Mkuu wa majeshi wa Lesotho auawa | Matukio ya Afrika | DW | 06.09.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

LESOTHO

Mkuu wa majeshi wa Lesotho auawa

Mkuu wa majeshi wa Lesotho, Khoantle Mots'omots'o, na maafisa wengine wawili wa ngazi za juu wamepigwa risasi na kuuawa wakiwa kwenye kambi ya jeshi, inasema serikali ya taifa hilo dogo kusini mwa Afrika.

Ingawa bado haijafahamika lengo la mauaji hayo ya jana (Septemba 5), nchi hiyo ya kifalme imekuwa ikikumbwa na mapinduzi ya kijeshi ya mara kwa mara yakifuatiwa na machafuko ya kisiasa tangu kupata uhuru wake kutoka Uingereza mwaka 1966. 

Kanali Tenki Mothae, katibu mkuu wa wizara ya ulinzi, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba maafisa wawili hao wa ngazi za juu jeshini walikuwa wanachunguzwa kutokana na mauaji ya kamanda mwengine wa kijeshi mwaka 2015.

Waziri Mkuu Thomas Thabane, aliyewahi kuikimbia nchi hiyo mwaka 2014 baada ya jaribio la mapinduzi na ambaye mkewe aliuawa kwa risasi mwezi Juni mwaka huu, hakutoa undani kuhusu mauaji hayo alipoongea na waandishi wa habari akisema kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Si Mothae wala waziri mkuu walioweza kuthibitisha ripoti za vyombo vya habari vya Afrika Kusini kwamba maafisa hao wawili ndio waliomuuwa mkuu wa majeshi, kisha nao wakauawa kwenye urushianaji risasi na wanajeshi wenzao.

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, taifa ambalo limeizunguka Lesotho pande zote, alilaani mauaji hayo huko akitoa wito wa utulivu na kutolipiza kisasi. 

Lesotho ndiye msambazaji mkubwa wa maji yanayotumiwa ndani ya maeneo ya viwanda nchini Afrika Kusini.

Zuma alisema pia kuwa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) itatuma ujumbe wa mawaziri kuchunguza hali ya mambo ilivyo nchini Lesotho.

Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, amekuwa akifanya ziara za mara kwa mara nchini Lesotho kujaribu kufikia makubaliano ya kisiasa kati ya pande hasimu kwa niaba ya SADC.

Tangu jaribio la mapinduzi la mwaka 2014, Lesotho imefanya chaguzi tatu, ukiwemo wa Juni, na zote hazikuweza kutoa mshindi wa wazi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga