Mswada wa ′kumtimua′ rais wa Brazil kuwasilishwa bungeni leo | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.04.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mswada wa 'kumtimua' rais wa Brazil kuwasilishwa bungeni leo

Mzozo wa kisiasa nchini Brazil unaingia hatua mpya leo, pale mswada kuhusu kumfungulia mashitaka au la rais Dilma Rousseff utakapowasilishwa bungeni. Kamati ya bunge kuhusu hatua hiyo tayari imekamilisha kikao chake.

Rais wa Brazil Dilma Rousseff anayekabiliwa na shinikizo

Rais wa Brazil Dilma Rousseff anayekabiliwa na shinikizo

Mswada juu ya kuwepo au kutokuwepo mjadala wa kumfungulia mashitaka rais wa Brazil Dilma Roussef kuhusu kutumia vibaya madaraka, unatarajiwa kuwasilishwa na mbunge Jovair Arantes saa saba mchana saa za Brazil, ambazo ni saa moja usiku Afrika mashariki.

Mzozo wa kisiasa katika nchi hiyo ulizidi kuchacha jana Jumanne, baada ya jaji wa mahakama kuu kuamuru kuundwa kwa tume itakayotafakari kushitakiwa kwa mwanasiasa mwingine mashuhuri, makamu rais Michel Temer.

Rais Dilma Rousseff ambaye ametupwa mkono na washirika wake muhimu, hivi sana anafanya chini juu kutafuta uungwaji mkono wa kutosha katika kikao cha pamoja cha bunge na seneti, au Congress, kuzuia kura ya bunge ambayo inaweza kupeleka kwenye baraza la seneti, mswada kuhusu kushitakiwa kwake.

Mchakato wa bunge ni kama ''mapinduzi''

Kwa muda sasa yamekuwa yakifanyika maandamano kumpinga Rais Rousseff

Kwa muda sasa yamekuwa yakifanyika maandamano kumpinga Rais Rousseff

Akizungumza na waandishi wa habari hapo jana, rais Rousseff aliulinganisha na mapinduzi mchakato wa kutaka kumuondoa madarakani.

''Nadhani jaribio lolote la kutumia madai kwamba rais alikiuka sheria ya kifedha kwa kuficha nakisi katika bajeti, kama msingi wa kumfungulia mashitaka, ni mapinduzi, ni mapinduzi kwa sababu halina msingi wa kisheria.'' Alisema Bi Rousseff.

Wiki iliyopita, msaidizi wa rais Dilma Rousseff alikuwa amesema rais huyo ananuia kulifanyia mabadiliko baraza la mawaziri, katika nchi hiyo yenye vyama vya siasa zaidi ya 12, na ambako nafasi za uwaziri na nyadhifa nyingine muhimu serikali zinatumiwa kama karata katika majadiliano ya kisiasa.

Hata hivyo, rais Rousseff ametangaza kusitishwa kwa hatua hiyo, hadi baada ya kura itakayopigwa bungeni kuhusu hatima ya uongozi wake, ambayo inatarajiwa katikati mwa mwezi huu wa April.

Wakosoaji wakosolewa

Wakosoaji wa rais huyo wanasema alizichezea akaunti za serikali na kuzidisha matumizi ya nchi wakati wa kampeni za mwaka 2014, na kufunikafunika athari za mdororo wa kiuchumi.

Hata hivyo mwanasheria mkuu wa nchi hiyo Jumanne alimtetea rais Dilma Rousseff, akikosoa vikali hoja za mwisho za kutaka afunguliwe mashitaka. Mwanasheria huyo, Jose Edouardo Cardozo alisema wapinzani wa rais huyo wanakiuka katiba, kwa kutaka kulipa kisasi kuhusiana na hatua za kisheria zilizochukuliwa dhidi yao, katika kashfa ya wizi wa fedha kwenye kampuni ya umma ya mafuta ya Petrobas.

Kura za maoni zinaonyesha kuwa kiwango cha wabrazil wanaomuunga mkono Rais Dilma Rousseff kimeshuka hadi asilimia 10 tu.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/rtre

Mhariri:Iddi Ssessanga

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com