1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

New Zealand yatangaza kutokomeza virusi vya corona

Sylvia Mwehozi
8 Juni 2020

Waziri mkuu wa New Zealand Jacinda Arden ametangaza kwamba taifa hilo, limefanikiwa kuutokomeza ugonjwa wa virusi vya corona na itaondoa hatua zote za kukabiliana na maambukizi isipokuwa tu udhibiti wa mipaka.

https://p.dw.com/p/3dQQY
Neuseeland Coronavirus Jacinda Ardern
Picha: Getty Images

Waziri mkuu Ardern ametangaza kwamba shughuli zote za umma na binafsi, biashara, utalii na usafiri wa umma sasa vinarejea kama kawaida bila ya kuzingatia suala la kukaa umbali kati ya mtu na mtu. New Zealand iliyo na wakaazi karibu milioni tano imetangaza kuondokana na janga hilo wakati mataifa mengine yaliyo na nguvu kiuchumi ikiwemo Brazil, India, Uingereza na Marekani zikipambana kukabiliana na kuenea kwa virusi hivyo. Waziri mkuu Ardern amewaeleza waandishi wa habari kuwa;

"Leo hii hakuna kesi yoyote nchini New Zealand. Tumepima karibu watu 40,000 dhidi ya COVID-19 katika siku 17 zilizopita na hakuna aliyekuwa na maambukizi. Hatuna mgonjwa hospitali wa COVID-19 kwa siku 12. Zimepita siku 40 tangu kesi ya mwisho ya maambukizi katika jamii, siku 22 tangu mtu huyo amalize hatua za kujitenga," alisema Waziri Mkuu Ardern.

Südafrika Lockerungen nach Lockdown
Mwanafunzi wa Afrika Kusini akitakasa mikono yake kabla ya kuingia shuleniPicha: AFP/M. Longari

Kulingana na waziri mkuu Ardern, New Zealand imeweza kufikia mafaniko hayo kutokana na siku 75 za vizuizi ambapo biashara kubwa zilifungwa na watu wote isipokuwa wafanyakazi katika sekta muhimu walitakiwa kubakia ndani. Hata hivyo udhibiti wa mipaka utaendelea kuzingatiwa na kila mmoja anayeingia nchini humo atapimwa. Taifa hilo liliripoti visa 1,154 vya maambukizi ya COVID-19 na vifo 22. Kutokana na tangazohilo, mchezo wa Rugby utarejea tena mwishoni mwa juma na mashabiki wataruhusiwa kuingia viwanjani.

Nchini Marekani macho yote yameelekezwa katika jiji la New York, linalofahamika kuwa na shughuli nyingi na ambalo limekuwa chini ya vizuizi tangu mwezi Machi. Kuanzia Jumatatu, New York inaanza kuondoa taratibu vizuizi hivyo ambapo shughuli za ujenzi, viwanda, biashara zitafunguliwa tena.

BdTD New York Corona-Beschränkungen gelockert | Social Distancing im Park
Tunazingatia umbali kati ya mtu na mtu. Hapa ni jijini New YorkPicha: Reuters/E. Munoz

New York ilikuwa kitovu cha maambukizi ya kirusi cha corona nchini Marekani na kwa ujumla zaidi ya watu 21,000 ndani ya jiji hilo walifariki kutokana na COVID-19.

Nchini Afrika Kusini wanafunzi wameanza kurejea madarasani hii leo kama sehemu ya mpango wa kuondoa taratibu vizuizi vilivyowekwa kwa miezi kadhaa. Kufunguliwa kwa shule kulicheleweshwa baada ya muungano wa vyama vya walimu kuwataka wafanyakazi wa shule kukaidi amri ya serikali wiki iliyopita, wakidai kwamba shule hazikuwa na hatua za kutosha za kiafya na usafi kuweza kuwalinda walimu na wanafunzi. Afrika Kusini imerekodi visa 50,000 huku vifo vikifikia karibu 1000. Hadi kufikia sasa zaidi ya watu 400,000 duniani kote wamepoteza maisha na wengine zaidi ya milioni 7 wakiambukizwa COVID-19.