1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nchi za Afrika zatakiwa kulinda haki za binaadamu

Admin.WagnerD28 Februari 2022

Makamu wa Rais wa Nigeria Yemi Osinanjo, amezindua  mkutano wa 64 wa mwaka wa mahakama, katika Mahakama ya Afrika inayoshughulika na haki za binadamu iliyopo Arusha Tanzania.

https://p.dw.com/p/47jPE
Tansania African Court of Human and people's Rights
Picha: DW/N. Natalis

amezitolea mwito nchi Afrika kuheshimu haki za binadamu na utawawa wa kisheria akisema kuwa Afrika inalo jukumu la kulinda raia wake katika masuala mbali mbali yanayohusu haki za binadamu. 

Katika mkutano huo, Makamu  wa Rais  wa Nigeria ambaye alimwakilisha Rais wa nchi hiyo  Muhammadu Buhari, amesema yapo matendo ambayo yanashuhudiwa katika nchi za Afrika ambayo yanakwenda kinyume na haki za binadamu na utawala wa kisheria na hivyo ili kuwa na Afrika yenye nguvu na umoja, ni sharti serikali za nchi za Afrika zihakikishe zinayatokomeza. Ametolea mfano masuala ya ulinzi wa haki za kuishi za watu hasa wanaoishi maeneo ya wanyamapori, umaskini uliokithiri, njaa na magonjwa yanayoendelea kuwauwa hasa watoto. Pia amegusia suala la mabadiliko ya tabia nchi na kuzitolea mwito hasa nchi za magharibi kuwepo mipango madhubuti ya kukabiliana na athari zake  kwani Afrika  ndio inayoathirika zaidi. 

" Mchango wa Afrika wa kusababisha mabadiliko ya tabia nchi ni mdogo sana lakini ndio inayoathirika zaidi. Huu ni wito kwa nchi za Magharibi kuendelea kulishughulikia aatizo hili lakini kwa nchi za Afrika kuwa na mpango ya pamoja ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi.” 

Kwa upande wake waziri mkuu wa Tanzania Kasimu Majaliwa aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan ametoa mwito kwa nchi za Afrika ambazo bado hazijajiunga na itifaki ya mahakama hiyo kufanya hivyo, huku akisisitiza mahakama hiyo kutokwenda kinyume na sheria za nchi husika.  "Ninafahamu utendaji kazi wa mahakama wakati mwingine haupo huru kukosolewa, hii imesababisha hata baadhi ya nchi kujitoa. Hii ni ishara ya wazi kwa mahakama kwamba katika utekelezaji wa majukumu yake isivunje uaminifu wake kwa nchi wanachama.” 

Ikumbukwe kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi nne zilizojotoa katika itifaki ya mahakama hiyo inayoruhusu watu na mashirika binafsi kupeleka kesi katika mahakama hiyo zinahusu masuala ya haki za binadamu jambo lililozua mjadala kama Taifa hilo la Afrika Mashariki linakwepa uwajibikaji kuhusu ulinzi wa haki za binadamu kwa raia wake au la. Mahakama hiyo ambayo kwa sasa inaongozwa na jaji mwanamke raia wa Tanzania Imani Aboud, ilianzishwa kwa lengo la kutetea na kulinda haki za binadamu Afrika, ambapo hata hivyo mpaka sasa inakabiliwa na changamoto ya kutotekelezwa kwa maamuzi yake. Kauli mbiu ya uzinduzi wa mwaka huu wa Mahakam ni mahakama ya Afrika na Afrika tunayoitaka. 

Mwandishi: Veronica Natalis DW, Arusha