Mo Farah aivunja rekodi ya Moorcroft | Michezo | DW | 06.06.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Mo Farah aivunja rekodi ya Moorcroft

Wanariadha na umati uliojitokeza katika mashindano ya Diamond League mjini Birmingham walitoa heshima zao mwisho kwa Muhammad Ali kwa kupiga makofi kwa dakika moja kabla ya mashindano kuanza

Bingwa mara mbili wa Olimpiki Mo Farah aliendelea na maandalizi ya Rio kwa kuvunja rekodi ya miaka 34 iliyowekwa na Muingereza David Moorcroft katika mbio za mita 3,000. Farah, mshindi wa dhahabu katika mita 5,000 na 10,000 katika mashindano ya Olimpiki ya London 2012, alishinda katika kutumia muda wa dakika saba, sekunde 32.62 na kuivunja rekodi ya Moorcroft ya 7:32.79 iliyowekwa 1982. Wakeyna Mathew Kiptanui na Hillary Maiyo walimaliza katika nafasi ya pili na tatu.

Mkenya Asbel Kiprop alishinda mbio za mita 1,500 kwa wanaume katika muda wa 3:29.33 na mwenzake Conseslus Kipruto akashinda mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji katika muda wa 8:00.12. Alifwatwa na Wakenya wenzake Paul Kipsiele Koech, 8:10.19. 3, Barnabas Kipyego, 8:14.74, Brimin Kiprop Kipruto, 8:19.33. 5, Jairus Kipchoge Birech, Kenya, 8:20.31 na Clement Kimutai Kemboi, 8:21.07.

Katika mita 800 bingwa wa Olimpiki Mkenya David Rudisha aliibuka mshindi. Francine Niyonsaba wa Burundi alishinda mbio za mita 800 kwa wanawake katika muda wa 1:56:92

Djokovic hakamatiki katika tennis

Novak Djokovic

Mwanatenis Novak Djokovic

Novak Djokovic amejiunga na kikundi cha magwiji wa mchezo wa tennis baada ya kumwangusha mchezaji anayeoridheshwa nambari mbili ulimwenguni Andy Murray kwa seti za 3-6 6-1 6-2 6-4 na kushinda taji lake la kwanza kuu la French Open na kushikilia mataji manne makuu ya grand slam kwa wakati mmoja.

Djokovic ndiye mtu wa tatu pekee baada ya Don Budge na Rod Laver kushinda mataji manne makuu kwa wakati mmoja, na mtu wa nane kushinda katika mashindano ya Wimbledon na French, US na Australian Opens. Mserbia huyo mwenye umri wa miaka 29 alielezea fahari ya kishinda taji la French Open "Ilikuwa mojawapo ya mambo yanayotokea wakati unapojaribu tu kuwa mahali pale. Ni kama roho imeondoka katika mwili wangu na nikauacha mwili wangu upambane katika hatua za mwisho mwisho, kwenda kushoto hadi kulia na kutaraji Andy atafanya kosa, na kweli likatokea. Ni tukio la kuvutia na mojawapo ya matukio ya kifahari katika taaluma yangu"

Djokovic bado yuko nyuma ya gwiji wa Uswisi Roger Federer na Mhispania Rafael Nadal katika idadi ya mataji makuu waliyoshinda lakini hawajawahi kuwa na mataji manne ya grand slam kwa wakati mmoja.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Iddi Ssessanga