1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa mawaziri wa fedha wa G7 kukamilika leo

18 Julai 2019

Mawaziri wa Fedha wa kundi la nchi 7 tajiri zaidi duniani, G7, wanatarajiwa kukamilisha mazungumzo yao kuhusu suala tata la kodi, kampuni kubwa za teknolojia na pendekezo la Facebook kuanzisha sarafu mpya ya kidijitali.

https://p.dw.com/p/3MFNs
Japan Treffen der G7-Finanzminister in Sendai
Picha: Reuters/Kyodo

Katika siku ya kwanza ya mkutano huo hapo jana uliowajumuisha pia magavana wa benki kuu ya G7, Waziri wa Fedha wa Ufaransa, Bruno Le Maire ana matumaini kwamba mawaziri hao watakubaliana kuhusu haja ya kudhibiti sarafu za kidijitali kama vile Libra ambayo imependekezwa na Facebook.

Mawaziri kutoka Marekani, Ufaransa na Ujerumani wameelezea wasiwasi wao kuhusu pendekezo hilo la Facebook, wakitolea mfano masuala kama vile viwango vya utakatishaji fedha na uhuru wa kila taifa.

Matumaini ya makubaliano kufikiwa

Le Maire amesema pia ana matumaini kwamba makubaliano ya kanuni kuhusu kiwango cha chini cha kimataifa au viwango vya ushuru, pamoja na mashirika ya kimataifa kuhakikisha kuna ufanisi katika ulipaji wa kodi, yatafanikiwa.

''Tumeona Marekani imechukua msimamo thabiti hivi karibuni na wamefanya uchunguzi 301 dhidi ya Ufaransa. Nataka kurudia tena kwamba hatutabadilisha huduma zetu za kodi ya kidijitali, kwa sababu uamuzi huu ulifanywa na watu wa Ufaransa kupitia bunge. Hata hivyo, kama jumuia ya kimataifa itafikia makubaliano yoyote, Ufaransa itaifuta,'' alisisitiza Le Maire.

Hata hivyo, waziri huyo wa fedha wa Ufaransa alikiri kuwa mazungumzo yao bado ni magumu kuhusu kodi na biashara za kidijitali.

Frankreich Chantilly G7 Finanzminstertreffen | Bruno Le Maire
Waziri wa Fedha wa Ufaransa, Bruno Le Maire Picha: Reuters/P. Rossignol

Tofauti na mvutano kati ya Marekani na Ufaransa wanaunga mkono kanuni za kuhakikisha kunakuwepo na kiwango cha chini cha kodi kama sehemu ya juhudi za miongoni mwa mataifa 139 za kufanyia marekebisho makubwa kanuni hizo za kimataifa za kodi.

Mawaziri hao wa Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Italia, Canada, Japan na Marekani pia watajadiliana kuhusu usawa, katika mkutano huo ambao unaandaa mkutano wa viongozi wa mataifa ya G7 utakaofanyika mwezi Agosti.

Wakati huo huo, Le Maire anatarajiwa kuongoza mazungumzo ya kutafuta mgombea mmoja wa kuchukua nafasi ya Christine Lagarde kuliongoza Shirika la Kimataifa la Fedha, IMF. Nafasi hiyo imewachwa wazi baada ya Lagarde kutajwa na viongozi wa Umoja wa Ulaya kuiongoza Benki Kuu ya Ulaya.

Duru zimeeleza kuwa majina ya wagombea kadhaa yamewasilishwa, lakini hadi sasa hakuna mtu yeyote ambaye amechaguliwa. Afisa wa Umoja wa Ulaya ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema wamekubaliana kuwa ni muhimu kuchagua jina moja na kuliwasilisha. Majina ya wagombea kadhaa yalijadiliwa, lakini hakuna orodha ya majina yaliyopendekezwa.