Mwaka 2007 umekuwa mbaya zaidi nchini Irak | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.12.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mwaka 2007 umekuwa mbaya zaidi nchini Irak

Hatua ya Marekani kuongeza idadi ya wanajeshi haikufua dafu

Wanajeshi wa Marekani nchini Irak

Wanajeshi wa Marekani nchini Irak

Mojawapo ya hatua kubwa iliyochukuliwa mwaka huu na serikali ya Marekani ni kuongeza idadi ya wanajeshi nchini Irak katikati ya mwezi Februari.

Lengo lilikuwa kuboresha usalama katika mji mkuu wa Irak, Baghdad na mkoa wa magharibi wa Al Anbar, maeneo mawili yanayoelezwa kuwa na machafuko mabaya zaidi nchini Irak. Kufikia mwezi Juni, wanajeshi 28,000 zaidi walikuwa wametumwa nchini Irak hivyo kuiongeza idadi ya wanajeshi nchini humo kufikia zaidi ya 160,000.

Kufikia msimu wa mapukutiko kulikuwa na zaidi ya wanajeshi 175,000 nchini Irak. Hii ni idadi kubwa zaidi ya wanajeshi wa Marekani kuwahi kupelekwa nchini Irak, na huku serikali ya Marekani ikizingumzia kupunguza idadi ya wanajeshi wake walio Irak, idadi halisi ya wanajeshi walio nchini humo haiendani na ahadi hiyo.

Serikali ya rais Bush ilisema kuongeza wanajeshi nchini Irak pia kulilenga kupunguza mauaji ya kikabila na kutoa muda zaidi kufanyike mabadiliko ya kisiasa katika serikali ya waziri mkuu Nouri al Maliki, inayoungwa mkono na Marekani.

Kwa mujibu wa shirika la hilali nyekundu, wakati wa ongezeko la wanajeshi, idadi ya wairaki waliolazimika kuyahama makazi yao iliongezeka mara nne. Kufikia mwisho wa mwaka wa 2007, shirika linalowahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, lilikadiria kuna wairaki milioni 2.3 waliohama makwao nchini Irak na zaidi ya wairaki milioni 2.3 waliihama nchi yao. Irak ina idadi ya wakaazi milioni 25.

Shirika la kimataifa lisilo la kiserikali liitwalo Refugees International, linalieleza tatizo la wakimbizi wa Irak kuwa janga la wakimbizi linalokua kwa kasi kubwa duniani. Mwezi Oktoba mwaka jana serikali ya Syria ilianza kuitisha visa za kusafiria kutoka kwa wairak. Kufikia wakati huo ilikuwa nchi pekee iliyowaruhusu wairaki waingie bila visa. Sheria hiyo mpya imewalazimu baadhi ya wairaki kurejea mjini Bahgdad, lakini idadi hiyo ingali chini ya 50,000.

Uchunguzi wa hivi karibuni uliofanywa na shirika la UNHCR kwa familia zinazorudi umebaini kuwa zaidi ya asilimia 18 walirejea kwa hiari. Wengi walirudi kwa sababu hawakuwa na visa, walikuwa wameishiwa na fedha au walirudishwa. Mauaji ya kikabila yamepungua katika miezi ya hivi karibuni lakini bado yanaendelea. Maiti zinaendelea kutupwa katika barabara za mji mkuu Baghdad kila siku.

Sababu moja ya kupungua kwa kiwango cha machafuko ni kwamba sehemu kubwa ya Baghdad imegawanywa kikabila. Maeneo ya makaazi sasa yamezingirwa na kuta na nondo zilizo na urefu wa mita kadhaa na kukiwa na vituo vya upekuzi. Maisha ya kawaida hayapo tena. Shirika la hilali nyekundu nchini Irak linakadiria wakimbizi wanane kati ya kumi wanatokea Baghdad.

