Musharraf atoka jeshini | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Musharraf atoka jeshini

Rais wa Pakistan,Perves Musharraf ameacha ukuu wa majeshi katika sherehe iliofanyika leo nchini Pakistan. Hatua ya sasa imefuatia shinikizo la ndani na nje.

default

Musharraf amejiuzulu kama mkuu wa jeshi

Katika siku ambayo wengi hawatakutarajia kuishuhudia,Musharraf,amekabidhi kijirungu,ambacho ni alama ya uongozi wa jeshi kwa naibu wake,Generali Ashfaq Kiyani katika sherehe ya kumuuga.Hiyo ni alama ya kumaliza miaka minane ya utawala wa kijeshi.

Musharraf, mwenye umri wa miaka 64 ataapishwa kesho alhamisi kama rais asiemwana jeshi.Musharraf amechukua hatua hiyo ili kutuliza wasiwasi wa ndani na nje kuhusu hatua yake ya Novemba 3 ambapo alitangaza hali ya hatari nchini Pakistan.

Musharraf amewaambia waliohudhuria kuwa kesho hata vaa tena sare za jeshi,akisikika kama anasikitika.Ameongeza kuwa amekuwa jeshini kwa kipindi cha miaka 46 na sasa analiaga jeshi ambalo kwa maneno yake alikuwa akilipenda maishani mwake.

Sherehe imefanyika katika makao makuu ya jeshi mjini Rawalpindi ambako alipokelewa na Generali Kiyani zamani mkuu wa kikosi cha ujasusi cha nchi hiyo.

Musharraf ambae amekuwa jeshini kwa kipindi cha zaidi ya miaka 40 amefanya kazi jeshini katika vitengo mbalimbali mkiwemo kuwa katika kikosi maaluma cha makamando. Pia alishiriki katika vita vya mara mbili dhidi ya India.Mwishowe aliongoza mapinduzi ya kijeshi mwaka wa 1999,yaliyoung’oa utawala wa raia.

Musharraf ambae wakati mmoja aliielezea sare ya jeshi kama ngozi yake ya pili,amevisifu vikosi vya jeshi la Pakistan, kama mmojawapo wa jeshi bora duniani, na kusema kuwa anaimani na mrithi wake Generali Kiyani.

Kujiuzulu kwake,kama mkuu wa majeshi,ni sehemu ya kutimiza,mwito wa Marekani mshirika wake mkuu pamoja na jamii ya kimataifa,ambayo hivi majuzi ilikuwa nyuma yake wakati akipambana dhidi ya Al Qaeda na wa Taleban.

Hata hivyo baado Musharraf anakabiliwa na shinikizo lingine ndani na nje ya Pakistan.Nalo ni kuondoa amri ya hali ya hatari aliyoitangaza wiki tatu na ushei zilizopita. Uchaguzi mkuu wa nchi hiyo umepangwa kufanyika januari tarehe nane mwakani.

Kituo kimoja cha televisheni cha kibinafsi,bila kutoa chanzo cha habari zake, kimesema kuwa,Musharraf anapanga kuondoa amri ya hali ya hatari katika kipindi kijacho cha saa 48.Lakini afisa wa ngazi za juu wa serikali ameliambia shirika la habari la AFP kuwa rais baado nachunguza uwezekano huo.Nae msemaji wa Musharraf,Rashid Quresh, amesema kiongozi huyo atalihutubia taifa hapo kesho,lakini hakutoa maelezo zaidi.

Rais wa Marekani,George W.Bush, pamoja na viongozi wengine wa nchi za magharibi wamekuwa wakimhimiza Musharraf,kujiuzulu kama mkuu wa majeshi, kuondoa amri ya hali ya hatari,kurejesha katiba,kuwaachilia huru wafungwa wa kisiasa na pia kuacha kuviandama vyombo vya habari.

Sasa mustakbala wa Musharraf kisiasa bila ya ushawishi wa jeshi,unategemea uungaji mkono wa mrithi wake Generali Kayani.Kayani anaegemea sana nchi za magharibi.Pia nguvu za vyama vya upinzani vya Pakistan zitakuwa kigezo kwake.

 • Tarehe 28.11.2007
 • Mwandishi Siraj Kalyango
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CU7J
 • Tarehe 28.11.2007
 • Mwandishi Siraj Kalyango
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CU7J

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com