Kikosi cha Cote D'Ivoire

Mashindano haya yalihamishiwa nchini Guinea ya Ikweta kwa kuwa wenyeji wa mashindano hayo wa hapo awali Morocco walitaka mashindano haya yaahirishwe kutokana na matatizo ya ugonjwa wa Ebola katika nchi jirani za Liberia, Guinea na Sierra Leone.

Lakini shirikisho la kandanda barani Afrika CAF lilikataa ombi hilo la Morocco na Guinea ya Ikweta katika dakika za mwisho ilikubali kuwa mwenyeji wa dharura wa mashindano haya. Na hakika walifanya kazi nzuri kwa muda mfupi wa miezi miwili kama anavyosema mchezaji wa zamani wa Mali Frederick Kanoute .

"Nafikiri Guinea ya Ikweta imefanya kazi nzuri kabisa, kwakuwa ilikuwa na muda mfupi wa kutayarisha mashindano haya ya Afrika. Pamoja na hayo ni bahati mbaya kwamba kumetokea mambo ambayo si mazuri. Ni lazima kutafakari kwamba mambo kama hayo hayatokei tena."

Fußball Bundesliga VfL Wolfsburg vs. TSG 1899 Hoffenheim

Kikosi cha Wolfsburg kinaelekea kucheza champions league

Rais wa Ghana John Dramani Mahama ametuma ujumbe kwa wachezaji wa kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo Black Stars na kuwapongeza kwa kuonesha mchezo mzuri , licha ya kushindwa. Mmevuka matarajio yetu , kutoka sifuri hadi kuwa mashujaa. Ninajivunia kuwa mmoja wenu," ameandika katika ukurasa wake wa Twitter. Mashabiki wa Ghana hata hivyo walibaki wamevunjika moyo kwa kushindwa kama anavyoeleza Nana fredua aliyekuwapo uwanjani mjini Bata jana.

"Tulipata nafasi nyingi, lakini hatimaye huu ni mchezo tu. Tumeshindwa, kwa hiyo tutajaribu tena mara nyingine."

Mbali ya taarifa za kutia moyo katika soka la Afrika , lakini kuna pia taarifa za kusikitisha , ambapo nchini Misri ligi ya nchi hiyo imeahirishwa baada ya watu 22 kuuwawa katika ghasia za hivi karibuni kabisa kati ya mashabiki na polisi, maafisa wamesema hii leo.

Mashabiki wa soka nchini Misri wamekuwa mara kwa mara wakihusika katika ghasia za kisiasa nchini humo na ghasia za jana Jumapili zinazusha hofu za mapambano zaidi katika siku zijazo.

Mashabiki wafariki Misri

Ghasia hizo ambazo ni kama zilizosababisha zaidi ya watu 70 kuuwawa baada ya mchezo wa ligi mjini Port Said mwaka 2012, zilizuka wakati maelfu ya mashabiki waliojaribu kulazimisha kuingia katika uwanja mjini Cairo kuangalia pambano , na kusababisha mtafaruku wakati polisi walipofyatua mabomu ya kutoa machozi na risasi dhidi ya mashabiki.

Maafisa wa hospitali wamesema wahanga wote waliuwawa katika mkanyagano, ambapo wengine walivunjia shingo.

Na sasa katika ligi ya Ujerumani Bundesliga , viongozi wa ligi hiyo Bayern Munich hawakuwa katika kiwango chao cha juu lakini walifanya vya kutosha kuisambaratisha VFB Stuttgart kwa mabao 2-0, ambapo mshambuliaji Arjen Robben na mlinzi David Alaba walifunga mabao hayo muhimu. Ushindi huo wa kwanza wa Bayern katika mwaka huu umeiweka timu hiyo pointi nane juu ya timu inayofuatia VFL Wolfsburg ambayo imeendelea kuonesha umahiri wake kwa kuishinda Hoffenheim kwa mabao 3-0.