Kufikia mwisho mwa mwaka 2007, mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa muungano yalipungua kwa kiwango kikubwa lakini bado 2,000 hufanywa kila mwezi. Miundombinu ya Irak, kama vile ugavi wa maji na umeme inaboreka, lakini bado iko chini ya viwango vya kabla uvamizi. Vile vile ajira na mauzo ya mafuto katika nchi za kigeni. Ukosefu wa ajira, kwa mujibu wa serikali ya Irak, uko kati ya asilimia 60 na 70.

Ripoti ya uchunguzi huo inasema Wairaki wanateseka kutokana na ongezeko la uhaba wa chakula, makazi, maji na usafi, huduma za afya, elimu na ajira. Kati ya wairaki milioni nne wanaotegemea msaada wa chakula ni asilimia 60 pekee wanaopataka chakula kupitia mfumo unaosimamiwa na serikali, ikilinganishwa na asilimia 96 mnamo mwaka wa 2004.

Karibu watu milioni 10 wanautegema mfumo huo, Mwezi Disemaba mwaka jana serikali ya Irak ilitangaza itapunguza idadi ya vitu inavyotoa katika mfumo wa chakula kutoka kumi hadi vitano kwa sababu ya gharama za miundombinu na mfumuko mkubwa wa bei. Kasi ya mfumuko wa bei inakadiriwa rasmi kufikia asilimia 70.

Kupunguzwa kwa msaada kunatarajiwa kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka huu wa 2008 na kumesababisha wasiwasi katika jamii ikiwa hatua muafaka hazitachukuliwa kukabiliana na ongezeko la umaskini na ukosefu wa ajira.

Watoto wa Irak wanaendelea kuteseka sana. Kasi ya utapiamlo miongoni mwa watoto imeongezeka kutoka asilimia 19 wakati wa kipindi cha vikwazo vya kiuchumi kabla uvamizi na kufikia asilimia 28 kwa wakati huu.

Mwaka wa 2007 pia umekuwa mwaka wa umwagaji mkubwa wa damu katika kipindi chote cha kuikalia Irak. Kundi linalopigania kuibadili sera ya kigeni ya Marekani liitwalo ´Just Foregn Policy´, linakadiria idadi ya wairaki waliouwawa kutokana na uvamizi wa Irak ulioongozwa na Marekani na hatua ya kuikalia nchi hiyo imefikia 1,139,602.

Mwaka wa 2007 wanajeshi 894 wa Marekani waliuwawa nchini Irak hivyo kuufanya mwaka huo kuwa mbaya zaidi wa muda ambao jeshi la Marekani limekuwa likiikalia Irak. Hayo ni kwa mujibu wa shirika linalojiita Icasualities.org

Wizara ya ulinzi ya Marekani inasema kufikia sasa wanajeshi 3,896 wameuwawa nchini Irak. Sehemu ya juhudi za jeshi la Marekani kupunguza machafuko imekuwa kuwalipa wapiganaji wa zamani. Mwishoni mwa mwaka jana jeshi la Marekani lilianza kuwalipa wanamgambo wa zamani dola 300 kama mshahara kila mwezi, likiwaita raia wanaojali maslahi.

Huku sera hii ikiwa imefaulu kupunguza machafuko mkoani al Anbar, imeongeza mipasuko ya kisiasa kati ya chama cha Washia na wasunni kwa kuwa idadi kubwa ya wanamgambo wa zamani wanaolipwa ni wasunni. Waziri mkuu wa Irak, Nuri al Maliki, amesema wanamgambo hao hawatakuwa sehemu ya jeshi la usalama la serikali, ambalo lina idadi kubwa ya wanamgambo wa kishia.

Kushindwa kwa sera ya Marekani kuongeza idadi ya wanajeshi nchini Irak kunadhihirika katika serikali ya mjini Baghdad huku ikiwa imegawanyika zaidi kuliko hapo awali na huku matumaini ya maridhiano yakififia. Kwa mujibu wa kura ya maoni iliyofanywa na shirika la BBC, asilimia 98 ya wasunni na asilimia 84 ya washia wanataka wanajeshi wote wa Marekani waondoke Irak.

 • Tarehe 30.12.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Chzz
 • Tarehe 30.12.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Chzz
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com