1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano juu ya usalama.

Abdu Said Mtullya6 Februari 2009

Mkutano juu ya masuala ya usalama umeanza leo mjini Munich ,ambapo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel pia anashiriki.

https://p.dw.com/p/GohL
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier aliefungua mkutano wa Munich leo.Picha: AP

Mkutano muhimu wa  kila mwaka  juu ya usalama  wa dunia umeanza leo mjini Munich ambapo Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa  wanashiriki. Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden pia anashiriki kwenye mkutano huo.

Viongozi wa nchi na serikali wanaohudhuria mkutano huo wa siku tatu uliofunguliwa  na waziri  wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier wanajadili masuala  ya kupunguza silaha, mgogoro wa Mashariki ya Kati, hali ya nchini Afghanistan na mzozo wa nyuklia wa Iran.

Kufuatia kuingia madarakani kwa rais Barack Obama pana matumaini makubwa  juu ya mkutano huo kuweza kumaliza zama za uhusiano wa mashaka mashaka baina ya Marekani na Urusi. Hatahivyo Urusi inawakilishwa na naibu waziri wa mambo ya nje kwenye mkutano huo Sergei Ivanov.

Kwa muda mrefu Marekani imekuwa inashiriki kwenye mikutano hiyo kwa kupeleka  wajumbe wa  ngazi  za uwaziri lakini  safari hii makamu wa rais wa nchi hiyo Joe Biden anashiriki mjini Munich.

Wachunguzi wa masuala ya kimataifa wanasema hiyo ni ishara ya dhamira ya utawala mpya wa Marekani juu ya kuleta mabadiliko katika sera  zake za nje.

Bwana Biden, hapo baadae atawahutubia wajumbe  zaidi ya mia tatu kutoka nchi zipatazo 50, wanaojadili masuala ya  upunguzaji wa silaha za nyuklia,Iran na Korea  ya kaskazini.

Katika hotuba yake bwana Biden anatarajiwa kufahamisha juu ya mtazamo mpya kuhusu  mpango wa Marekani wa kuweka mtandao  wa ulinzi wa makombora.

Utawala wa Marekani wa hapo awali ulikuwa unakusudia kutandaza mtandao huo barani Ulaya kwa kuhoji kwamba una lengo la kukabili hatari kutoka Iran.Lakini mpango huo   umeikasirisha Urusi.

Mjumbe wa Iran Ali Larijani anaeuhudhuria mkutano wa mjini Munich atashiriki kwenye   mjadala juu udhibiti wa silaha na hususan juu ya sialha za nyuklia.

Lakini ameazimia kutozungumzia mpango wa nyuklia wa nchi yake. Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton  ameashiria kuwa  atatumia fursa  zilizopo kushauriana na Urusi juu ya njia za kuzuia harakati  za kinyuklia za Iran.

Katika siku ya mwisho ya mkutano huo jumapili,wajumbe watajadili hali ya Afghanistan  ambapo majeshi  ya kimataifa  yanayoongozwa na  Nato yanashiriki katika  kulinda amani nchini humo.

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan pia anahudhuria mkutano wa mjini Munich....