1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkwamo waongezeka ;Urusi yaonya vikwazo vitawarudia walioviweka

8 Machi 2014

Urusi imesema kuwa vikwazo vyovyote vya Marekani vitakavyowekwa dhidi yake kuhusiana na mzozo wa Ukraine vitairudia Marekani na kwamba jimbo la Crimea lina haki ya kuamua mustakabali wake

https://p.dw.com/p/1BM5l
Ukraine Krim Sewastopol Russischer Soldat
wanajeshi wa Urusi ndani ya UkrainePicha: Reuters

Wakati huo huo watu wenye silaha wamekamata kituo kingine cha kijeshi cha Ukraine katika eneo hilo la rasi.

Katika mazungumzo kwa njia ya simu na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John kerry, waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov ameonya dhidi ya "hatua za haraka na zisizo na mipango" ambazo zinaweza kuathiri uhusiano kati ya Urusi na Marekani, imesema wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi jana Ijumaa (07.03.2014).

Solidaritätskonzert in Moskau für die Krim 07.06.2014
Maandamano ya kuunga mkono Urusi mjini MoscowPicha: picture-alliance/dpa

"vikwazo, ni dhahiri kuwa vitaiathiri Marekani pia", taarifa hiyo imesema.

Waendelea na majadiliano

Kerry amesisitiza umuhimu wa kutatua hali hiyo kupitia njia za kidiplomasia na kusema yeye pamoja na Lavrov wataendelea kufanya mashauriano, wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imesema.

Ilikuwa ni majibizano ya pili katika ngazi ya juu kati ya mahasimu hao wa wakati wa vita baridi katika muda wa saa 24 zilizopita kuhusiana na hatua ya Urusi kulidhibiti eneo la Ukraine katika rasi ya Crimea.

Spanien Ukraine Russland Außenminister Segej Lawrow in Madrid
Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei LavrovPicha: Reuters

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema baada ya mazungumzo ya saa moja na rais wa Marekani Barack Obama kwamba msimamo wao kuhusiana na jimbo hilo la zamani la uliyokuwa muungano wa Kisoviet bado unatofautiana sana. Obama ametangaza vikwazo vya kwanza dhidi ya Urusi siku ya Alhamis.

Rais wa Urusi Vladimir Putin amefungua rasmi michezo ya walemavu ya olimpiki ya majira ya baridi , michezo ambayo imesusiwa na viongozi mbali mbali wa mataifa ya Ulaya , amesema maafisa wapya wa ukraine ambao wanapendelea mataifa ya ulaya wamechukua hatua kinyume na sheria kuhusiana na maeneo ya mashariki, kusini mashariki na Crimea.

Ukraine Krise Putin Kabinettssitzung 05.03.2014
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Reuters/Alexei Druzhinin/RIA Novosti

Ilitoa msaada

Urusi haiwezi kupuuzia miito ya kutakiwa kutoa msaada na imechukua hatua muafaka, kwa mujibu wa sheria za kimataifa," amesema.

Serhiy Adtakhov , msaidizi wa kamanda wa kikosi cha ulinzi wa mipakani nchini Ukraine, amesema wanajeshi 30,000 wa Urusi kwa sasa wako Crimea ikilinganishwa na wanajeshi 11,000 ambao wako katika vituo vya kijeshi vya Urusi katika eneo la bahari nyeusi katika bandari ya Sevastopol kabla ya mzozo huo.

Wizara ya ulinzi ya Marekani inakadiria kuwa zaidi ya wanajeshi 20,000 wa Urusi huenda wako katika jimbo hilo la Crimea.

Jana Ijumaa (07.03.2014) watu wenye silaha waliliingiza lori katika kituo cha ulinzi wa makombora cha Ukraine katika mji wa bandari wa Sevastopol, kwa mujibu wa ripota wa shirika la habari la Reuters ambaye yuko katika eneo hilo.

Lakini hakuna risasi zilizofyatuliwa na waziri mkuu wa Crimea ambaye anaiunga mkono Urusi amesema baadaye kuwa mkwamo umemalizika.

Putin anakana kuwa wanajeshi ambao hawana nembo ya taifa ambao wamewazingira wanajeshi wa Ukraine katika vituo vyao kwamba wanaongozwa na Urusi, licha ya kuwa magari yao yana namba za jeshi la Urusi. Mataifa ya magharibi yamefanya kichekesho matamshi yake hayo.

Ukraine Russland Krim-Krise Obama 06.03.2014
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: picture-alliance/dpa

Mzozo huo mkubwa kati ya mataifa ya mashariki na magharibi tangu kumalizika kwa vita baridi umeongezeka siku ya Alhamis wakati bunge la Crimea , likiwa na wajumbe wengi ambao ni wa asili ya Urusi , lilipopiga kura kujiunga na Urusi na kupanga kura ya maoni itakayofanyika Machi 16.

Mzozo huo umetokana na kuangushwa mwezi uliopita kwa rais Victor Yanukovich baada ya maandamano mjini Kiev ambayo yamesababisha ghasia.

Uturuki nayo yajihami

Uturuki iliamuru ndege zake za kijeshi kuruka haraka baada ya ndege ya uchunguzi ya Urusi kuruka katika eneo la pwani ya bahari nyeusi na meli ya kivita ya Marekani kupita katika ujia wa baharini wa Bosphorus nchini Uturuki wakati ikielekea katika bahari nyeusi, licha ya kuwa jeshi la Marekani limesema kuwa meli hiyo ya kivita ilikuwa katika safari zake za kawaida.

Russland Armee Ukraine Krim Kriegsschiffe
Meli za kivita za Urusi katika eneo la CrimeaPicha: picture-alliance/dpa

China wakati huo huo imetoa wito wa utulivu na kujizuwia katika mzozo huo wa Ukraine, ikisema kuwa suala hilo linapaswa kutatuliwa kwa njia za mazungumzo na za kisiasa.

Maandamano mapya ya kuiunga mkono Urusi katika mji wa mashariki wa Donetsk baada ya Urusi kutishia kusitisha ugavi wa gesi nchini humo yanapangwa , na kuendeleza zaidi uhasama na mataifa ya magharibi.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre

Mhariri: Iddi Ssessanga