1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mvua kubwa yasababisha vifo vya watu wengine 29 Afghanistan

20 Aprili 2024

Mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha vifo vya watu wengine 29 nchini Afghanistan katika muda wa siku nne zilizopita. Haya yamesemwa leo na idara ya kudhibiti majanga ya serikali

https://p.dw.com/p/4f0bw
Wanaume wavukishwa eneo la mafuriko kwa magari ya jeshi wilayani Boldak nchini Afghanistan mnamo Aprili 13, 2024
Mafuriko nchini Afghanistan Picha: SANAULLAH SEIAM/AFP/Getty Images

Msemaji wa idara hiyo, Janan Sayeq, amesema watu hao 29, walifariki dunia kwenye mikoa 10 tofauti kutokana na mvua hiyo kubwa iliyoanza kunyesha siku ya Jumatano hadi leo Jumamosi.

Soma pia:Maporomoko ya udongo yaua zaidi ya watu 30 Afghanistan

Sayeq ameongeza kuwa watu wengine saba walijeruhiwa katika kipindi hicho na nyumba 72 kuharibiwa huku zaidi ya ekari 2,500 za mashamba zikisombwa.

Watu 25,000 wanahitaji msaada nchini Afghanistan

Kulingana na takwimu rasmi, zaidi ya watu 100 wamefariki katika mafuriko mwezi huu huku zaidi ya familia 25,000 zikihitaji msaada.

Mwaka uliopita, Umoja wa Mataifa ulionya kuwa Afghanistan inakabiliwa na mabadiliko makubwa ya hali ya hewa.

Soma pia:Mamia wafa kwa mafuriko Pakistan, Afghanistan

Baada ya miongo minne ya vita, nchi hiyo iko katika orodha ya mataifa ambayo hayajajiandaa vizuri kukabiliana na hali mbaya ya hewa, ambayo wanasayansi wanasema inazidi kujitokeza mara kwa mara na kuwa mbaya zaidi.