Nani atakayevaa viatu vya Lahm? | Michezo | DW | 04.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Nani atakayevaa viatu vya Lahm?

Baada ya nahodha wa timu ya Ujerumani Philipp Lahm kustaafu kutoka soka la Kimataifa, mrithi wa nafasi yake ya beki wa kulia ni lazima apatikane. Hilo ndilo suala analopaswa kulitafutia ufumbuzi kocha Joachim Löw

Hilo huenda likatatuliwa katika msimu ujao wa Bundesliga, ambapo wagombea kadhaa wataweza kujitokeza.Siyo rahisi kwa Ujerumani kulijaza pengo la Lahm. Wala siyo rahisi hata kwa nchi nyingine yoyote. Ujasiri, ushujaa na uongozi ambao Lahm alileta katika Die Mannschaft ulikuwa wa kipekee.

Huku Bastian Schweinsteiger akiwa mstari wa mbele kwa wale wanaoweza kupewa unahodha wa kikosi, pengo la Lahm lazima lijazwe na mtu mwenye ujuzi mkubwa wa kiufundi kama wake. Miongoni mwa majina yanayopigiwa darubini ni Sebastian Jung wa VfL Wolfsburg, Kevin Grosskreutz wa Borussia Dortmund, Oliver Sorg wa Freiburg, Christian Träsch wa Wolfsburg, na Andreas Beck wa Hoffenheim.

Licha ya majina hayo yote, uthabiti wa Löw hauwezi kusahaulika. Wakati mmoja alisifiwa kwa kuwa msumbufu sana, lakini Löw ndiye aliyekuwa na kicheko cha mwisho nchini Brazil baada ya uongozi wake wa kihafidhina kuipa Ujerumani Kombe la nne la Dunia. Hata wakati kukiwa na mabadiliko ya kufanywa hapo mbeleni, Löw lazima awe makini, mazoea yake ya karibuni ya kuwa na safu ya ulinzi yenye mabeki wa kati, yana maana kuwa Jerome Boateng huenda akawekwa upande wa kulia, na kuwacha nafasi ya beki mwingine wa kati (wakati wa Holger Badstuber kurejea tena kikosini?)

Hata hivyo, baada ya Boateng kucheza vyema katika katikati ya ulinzi, Benedikt Höwedes na Mats Hummels ndiyo sura ya safu ya ulinzi ya Ujerumani, na nafasi ya beki wa kulia bado iko wazi. Na Löw ana msimu mzima wa kuamua ni nani atakayekuwa mshindi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohamed Khelef