1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Morales azoa ushindi wa kishindo

Mohammed Khelef13 Oktoba 2014

Rais Evo Morales wa Bolivia amepata ushindi mkubwa na kuepuka uchaguzi wa marejeo, akirejea madarakani kwa muhula wa tatu na akiuita ushindi huo kuwa ni ushindi kwa mageuzi makubwa ya kisoshalisti.

https://p.dw.com/p/1DU45
Rais Evo Morales wa Bolivia.
Rais Evo Morales wa Bolivia.Picha: Reuters/Gaston Brito

Licha ya kwamba matokeo rasmi hayajatangazwa na Baraza Kuu la Uchaguzi, jumla ya asilimia 70 ya kura zimeshahisabiwa na mkulima huyo wa coca, Evo Morales, anaongoza kwa asilimia zaidi ya 60, akimuacha mpinzani wake wa karibu, Samuel Doria Medin, tajiri anayemiliki viwanda vya saruji, kwa mbali akiwa na asilimia 20.

Wafuasi wa Morales walikusanyika kwenye kasri la rais tangu usiku wa Jumapili (12 Oktoba), wakishangiria ushindi wa kiongozi wa kwanza kunasibishwa na jamii ya wenyeji halisi wa Bolivia, ambao ndio wengi kwenye taifa hilo lenye utajiri wa mafuta, gesi na ardhi ya kilimo.

"Kuna hisia kali sana, sio tu ndani ya Bolivia lakini kote Marekani ya Kusini na Caribbean. Hisia ya ukombozi wa watu wetu. Hadi lini tutaendelea kuwa watiifu kwa himaya ya Marekani tu? Kwa mfumo wa kibepari? Ushindi huu ni wa wapingao ukoloni na wapingano ubeberu. Ni wa watu wa Bolivia," Morales aliwaambia wafuasi hao.

Morales, aliyeingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2006, sasa ataweza kutanua falsafa yake ya "usoshalisti wa wazawa", ambayo kwayo amebinafsisha sekta muhimu za uchumi kama vile mafuta na gesi na kuingiza fedha za umma kwenye programu za ustawi wa jamii, kujenga barabara na skuli mpya.

Wafuasi wa Morales wakishangiria ushindi wa kiongozi wao.
Wafuasi wa Morales wakishangiria ushindi wa kiongozi wao.Picha: Reuters/David Mercado

'Kiongozi wa watu'

Wafuasi wake waliojitokeza kwenye viwanja vya majengo ya mashuhuri ya serikali kwenye mji mkuu, La Paz, wanamchukulia Morales kama kiongozi anayesimamia kwa dhati maslahi ya raia wa kawaida, wengi wao wakiwa wameachwa nje ya neema ya rasilimali za nchi hiyo na serikali zilizotangulia, ambazo zikiungwa mkono na Marekani na kampuni za mafuta za kigeni.

"Rais Evo Morales anafanya hasa kile alichosema angelikifanya, na muhula wake huu wa tatu utakuwa mzuri zaidi. Uugwaji wako mkono ni mkubwa. Kwetu huu ni ushindi mkubwa. Watu wa Bolivia wamejitokeza kupiga kura kuhakikisha mageuzi yanaendelea," alisema Jaime Abela, rais wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi, La Paz Neighbors Federation, ambalo limekuwa likimuunga mkono Morales tangu awali.

Sasa Morales ana nafasi pia ya kutekeleza ahadi yake ya kuigeuza Bolivia kuwa kituo cha nishati katika eneo la kusini mwa Amerika, kwa kutumia nishati ya nyuklia.

Wakosoaji wake wanasema kasi yake ya ubinafsishaji na kuelemea sana siasa za kisoshalisti kunahatarisha sekta binafsi inayoangaliwa na wengi kwenye mataifa ya Magharibi kama nguzo kuu ya uchumi imara.

Hata hivyo, ndani ya mihula yake miwili ya uraisi, idadi ya raia wanaoishi kwenye ufukara uliotitia imeshuka hadi kufikia wastani wa mtu mmoja kwa kila watano miongoni mwa raia milioni 6 wa nchi hiyo, ambayo bado inatajwa kuwa masikini kabisa katika bara la Amerika.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo