MPLA yashinda uchaguzi Angola | Matukio ya Afrika | DW | 03.09.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

MPLA yashinda uchaguzi Angola

Nchini Angola chama tawala cha MPLA cha rais Jose eduardo dos Santos kimetangazwa rasmi kuwa kimeshinda uchaguzi wa bunge la nchi hiyo uliofanyika Ijumaa iliyopita.

Vyombo vya habari vya serikali vilitangaza taarifa hiyo hata kabla ya matokeo ya mwisho kutolewa. Kwa hivyo, rais dos Santos anabakia miaka mitano zaidi madarakani.

Wapiga kura wa Angola wakisubiri kushiriki uchaguzi mjini Luanda

Wapiga kura wa Angola wakisubiri kushiriki uchaguzi mjini Luanda

Kutokana na mabadiliko ya katiba ya mwaka 2010 ni kwamba kiongozi wa chama kilichopata kura nyingi kabisa anakuwa rais na mkuu wa serikali.  Taarifa za Tume ya Uchaguzi iliyotangazwa katika mji mkuu wa Luanda ilitaja kwamba asilimia 75 ya wapiga kura walikichagua chama cha MPLA.

Chama kikubwa kabisa cha upinzani, UNITA, kilipata asilimia 18 ya kura. Msemaji wa upinzani na waangalizi huru wa uchaguzi hapo kabla walilalamika kwamba kulikuweko kasoro katika zoezi la uchaguzi huo. Jumla ya viti 220 vimeshindaniwa katika uchaguzi huo.

Uchaguzi umekwenda kwa amani

Mamlaka nchini humo imesema kuwa zoezi la upigaji kura limefanyika kwa amani. Huu ni uchaguzi wa tatu nchini Angola tangu ipate uhuru wake kutoka kwa Wareno mwaka 1975. Uchaguzi wa mwisho ulifanyika mwaka 2008.

Kituo cha kupigia kura Angola

Kituo cha kupigia kura Angola

Uchaguzi uliotangulia kabla ya huo wa mwaka 2008 ulifanyika mwaka 1992. Matokeo ya kutatanisha ya uchaguzi huo yalizusha awamu ya pili vya vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.

Katika uchaguzi wa safari hii, kwa mara ya kwanza Waangola walioko nje wanaoishi nchini Ureno wamekataliwa kupiaga kura.

José Eduardo dos Santos, Rais wa Angola

José Eduardo dos Santos, Rais wa Angola

Angola imepata mafanikio kiuchumi kutokana na mafuta. Hata hivyo wachambuzi wameonya kuwa wakati wasomi wachache wananufaika, kundi kubwa la raia wameendelea kubaki katika dimbwi la umasikini.

Mwandishi: Stumai George

Mhariri: Othman Miraji