1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mudavadi atengana na Kenyatta

Admin.WagnerD3 Januari 2013

Ndoa ya kisiasa kati ya Naibu waziri Mkuu Musalia Mudavadi na Muungano wa Jubilee Coalition unaojumuisha chama cha TNA cha Naibu waziri Mkuu Uhuru Kenyatta na chama cha URP kinachoongozwa na William Ruto imevunjika.

https://p.dw.com/p/17Cx7
Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta
Kenia Uhuru KenyattaPicha: picture-alliance/dpa

Naibu Waziri Mkuu Musalia Mudavadi ameamua kujibwaga uwanjani kuwania kiti cha urais kwa tikiti ya chama chake cha UDF. Mudavadi alijiondoa kutoka muungano wa Jubilee baada ya mkataba kati yake na Uhuru Kenyatta kuvunjika ambapo Uhuru aliahidi kumuachia Mudavadi nafasi ya kugombea urais kwa tikiti ya muungano wa Jubilee Coalition na baadaye kumgeuka.

Hatua hiyo inafikiwa baada ya vuta nikuvute ya siku mbili, Jumatatu na Jumatano katika ofisi ya msajili wa vyama vya kisiasa mjini Nairobi, chama cha UDF kimejiondoa rasmi kwenye muungano wa Jubilee na kuamua kusimama kivyake kwenye kinnyang'anyiro cha urais.

Sababu za kutengana zaelezwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano katika chama cha UDF Mundia Muchiri alisema “Sisi tumekubaliana ya kwamba tunaondoka kutoka katika huu muungano na tume na tunasema kwamba hakuna tena muungano wa Jubilee. Tumevunjilia mbali muungano wa Jubilee sababu ni kwamba kuafikiana, kulikuwa na ukiukaji wa mkataba, tumeandika barua na tukasema ya kwamba sheria haikufuatwa vile inatakikana”.

Musalia Mudavadi wakati akiwa ODM
Wahlen in KeniaPicha: AP

Chama cha UDF kilitaka musajili wa vyama vya kisiasa avunjilie mbali muungano mzima wa Jubilee unaojumuisha chama cha TNA na chama cha URP lakini hilo halikufanyika hapo jana.

Katibu mkuu wa chama cha TNA Onyango Oloo anasema chama cha UDF kilikuwa sawa na ndoa ya mke wa pili na haiwezi kuathiri ndoa ya mke wa kwanza. “Tulitaka kumaliza uhusiano huu kwa upole lakini ndugu zetu katika UDF hawakupendezwa na badala yake kile wametaka ni muungano mzima uvunje pamoja na ule uliobuniwa kabla wao wajiunge. Ukikubali kuolewa mke wa pili ni sharti ukubali kwamba ukijiondoa kutoka kwa ndoa si lazima ndoa ya kwanza nayo ivunjike. Tutabaki kuwa muungano wa jubilee na tutabaki na URP na tutaendelea mbele”.

Mudavadi kuungana na kuungana na Wamalwa

Duru zinasema kwamba  Musalia Mudavadi sasa ameunagana na mgombea urais wa tikiti ya chama cha New Ford Kenya kubuni muungano wa tatu wa kisiasa. Baada ya Mudavadi kutofautiana na Uhuru Kenyatta, Kiongozi wa chama cha New Ford Kenya Waziri wa Sheria Eugene Wamalwa amemtaka Mudavadi kujiunga naye. “Nimemualika Mheshimiwa Musalia Mudavadi kama maneno yaliharibika vile yaliharibika kule Jubilee ya kwamba milango yetu iko wazi na yeye akiwa tayari sisi tuko tayari aje tufanye kazi”. alisema Wamalwa.

Muungano wa kwanza wa kisiasa unaovijumuisha vyama vya ODM, Ford Kenya na Wiper Democratic Movement tayari  umemuidhinisha Waziri Mkuu Raila Odinga kuwania wadhifa wa urais naye makamu wa Rais Kalonzo Musyoka akiwa mgombea mwenza atakechukua nafasi ya naibu wa Rais.

Wajumbe wa Muungano wa Jubilee wameamua ni  Naibu waziri mkuu uhuru Kenyatta wa chama cha TNA atakayeshika usukani kugombea urais kwa tikiti ya muungano huo huku William Ruto akiwa Naibu wake. Wagombea wengine ambao wangali wanayumbayumba ni Raphael Tuju, Peter Keneth na James Ole Kiyiapi.

Mwandishi: Alfred Kiti
Mhariri: Josephat Charo