Mwanaharakati Rupert Neudeck amefariki | Matukio ya Kisiasa | DW | 31.05.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mwanaharakati Rupert Neudeck amefariki

Mwanzilishi mwenzi wa shirika la misaada, Cap Anamur Rupert Neudeck aliewasaidia watu katika sehemu mbalimbali za dunia amefariki baada ya kufanyiwa upasuaji wa moyo mjini Berlin

Deutschland Berlin Rupert Neudeck

Mwanzilishi wa shirika la misaada "Cap Anamur",Rupert Neudeck afariki

Marehemu huyo atakumbukwa hasa kwa mchango alioutoa katika kuwasaidia wakimbizi wa Vietnam.

Hayati Neudeck ambae pia alikuwa mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu alianzisha kamati iliyoitwa "Meli kwa ajili ya Vietnam" mnamo mwaka wa 1979 kwa msaada wa mwandishi maarufu wa riwaya wa Ujerumani Heinrich Böll. Ni katika wakati huo ambapo jina la mwanaharakati huyo lilianza kujulikana duniani kote.

Meli hiyo Cap Anamur iliyaokoa maisha ya wakimbizi zaidi ya 11,000 wa Vietnam kwenye bahari ya China hadi mwaka 1982. Rupert Neudeck alianzisha juhudi za kuwasaidia wakimbizi wa Vietnam pamoja na mkewe Christel.

Katika miaka iliyofuatia shirika hilo la Cap Anamur lilipanuza shughuli zake katika nyanja nyingine za kijamii. Mnamo mwaka wa 2002 mwanaharakati huyo alianzisha shirika la "kofia za kijani" ambapo mafundi vijana walijiwajibisha kwa muda wa miezi kadhaa kujenga nyumba,vijiji au mobomba ya maji yaliyoharibika katika sehemu za migogoro.

Msamaria mwema huyo alizaliwa mnamo mwaka wa 1939 katika mji wa Gdansk ambao leo ni sehemu ya Poland. Alisomea,fasihi na lugha ya kijerumani, elimu ya jamii,taaluma ya dini na falsafa ,kwenye vyuo vya Bonn, Münster na Salzburg. Kuanzia miaka ya sabini alianza kufanya kazi ya uandishi wa habari.

Umaarufu wajengeka

Neudeck kwenye meli ya Cap Anamur

Neudeck kwenye meli ya Cap Anamur

Lakini umaarufu wa Rupert Neudeck ulitokana na kuwa mwanzilishi mwenzi wa shirika la misaada la Cap Anamur. Yeye mwenyewe alikuwa mkimbizi wakati alipokuwa mtoto. Alinusurika kifo wakati meli ya "Wilhelm Gustloff" iliyokuwa inawasafirisha kutoka mashariki kuzamishwa na kombora la manowari ya Urusi.

Rupert aliratibisha shughuli zake kutokea nyumbani kwake. Aliwasiliana na wanaharakati wenzake wa shirika la misaada waliokuwa wanafanya kazi za kutoa misaada barani Afrika na katika sehemu zingine za dunia.

Rupert Neudeck alikuwa nyumbani popote alipokuwapo,iwe miongoni mwa Wakurdi katika nchini Uturuki au Bosnia. Na alikuwapo pale ambapo palikuwapo na tatizo.Baadae alisema kwa mzaa kwamba alikuwa msafirishaji watu kinyume na sheria.Sababu ni kwamba hakuweza kuvumilia kuona watu wanakufa.Hakusubiri itifaki za kiserikali. Alitaka kusaidia mara moja.

Mwandishi: Wagener ,Volker.

Mfasiri: Mtullya Abdu.

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com