MPLA cha Angola chadai kushinda uchaguzi | Matukio ya Afrika | DW | 24.08.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

MPLA cha Angola chadai kushinda uchaguzi

Chama tawala nchini Angola, MPLA Alhamisi hii kimedai kushinda kwa kura nyingi katika uchaguzi mkuu, wakati ambapo tayari kura milioni tano zimekwishahesabiwa na kufanya njia nyeupe kwa waziri wa usalama Jouao Lourenco

Angola Präsidentschaftswahlen Joao Lourenco (Reuters/S. Eisenhammer)

Joao Lourenco, waziri wa usalama wa Angola anayetarajiwa kupokea madaraka kutoka kwa Rais Jose Eduardo dos Santos

Waziri huyo wa usalama Jouao Lourenco, atapokea madaraka kutoka kwa Rais Jose Eduardo dos Santos aliyetawala kwa miaka 38. 

Chama cha MPLA kimesema kwamba kimeshinda uchaguzi huo uliofanyika jana Jumatano baada ya kupitia taarifa kutoka kwa mawakala wake walio kwenye vituo mbalimbali kote nchini humo, amesema afisa mwandamizi kutoka makao makuu ya chama hicho yaliyoko mji mkuu wa nchi hiyo, Luanda, Joao Martins. Martins amesema hii inamaanisha kwamba waziri wa ulinzi Joao Lourenco ndiye atakayemrithi dos Santos, aliyekuwa mamlakani tangu mwaka 1979, hii ikiwa ni kulingana na shirika hilo la habari la Ureno, Lusa. 

Ripoti hii imekuja wakati chama kikuu cha upinzani, UNITA, kikituhumu kwamba jeshi la polisi lilifyatua risasi na kuwakamata raia karibu na baadhi ya vituo vya kupigia kura wakati watu wakiendelea kupiga kura katika mji wa Huambo. Maafisa wa uchaguzi hata hivyo walisema zoezi la kupiga kura lilienda vizuri, pamoja na matatizo madogomadogo na ucheleweshaji.  

Kiasi ya Waangola milioni 9.3 walijiandikisha kuwapigia kura wabunge 220 wa bunge la kitaifa. Chama kitakachoshinda kitachagua Rais.  

Mkuu wa tume ya uchaguzi, Andre sa Silva Neto amewaambia waandishi wa habari kwamba zoezi la uchaguzi linaendelea vizuri. Amesema wameridhishwa na mwenendo wa wapiga kura na kuongeza kuwa imewafurahisha wao na Afrika kwa ujumla.

Bildergalerie langjährige Herrscher Jose Eduardo dos Santos (Getty Images/AFP/S. De Sakutin)

Rais wa Angola, Jose Eduardo dos Santos na mkewe wakiwa katika shuguli za chama

Waangalizi wa kimataifa nao walieleza kuridhishwa na maandalizi ya zoezi zima mara baada ya kukutana na rais wa tume ya taifa ya uchaguzi ya nchi hiyo Andre da Silva Neto mjini Luanda. Ujumbe huo wa waangalizi wa muda mfupi ulioongozwa na waziri mkuu wa zamani wa Visiwa vya Cape Verde Jose Maria Neves uliagizwa na Umoja wa Afrika AU kuuangazia uchaguzi huo mkuu, na ulikuwa na wajumbe 40.

Tume ya uchaguzi ilitarajiwa kuanza kutoa matokeo ya awali jioni leo hii, wakati ambapo tayari chama tawala kilikuwa kikitabiriwa kusalia madarakani. Ingawa tayari kimekishatangaza kuwa kinaongoza katika matokeo ya kura hizo, lakini kinakabiliwa na kupungua kwa uungwaji mkono kutokana na mdororo wa uchumi kwenye taifa hilo tajiri kwa uzalishaji wa mafuta.

Msemaji wa moja ya vyama vikuu vya upinzani, cha UNITA Alcides Sakala amehoji kuhusu tamko hilo la MPLA kudai kuongoza kwenye matokeo wakati bado tume ya uchaguzi haijaanza kutoka hata matokeo ya awali ya uchaguzi. 

Awali, vyama viwili vikuu vya upinzani kwenye uchaguzi huo vya UNITA na Casa-CE vilidai kuwa kampeni hazikuendeshwa kwa usawa na kuongeza kuwa wapiga kura kwenye ngome za vyama hivyo walilazimishwa kupiga kura kwenye vituo vilivyoko mbali na maeneo wanapoishi.  

Lourenco anayetabiriwa kuchukua madaraka kutoka kwa dos Santos, ana miaka 63 na ni gavana wa zamani aliyepigana kwenye vita dhidi ya utawala wa kikoloni wa Kireno pamoja na vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika mwaka 2002.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE/RTRE/APE.
Mhariri: Mohammed Khelef