Mswada wa mabadiliko ya tabia nchi wawasilishwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.12.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mswada wa mabadiliko ya tabia nchi wawasilishwa

Wajumbe wanaoshiriki kwenye mazungumzo ya dunia juu ya athari za mabadiliko ya tabia nchi mjini Paris, wanatazamia kupata makubaliano ya gharama na ufadhili wa hatua za kukabiliana na janga hilo la kilimwengu.

Frankreich COP-21 Joel Domenjoud

Mwanaharakati akosoma bango kwa ajili ya mkutano wa mazingira mjini Paris

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius amesema ana matumaini kwamba andiko la mwisho la makubaliano yaliyosubiriwa kwa muda mrefu litakuwa tayari leo Jumamosi (12.12.2015).

Lakini kulikuwa hakuna uhakika baada ya siku ambayo ilishuhudia malumbano makali wakati nchi 195 zilijaribu kuondoa tofauti zao za mwisho,na huenda pia zisizoweza kuondolewa.

Mikutano ya mawaziri na maafisa wa ngazi ya juu ilitarajiwa kuendelea hadi alfajiri ya leo Jumamosi kwa usiku wa pili mfululizo.

COP21 Klimafonferenz Frankreich Außenminister Laurent Fabius

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa Laurent Fabius

Iwapo muafaka utafikiwa, itakuwa ni mara ya kwanza kwamba nchi zote za dunia kwa pamoja zimeahidi kupunguza utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira ili kuiweka sayari ya dunia kutopata ujoto zaidi hadi katika viwango vya maafa.

"Tofauti tayari zimesababisha kuahirishwa kwa rasimu ya mwisho kwa siku moja. Kesho asubuhi, (leo), nitaweza kuwasilisha waraka ambao, nina hakika, utaidhinishwa na itakuwa hatua kubwa mbele kwa binadamu wote," Fabius alisema.

Wachafuzi wakubwa

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alikutana na wahusika kadhaa ambao ni pamoja na mataifa matatu yanayochafua zaidi hali ya hewa- China, Marekani na India- pamoja na Afrika kusini, Venezuela yenye utajiri mkubwa wa mafuta, Kuwait, Singapore, Australia na Bahrain.

Kile kinachoitwa muungano wenye matumaini makubwa, zaidi ya nchi tajiri na masikini 90 zikiongozwa na Umoja wa Ulaya na Marekani kupambana na mtazamo wa kundi la G77 la nchi zinazoendelea, umeonya dhidi ya kupungua kwa matumaini.

"Hatutaridhika na kiwango cha chini cha pamoja cha udhibiti,"alitangaza waziri wa mazingira wa Ujerumani Barbara Hendricks.

Kundi hilo lilipata nguvu pale Brazil, inayoonekana kuwa mjumbe muhimu wa majadiliano katika mazungumzo hayo, kujiunga na kundi hilo.

Bildergalerie Klima Proteste Ukraine Kiew

Waandamanaji wanaharakati wakishiriki katika maandamano ya dunia kulinda mazingira nchini Ukraine

Christoph Bals wa kundi linaloangalia hali ya mazingira la Ujerumani Germanwatch ameona kwamba kama ishara kwamba mataifa yanayoendelea na yale yaliyoendelea yanasogea kwa pamoja kupata suluhisho, wakati Brazil , Afrika kusini na Mexico zikichukua "jukumu muhimu la kuwa kama daraja."

Tofauti bado zipo

Nchi bado zinatofautiana kuhusiana na vipi inawezekana kufikia lengo la muda mrefu la kubakisha kiwango cha joto chini ya nyuzi joto mbili, wakati nchi nyingi zikisema kwamba ni pale tu kiwango cha nyuzi joto 1.5 kitakapofikiwa ndipo kutakapoepushwa athari mbaya za ujoto duniani.

Suala ambalo bado halijapatiwa jibu ni juu ya kutoa msaada wa fedha kwa mataifa yanayoendelea. Umoja wa Ulaya na Marekani zinataka mataifa yanayoinukia kiuchumi kusaidia, lakini mengi yanakataa pendekezo hilo. Mataifa ya magharibi yenye viwanda yanasema yanabeba jukumu la kihistoria kwa karne moja na nusu ya matumizi makubwa ya mafuta na makaa ya mawe, hali iliyochangia kuchafuliwa kwa mazingira.

Australien Sydney Anti Klimawandel Demonstration

Waandamanaji wanaharakati wa mazingira nchini Australia

Ni vipi kuelezea kile hasa kinachoweza kutokea katika muda wa miaka 85 ijayo ni suala gumu, wakati mataifa yanayotoa mafuta kwa wingi kama Saudi Arabia na Venezuela yakijaribu sana kuzuwia maneno ambayo yanaelekea kudokeza kwamba nishati ya mafuta na makaa ya mawe isitumike kabisa.

Mwandishi: Sekione Kitojo /dpae
Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com