Iran yamkamata kiongozi wa waasi.
23 Februari 2010Maafisa wa Iran wamearifu kuwa wamemkamata kiongozi wa wanaitikadi kali wa kisunni wakati akiwa ndani ya ndege .
Mtu huyo Abdolmalek Rigi anaongoza kundi la wapiganaji wa Jundallah-yaani askari wa Mungu.
Iran inasema ilimkamata Abdolmalik Rigi saa 24 baada kuwapo kwenye kituo cha kijeshi cha Marekani nchini Afghanistan.
Iran imesema kukamatwa kwa mtu huyo ambae ni kiongozi wa wanaitikadi kali wa kisunni ni pigo kwa maadui wake wakubwa wa magharibi.
Waziri wa upelelezi wa Iran bwana Heydar Moslehi anadai kwamba Marekani ilimpa Rigi pasipoti ya kiafghani na kwamba alifika hadi Ulaya na kukutana na mkuu wa kijeshi wa NATO.
Lakini Marekani imekanusha madai hayo na kuyaita kuwa ni uzushi.
Katika orodha ya watu wanaotafutwa na Iran, Abdolmalek Rigi alikuwa katika nafasi ya kwanza.
Kiongozi huyo wa kundi la waasi linaloitwa Jundallah yaani askari wa Mungu amekuwa anapelembwa kwa muda wa miezi mitano kabla ya kukamatwa .
Iran inadai kwamba Rigi amekuwa anaongoza mashambulio dhidi ya nchi hiyo kutokea Pakistan.
Shirika la habari ,la Iran limemkariri waziri wa upelelezi bwana Moslehi akisema kuwa Abdolmalek Rigi alikamatwa ndani ya ndege iliyokuwa inaelekea Kyrgyzstan kutokea Dubai.
Waziri Moslehi amesema kukamatwa kwa kiongozi huyo wa kundi la wanaitikadi kali wa kisunni, ni kashfa kubwa kwa Dubai.Ameeleza kuwa mkasa huo unaonyesha jinsi Israel inavyozitumia Marekani na nchi za Ulaya kwa lengo la kuligeuza eneo la nchi za kiarabu kuwa maficho ya magaidi.
Iran imekuwa inamsaka Rigi kwa miaka kadhaa ambae inadai ana uhusiano na idara za ujasusi za Pakistan, Uingereza na Marekani.
Abdomalik Rigi anadaiwa kufanya mashambulio katika jimbo la Sistan-Baluchistan linalopakana na Afghanistan na Pakistan, njia kubwa ya mihadarati.
Jimbo la Sistan Baluchistan ni maskani ya idadi kubwa ya wasunni na ni jiko la upinzani dhidi ya watawala wa kishia wa Iran.
Kundi la Abdolmalik Rigi, Jundallah lilidai kuwa lilifanya shambulio la kujitoa mhanga katika mji Pisheen ambapo watu 42 waliuawa ikiwa pamoja na walinzi saba wa mapinduzi ya Iran na viongozi kadhaa wa makabila Shambulio hilo lilifanyika mwezi oktoba mwaka jana.
Kundi hilo pia lilidai kuwa lilifanya shambulio la bomu mwezi mei mwaka jana, kwenye msikiti wa washia Amir al-Momenin katika mji wa Zahedan nchini Iran.
Watu 20 waliuawa na hamsini walijeruhiwa.
Maafisa wa Iran wamesema Rigi mara kwa mara alikuwa anavuka mpaka kutoka Pakistan na kuingia Iran ili kuongoza mashambulio katika jimbo la Sistan- Baluchistan ndani ya Iran.
Iran pia imemtia ndani Mohammed Ali Jafari nduguye Abdolmalik ambae amewekwa katika orodha ya watu wanaosubiri adhabu ya kifo.Abdolmaliki pia amesema kundi la Jundallah lilipewa amri kutoka Marekani , za kufanya mashambulio ndani ya Iran. Amesema kundi hilo lilianzishwa na linagharimiwa na Marekani.
Mwandishi/Mtullya Abdu/AFPE/RTRE/
Mhariri/Abdul-Rahman