1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwili wa Kiptum wasafirishwa kwa mazishi

23 Februari 2024

Wakenya waomboleza kifo cha mshikiliji wa rekodi ya dunia ya mbio za masafa marefu Kiptum wakati mwili wake ukipelekwa nyumbani.

https://p.dw.com/p/4cktf
USA Chigaco
Kevin Kiptum mwanariadha wa Kenya baada ya kuandisha rekodi ya dunia katika mbio za masafa marefu Chicago.Picha: KAMIL KRZACZYNSKI/AFP/Getty Images

Mamia ya Wakenya wametoa heshima zao wakati mwili wa mwanariadha aliyeshikilia rekodi ya dunia ya mbio za marathon Kelvin Kiptum, ambaye alikuwa na ndoto ya kuvunja kizuizi cha kukimbia kwa saa mbili, ukipelekwa kijijini kwao kwa mazishi.

Kiptum, 24, na kocha wake Gervais Hakizimana waliaga dunia mapema mwezi huu wakati mkimbiaji huyo alipopoteza udhibiti wa gari alilokuwa akiendesha katika Bonde la Ufa na kugonga mti.

Soma pia:Kiptum atahadharishwa baada ya kuvunja rekodi ya dunia

Ripoti ya daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa mwanariadha huyo amesema alifariki kutokana na majeraha ya kichwa kutokana na ajali hiyo.

Huku wakiimba nyimbo za dini na kushikana mikono, waombolezaji waliandamana na msafara uliokuwa umebeba jeneza la Kiptum lilipambwa kwa maua wakati likiondoka katika chumba cha kuhifadhia maiti katika mji wa Eldoret, magharibi mwa Kenya.

Jeneza hilo lilifunguliwa ili kuwaruhusu waombolezaji kuutazama mwili wa mwenda zake katika mji mkuu wa eneo hilo kabla ya kuelekea katika kijiji cha Chepsamo.

Babake Kiptum alimshikilia mtoto wa kiume wa marehemu mwenye umri wa miaka 7, huku mshikiliaji wa rekodi ya dunia ya mita 1,500 kwa wanawake, Faith Kipyegon kwa huzuni akifunika uso wake kwa mikono.

Mafanikio katika muda mfupi

USA Chigaco
Kelvin Kiptum akisherehekea baada ya kushinda Marathon Chicago.Picha: KAMIL KRZACZYNSKI/AFP/Getty Images

 

 

Kiptum alikuwa ameshiriki mbio za masafa marefu mara tatu pekee lakini kila moja ilikuwa kati ya mbio mara saba za kasi zaidi kuwahi kurekodiwa. Aliweka rekodi ya dunia katika mbio za Chicago Marathon mwezi Oktoba kwa saa mbili na sekunde 35, na kuvuka 2:01:09 iliyowekwa na Eliud Kipchoge mnamo 2022.

Kiptum alitarajia kuvunja rekodi kwa kutimka kwa saa mbili mjini Rotterdam mwezi Aprili na pia alitarajiwa kushiriki kwa mara ya kwanza katika Olimpiki mjini Paris mwaka huu katika mbio ambazo angeweza kushindana kwa mara ya kwanza na Kipchoge.

Jeneza hilo litasafirishwa takriban kilomita 80 (maili 50) kutoka Eldoret hadi Chepsamo, ambapo Kiptum alifanya kazi kama mchungaji wa mifugo kabla ya kuwa mkimbiaji kitaaluma. Atazikwa siku ya Ijumaa ya tarehe 23.02.2024.

Kiptum ameacha mke wake, mwanawe wa kiume mwenye umri wa miaka saba na bintiye wa miaka sita. Rais wa Kenya William Ruto aliagiza nyumba kujengwa kwa ajili ya familia hiyo.

Kocha wake Hakizimana alizikwa siku ya Jumatano nchini kwao Rwanda.