1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Monaco yatwaa ubingwa wa Ligue1

18 Mei 2017

Chipukizi nyota wa Monaco Kylian Mbappe aliisaidia Monaco kunyakua taji lao la kwanza la ligi kuu ya nchini Ufaransa Ligue 1 katika kipindi cha miaka 17

https://p.dw.com/p/2dAFZ
Frankreich Fußball AS Monaco - Saint-Etienne
Picha: Reuters/J.-P. Amet

Mbappe mwenye umri wa miaka 18, alitimka na kuwavuka mabeki wa Saint Etienne na kupachika kiustadi goli la ufunguzi katika mechi hiyo dakika zilipotimu 19 katika uwanja wa Stade Louis II, na hapo ndipo utawala wa Paris Saint Germain wa miaka minne katika ligi hiyo ulipofikishwa kikomo. Valere Germain alipachika wavuni goli la pili katika dakika ya mwisho ya mechi.

"Hatimaye tunaweza kusema sisi ni mabingwa. Ninajivunia sana timu hii, ninajivunia wachezaji hawa. Ni ndoto kwangu, nina furaha sana," nahodha wa Monaco Radamel Falcao aliliambia shirika la habari la Canal+.

Monaco walio chini ya ukufunzi wa Leonardo Jardim walikuwa wanahitaji alama moja pekeyake kabla mechi hiyo na Saint Etienne ili waweze kutawazwa mabingwa wa Ufaransa kutokana na kuwa walikuwa na tofauti kubwa ya magoli wakilinganishwa na wapinzani wao. Kwa ushindi huo walifikia jumla ya alama 92, alama sita mbele ya PSG walio katika nafasi ya pili kwenye jedwali la Ligue 1.

Italien Pokalfinale Juventus Turin - Lazio Rom
Juventus watwaa Kombe la ItaliaPicha: Imago/HochZwei/Syndication

Kwengineko Ulaya, huko nchini Italia, Juventus waliwalaza Lazio usiku wa Jumatano na kulibeba taji la Italian Cup. Juventus walipata ushindi wa mabao 2-0 beki wa kulia Dani Alves na Leonardo Bonucci wakiwa wafungaji wa mabao hayo katika uwanja wa Olympic.

Ushindi huu umewaweka katika nafasi nzuri ya kushinda mataji matatu msimu huu, kwani wanakaribia kuishinda ligi kuu ya nchini Italia Serie A kwa mara ya sita mfululizo, kabla kuchuana na Real Madrid katika fainali ya Ligi ya vilabu bingwa barani Ulaya tarehe 3 Juni huko Cardiff.

Kwa kushinda taji hilo, klabu hiyo ya Turin, imeweka rekodi kwa kulishinda kombe hilo la Italian cup kwa mara ya 12.

"Heko kwa vijana wangu kwa yale waliyofanya katika kipindi cha kwanza na kuepuka changamoto katika safu ya ulinzi katika kipindi cha pili," alisema kocha wa mkufunzi wa Juventus Massimiliano Allegri.

Mwandishi: Jacob Safari/Reuters/AFPE
Mhariri: Bruce Amani