Mwaka Mpya 2016 wakaribishwa licha ya khofu za ugaidi | Masuala ya Jamii | DW | 01.01.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Mwaka Mpya 2016 wakaribishwa licha ya khofu za ugaidi

Mamilioni ya watu ulimwenguni wameukaribisha mwaka mpya kwa mchanganyiko wa matumiani, khofu na kumbukumbu za namna mwaka 2015 ulivyoinamiwa na matukio mengi mabaya yakiwemo ya ugaidi.

Sherehe za kuupokea mwaka mpya mjini Jakarta, Indonesia.

Sherehe za kuupokea mwaka mpya mjini Jakarta, Indonesia.

Nchini Ujerumani, polisi iliwaonya watu kukaa mbali na vituo vya treni na kujiepusha na mikusanyiko mikubwa baada ya kile walichosema ni "ishara za njama za mashambulizi ya kigaidi" yaliyopangwa na kundi linalojiita Dola la Kiislamu katika mji wa kusini wa Munich.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Bavaria, Joachim Herrmann, aliwaambia waandishi wa habari kwamba polisi ilikuwa imepokea "taarifa za uhakika" kuwa mashambulizi hayo yalipangwa kufanyika kwenye sherehe za Mkesha wa Mwaka Mpya.

Mkuu wa polisi wa Munich, Hubertus Andrae alisema mamlaka nchini Ujerumani zilipewa taarifa hizo na shirika moja la kijasusi la nchi ya kigeni kwamba magaidi wa Dola la Kiislamu walikuwa wanapanga mashambulizi wakitumia washambuliaji watano hadi saba wa kujitoa muhanga. Kwa mujibu wa shirika la habari la Ujerumani, dpa, hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa.

Paris wajitokeza licha ya hofu ya mashambulizi

Polisi wakilinda kituo cha treni mjini Munich kutokana na kitisho cha mashambulizi ya kigaidi.

Polisi wakilinda kituo cha treni mjini Munich kutokana na kitisho cha mashambulizi ya kigaidi.

Nchini Ufaransa, zaidi ya maafisa 100,000 wa polisi walitumwa kwenye maeneo kadhaa kulinda sherehe, huku wakaazi wa mji mkuu, Paris, wakijitokeza kwa wingi kwenye viwanja vya Champs Elysees kuupokea mwaka 2016, ukiwa mkusanyiko wa kwanza mkubwa tangu mashambulizi ya kigaidi ya Novemba 13.

Kwenye hotuba yake ya Mwaka Mpya, Rais Francois Hollande, alisema "bado Ufaransa haijamalizana na ugaidi" na kwamba kitisho cha mashambulizi mengine "bado kinaendelea kuwa kikubwa."

Nchini Ubelgiji, polisi waliwakamata watu watano wakishukiwa kupanga mashambulizi kwenye Mkesha wa Mwaka Mpya mjini Brussels, huku pia wakitangaza kumtia nguvuni mshukiwa wa kumi wa mashambulizi ya Paris.

Moto hotelini Dubai

Huko Dubai, moto mkubwa ulizuka kwenye hoteli moja ya kifahari na kuwajeruhi watu 16, muda mchache kabla ya sherehe za mwaka mpya kuanza. Picha zilizosambaa mitandaoni zinaonesha Hoteli ya Address Downtown, ambayo iko karibu na jengo refu kabisa duniani, Burj Khalifa, ikiungua moto kwenye ghorofa zake kadhaa, huku ving'ora vikilia na helikopta za uokozi zikizunguka.

Jengo la Hoteli ya Address Brand likiwaka moto mjini Dubai kwenye mkesha wa mwaka mpya.

Jengo la Hoteli ya Address Brand likiwaka moto mjini Dubai kwenye mkesha wa mwaka mpya.

Mkuu wa polisi wa Dubai, Jenerali Khamis Matar al-Mzeima, alisema wageni wote kwenye hoteli hiyo ya viwango vya ubora wa nyota tano wamehamishwa.

Hata hivyo, serikali ya Dubai iliendelea na shamrashamra kwa kurusha fashifashi za aina yake kuukaribisha Mwaka Mpya wa 2016, huku moto huo ukiendelea kuzimwa. Bado chanzo cha moto huo uliochukuwa masaa kadhaa kabla ya kuzimwa, hakijafahamika. Mashahidi wanasema ulianza majira ya saa tatu unusu usiku kwa saa za Mashariki ya Kati kwenye ghorofa za kati na kuzagaa kote.

Mji wa Sydney, ambao kawaida huwa wa mwanzo kuupokea Mwaka Mpya, ulirusha fashifashi za mapambo ya kifahari takribani masaa sita kabla ya kwengine kokote duniani.

Baada ya Asia, Mashariki ya Kati, Ulaya na Afrika, shamrashamra za mwaka mpya zinatazamiwa kukamilika kwenye mataifa ya Amerika ya Kaskazini na Kusini.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP/Reuters
Mhariri: Bruce Amani

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com