Mutharika atangazwa kushinda muhula wa pili madarakani | Matukio ya Afrika | DW | 28.05.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mutharika atangazwa kushinda muhula wa pili madarakani

Rais wa Malawi Peter Mutharika amechaguliwa kwa muhula wa pili madarakani baada ya kupata ushindi katika uchaguzi wa wiki iliyopita uliogubikwa na madai ya udanganyifu. 

Mutharika amepata ushindi mwembamba wa asilimia 38.6 ya kura akimpita mpinzani wake wa karibu Lazarus Chakwera wa chama cha Malawi Congress MCP aliyejipatia asilimia 35.4 ya kura. Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Jane Ansah alietangaza matokeo hayo alisema kuwa, "ninapenda kutanguliza pongezi zangu kwa rais mteule na makamu wake. Umechaguliwa na watu wa Malawi kuiongoza nchi kuelekea mustakabali bora,  umepewa jukumu la kuongoza ajenda ya maendeleo ya taifa hili kwa miaka mitano ijayo."

Matokeo ya mwisho ya uchaguzihuo uliofanyika wiki iliyopita yalitangazwa baada ya kuzozaniwa mahakamani ambapo kiongozi wa upinzani Chakwera alipata zuio la muda la mahakama kutokana na madai ya udanganyifu.

Jaji wa mahakama kuu Charles Mkandawire aliondoa zuio hilo na dakika chache tu baadae tume ikathibitisha ushindi wa Mutharika. Chama cha upinzani cha MCP kiliitaka tume ya uchaguzi kuchunguza madai 147 yaliyowasilishwa kuhusiana na hitilafu zilizojitokeza wakati wa uchaguzi. Mahakama baadae ilisema kwamba uchunguzi kuhusiana na madai ya udanganyifu unaweza kuendelea baada ya matokeo kutangazwa.

 Lazarus Chakwera Präsidentschaftswahlen Kandidat Malawi (Getty Images/AFP/A. Gumulira)

Kiongozi wa upinzani Malawi Lazarus Chakwera (katikati)

Vyama vya upinzani vimelalamika kwamba idadi kubwa ya karatasi za kupigia kura zilikuwa zimechezewa kwa kutumia wino wa kufanya masahihisho. Mkuu wa jeshi la polisi Rodney Jose ametoa onyo kali dhidi ya waandamanaji wa upinzani ambao walijitokeza katika mji mkuu wa Lilongwe na mji wa kaskazini wa Mzuzu akisema ghasia hazitavumiliwa.

Waangalizi wa Umoja wa Ulaya walielezea kampeni za uchaguzi kuwa "ziliandaliwa vyema, zilishirikisha wote na zilikuwa  za wazi na zenye ushindani".

Mutharika aligombea kupitia chama cha Democratic Progressive DPP ambacho kilianzishwa mwaka 2004 na kaka yake rais wa zamani Bingu wa Mutharika.  Rais huyo ametoa ahadi za kupambana na ufisadi na kuboresha miundombinu lakini muhula wake wa kwanza ofisini ameshindwa kukabiliana na ufisadi na wimbi la mauaji ya Albino. Yeye mwenyewe amekabiliwa na madai ya ufisadi ambapo mwezi Novemba alilazimika kurejesha kiasi cha dola 200,000 za kimarekani kama mchango kutoka kwa mfanyabiashara anayekabiliwa na tuhuma za rushwa katika mkataba wa dola milioni tatu wa usambazaji chakula kwa jeshi la polisi.

AFP/DPA

 

 

DW inapendekeza