Ni nani atacheza Ulaya na nani ataiaga Bundesliga? | Michezo | DW | 05.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Ni nani atacheza Ulaya na nani ataiaga Bundesliga?

Baada ya kukamilika mechi za siku ya 33 katika Bundesliga, ilidhihirika kuwa vita vya kutaka kuepuka kushushwa daraja na vile vya kutaka kucheza soka la Ulaya vitaamuliwa katika siku ya mwisho kabisa ya ligi.

Vita vya kuamua ni nani atakayetimuliwa katika Bundesliga vitaamuliwa siku ya mwisho baada ya Hamburg, Nuremberg na Eintracht Braunschweig kushindwa mechi zao. Nuremberg walihitaji ushindi dhidi ya Hannover ili kupata nafasi ya kuwapokonya nafasi Hamburg katika mechi za mchujo. Lakini mambo hayakwenda vyema baada ya kuonjeshwa magoli mawili kwa sifuri.

Na kwa bahati nzuri kwa Nuremberg, Hamburg pia walipata kichapo na kuliwacha pengo baina yao kusalia kuwa pointi moja. Bayern Munich ilihitaji kitu cha kuwasaidia kusahau masaibu ya Champions League, na hivyo wakawachabanga Hamburg magoli manne kwa moja. Kocha wa Hamburg Mirko Slomka aliwachwa kinywa wazi baada ya kichapo hicho.

Borussia Mönchengladbach iliwaongezea mbinyo Wolfsburg kabla ya siku ya mwisho

Borussia Mönchengladbach iliwaongezea mbinyo Wolfsburg kabla ya siku ya mwisho

Mchuano mwingine uliokuwa na umuhimu mkubwa ulikuwa kati ya washika mkia Braunschweig na Augsburg. Wakati matokeo yalipoendelea kuwa sifuri kwa sifuri, mashabiki wa nyumbani walifahamu kuwa goli moja lingewapeleka juu ya Hamburg na Nuremberg hadi awamu ya mechi za mchujo. Lakini mambo yakageuka na hilo bao likafungwa na wageni Augsburg. Baada ya mechi, kocha wa Brauschweig alionekana kuvunjika moyo Torsten Lieberknecht

Wakati huo huo, Robert Lewandowski aliwaaga mashabiki wa timu yake inayoshikilia nafasi ya pili Borussia Dortmund kabla ya kuhamia klabu ya Bayern Munich msimu ujao. Na alifanya hivyo baada ya timu yake kusajili ushindi wa magoli matatu kwa mawili dhidi ya Hoffenheim.

Wolfsburg waliuanza mchezo wakiwa pointi moja nyuma ya Leverkusen katika nafasi ya kufuzu katika Champions League, huku wenyeji wao STUTTGART wakitafuta tu point moja ili kujiondoa eneo la hatari. Licha ya hayo walishindwa magoli mawili kwa moja.

Kwa kushinda mechi zake mbili za mwisho, Borussia Moenchengladbach inaweza kuzipiku Bayer Leverkusen na Wolfsburg, ili kufuzu katika Champions League katika siku ya mwisho ya msimu. Gladbach waliweza kuwafunga Mainz magoli matatu kwa moja, lakini pia walimuaga mlinda lango Marc-André ter Stegen anayeelekea Barcelona msimu ujao.

Leverkusen katika nafasi ya nne, wanahitaji ushindi katika mechi zao mbili za mwisho ili kujihakikishia soka la Champions League msimu ujao. Na jumamosi walifaulu kuwanyamazisha Frankfurt magoli mawili kwa bila.

Schalke ilihitaji ushindi ili kuizuia Leverkusen kuikaribia na kuhujumu tikiti yao ya kufuzu moja kwa moja katika Champions League na hilo walifaulu baada ya kuizaba Freiburg magoli mawili kwa bila. Katika mechi nyingine ambayo haikuwa na umuhimu, Werder Bremen waliwafunga Hertha Berlin magoli mawili kwa bila.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com