Bundesliga VfB Stuttgart 05 vs FC Bayern 07.02.2015

Mlinzi wa Bayern Munich David Alaba

Schalke 04 ilifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Borussia Moenchengladbach , na makamu bingwa wa msimu uliopita Borussia Dortmund nayo iliona mwezi baada ya kupata ushindi wa kwanza mnono msimu huu wa mabao 3-0 dhidi ya Freiburg na kuwainua kutoka mkiani kabisa mwa ligi hadi nafasi ya 16 , kama mlinzi Marcel Schmelzer anavyoeleza nini kilibadilika siku hiyo.

"Bila shaka , tangu mwanzo hadi mwisho tuliweza kutumia mpango wetu, kwamba tulikuwa makini katika ulinzi na mbele tuliweza kupata bao la kuongoza. Hilo kwetu lilikuwa muhimu, kwamba tupate bao la kuongoza haraka, ili tuweze kupata hisia na sio kila mara kufungwa bao. Kuanzia hapo , leo ndio ufunguo wa mafanikio."

Lakini sio Borussia Dortmund pekee iliyoonesha kufufuka, lakini pia Werder Bremen ambayo jana ilpata ushindi wake wa tatu mfululizo , kwa kuishinda Bayer Leverkusen kwa mabao 2-1 na kuwashangaza wadadi wa masuala ya soka nchini Ujerumani, kama anavyosema kocha wa Leverkusen Roger Schmidt kwamba walishindwa kuuvusha mpira katika msitari wa mwisho.

Bundesliga Freiburg vs Dortmund 07.02.2015 Aubameyang

Borussia Dortmund wakifurahia ushindi

"Kwa mara nyingine tena tumekuwa na mchezo , ambao tungeweza kubadilisha matokeo ama ni lazima tubadilishe matokeo, lakini tumeshindwa kuuingiza mpira wavuni. Hali hii inatufuata kiasi katika msimu huu."

Premier League

Katika ligi ya Uingereza , Premier League Manchester City inalazimika kushinda michezo yake yote iliyobaki ili kuweza kuwa na nafasi ya kutetea taji lao. Ikiwa imezidiwa pointi saba zinazoitenganisha timu hiyo na viongozi wa Premier League Chelsea , mabingwa watetezi Manchester City wanaamini kwamba ni uchezaji bora tu katika michezo yake 14 iliyobakia itawapa nafasi ya kupambana kurejesha taji hilo.

Machester City inajitayarisha kupambana na Stoke City siku ya Jumatano, wakati Arsenal itajaribu kurudisha imani kwa mashabiki wake kesho Jumanne watakapotiana kifuani na Lescester City uwanjani Emarate.

Mlinzi wa Liverpool Martin Skrtel anategemea safu ya ulinzi ya kikosi hicho cha Wekundu kuimarika na kusaidia kutuliza safu ya ushambuliaji ya Tottenham Hotspurs wakati mahasimu hao watakapokuwa wakiwania nafasi ya nne katika ligi hiyo watakapokutana uwanjani Anfield kesho Jumanne

Dani Alves, Neymar , Leo Messi FC Barcelona gegen Atletico Madrid

Wachezaji wa Barcelona

Nchini Uhispania, Barcelona wanacheza kwa mitindo ambayo inaashiria huenda wanaonyesha kuimarika katika wakati muafaka na watataka kuhamishia hali hiyo kupata nafasi katika fainali ya kombe la mfalme siku ya Jumatano.

Mabingwa hao mara 26 katika vikombe vya ndani, Barca wanaingia katika pambano lao la nusu fainali , mchezo wa kwanza nyumbani kwa Villareal baada ya kuirarua jana Jumapili Athletico Bilbao kwa mabao 5-2, ushindi uliowanyanyua hadi pointi moja nyuma ya viongozi wa ligi hiyo Real Madrid ambao walisambaratishwa siku ya Jumamosi kwa kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya Atletico Madrid.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / rtre / afpe / dpae

Mhariri : Mohammed Abdul Rahman / Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com