Moi azikwa na maelfu kwenye shamba lake mjini Kabarak | Matukio ya Afrika | DW | 12.02.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Moi azikwa na maelfu kwenye shamba lake mjini Kabarak

Mwili wa aliyekuwa rais wa pili wa taifa la Kenya, Daniel arap Moi, umezikwa kwenye shamba la Kabarak, katika mji wa Nakuru, ambapo mwanaye alikabidhiwa ‘kirungu' chake kama ishara ya kuendelezwa uongozi wa familia.

Viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta wamemkumbuka Rais Moikama mtu mkarimu, mpenda amani na kiongozi shupavu, huku wanachama wa KANU, chama ambacho alikitumia kama tiketi yake ya uongozi, kikitangaza siku 40 za maombolezi kwa wanachama wake.

Rais Uhuru Kenyatta aliwavunja mbavu waombolezaji katika hafla ya kumzika kiongozi wa pili wa taifa, hayati Rais Daniel arap Moi, alipozungumzia wakati mmoja alipoamriwa na Rais Moi kusafiri kutoka Nairobi hadi Nakuru kwa chini ya saa moja kufuatia kosa alilofanya. Rais Uhuru amemuomboleza Rais Moi kama kiongozi muadilifu na ambaye uongozi wake utaenziwa. Alitumia fursa hiyo kuzindua tena mradi wa hospitali ya Kabarak uliokuwa mradi wa mwisho wa hayati Rais Moi:

Kenia 1992 | Daniel Arap Moi, ehemaliger Präsident (Getty Images/AFP/A. Joe)

Picha hayati Arap Moi mwaka 1992

Siasa zaibuka

Maswala ya kisiasa hayakuwekwa kando kwenye hafla hii ya maziko, miongoni mwa matukio haya ikiwa wakati mbunge wa Rongai Raymond Moi alipomkabidhi kakake mdogo, Seneta Gideon Moi, kile kirungu cha Rais Moi, ikionekana kwamba sasa Seneta Gideon ndiye atakayeuendeleza uongozi wa baba yao:

Naibu wa Rais William Ruto ameelezea kuwa anajivunia uhusiano wake wa kisiasa na hayati Rais Moi aliyewahimiza wakati wote kuepuka siasa za chuki. Hayati Rais Daniel Arap Moi amezikwa kando ya marahemu mke wake Lena Moi katika shamba la Kabarak hapa Nakuru, shughuli iliyondaliwa kwa heshima zote za kijeshi ikiwa ni pamoja na kupigwa kwa mizinga 19.

Maelfu wadamka kumzika Moi

Kenia Nairobi 2002 | Uhuru Kenyatta & Daniel arap Moi, Präsident (Getty Images/AFP/S. Maina)

Kenyatta na Moi mwaka 2002

Mmoja baada ya mwengine waombolezaji walimiminika baada ya malango ya Chuo Kikuu cha Kabarak kufunguliwa mwendo wa saa kumi na moja asubuhi ya Jumatano. Baadhi walikesha nje ya majengo haya ilimradi wawe wa kwanza kufika hapa, wengine wakisafiri kutoka miji ya mbali ili kushuhudia tukio hili.

Miongoni mwa mambo ambayo atakumbukwa nayo Hayati Moi ni jukumu lake kwenye kuifufuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Luteni Lazarus Sumbeiyo, aliyekuwa mpatanishi rasmi wa taifa la Sudan, amesema Moi aliupa kipaumbele ushirikiano wa Jumuiya hiyo alioamini ungehimiza maendeleo na ukuaji wa mataifa haya:

Tazama vidio 01:02

Rais mstaafu wa Kenya Daniel arap Moi aaga dunia

Hata hivyo kuliibuka purukushani wakati Gavana wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko alipoondolewa kwa nguvu na maafisa wa usalama kutoka kwenye jukwaa. Ilibainika baadaye kwamba gavana huyo alikuwa amekiuka itifaki kwa kufika baada ya rais kuwasili kwenye sherehe hiyo.

Hayati Rais Daniel Arap Moi amezikwa kando ya marehemu mke wake, Lena Moi, katika shamba lake la Kabarak, kwani ndivyo alivyoagiza. Shughuli nzima ya mazishi yake imeandaliwa kwa heshima zote za kijeshi.