Mji wa Slaviansk wakombolewa;waasi watimka | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.07.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mji wa Slaviansk wakombolewa;waasi watimka

Jeshi la Ukraine Jumamosi (05.07.2014) limeuteka tena mji uliokuwa ngome kuu ya waasi wanaotaka kujitenga wa Slaviansk baada ya waasi wanaoiunga mkono Urusi kukimbia kufuatia mashambulizi makubwa ya kijeshi dhidi yao.

Wanajeshi wa Ukraine karibu na mji wa Slaviansk. (03.07.2014)

Wanajeshi wa Ukraine karibu na mji wa Slaviansk. (03.07.2014)

Meya wa mji huo Vladimir Pavlenko ameliambia shirika la habari la Urusi Interfax kwamba mashambulizi makubwa ya mizinga na ya anga yanayofanywa na majeshi ya Ukraine kwa siku kadhaa sasa yamepelekea waasi hao kuutekeleza mji huo muhimu kimkati wa wakaazi wa 110,000 mashariki ya nchi hiyo.

Mwandishi habari wa shirika la habari la Uingereza Reuters ameshuhudia msafara wa magari ya kijeshi takriban ishirini na mabasi yaliyojaa waasi wenye silaha yakiondoka kwenye mji wa Kramatorsk ambako walikimbia awali kutoka mji wa karibu wa Slaviansk ambayo ni ngome kuu ya waasi.

Waziri wa mambo ya ndani Arsen Avakov amesema idadi kubwa ya waasi wameukimbia mji wa Slaviansk kufuatia mfulululizo wa mashambulizi kutoka vikosi vya Ukraine.

Amesema katika taarifa kwenye mtandao wake wa Facebook kwamba idadi kubwa ya wanamgambo wameondoka Slaviansk na vikosi vyao vimekuwa vikiwashambulia wakati wakitimka na kwamba waasi hao wamepata hasara kubwa na wanasalimu amri.

Waasi wazidiwa nguvu

Wanajeshi wa Ukraine karibu na mji wa Slaviansk. (03.07.2014)

Wanajeshi wa Ukraine karibu na mji wa Slaviansk. (03.07.2014)

Duru ilio karibu na waasi imeliambia shirika la habari la Reuters kwamba waasi wamezidiwa kwa wingi na wanajeshi wa Ukraine yaani muasi mmoja kwa wanajeshi 50. Duru hiyo ikizungumza kwa shati ya kutotajwa jina imesema vikosi vya Ukraine vina idadi kubwa ya wanajeshi na zana za kijeshi.

Aleksandr Borodai kiongozi wa eneo lililojitangazia kuwa Jamhuri ya Wananchi la Donetsk amekaririwa na shirika la habari la Interfax akisema "Vikosi vya adhabu vya Ukraine vimefanya mashambulizi makubwa na kwa kuzingatia wingi wa idadi ya vikosi vya maadui vikosi vya Jamhuri ya Wananchi ya Donetsk vimelazimika kuondoka kwenye vituo vya awali katika sehemu ya kaskazini ya mstari wa mbele wa mapambano.

Rais wa Ukraine Petro Poroshenko baada ya kuarifiwa na mkuu mpya wa majeshi aliyeteuliwa hivi karibuni aliamuru kupeperushwa kwa bendera za Ukraine kwenye majengo ya serikali huko Slaviansk.

Bendera ya Ukraine baadae ilipepea kwenye jengo la halmashauri ya jiji kuchukuwa nafasi ya ile ya Urusi ambayo imekuwa ikipepea tokea waasi walipoyanyakuwa majengo muhimu ya serikali hapo mwezi wa Aprili.

Slaviansk ngome kuu ya waasi

Kikosi cha Ulinzi wa Taifa cha Ukraine huko Slaviansk.

Kikosi cha Ulinzi wa Taifa cha Ukraine huko Slaviansk.

Slaviansk ilikuwa ni ngome madhubuti ya wanamgambo wanaopambana na vikosi vya serikali mashariki ya Ukraine. Kukombolewa kwa mji huo utakuwa ushindi mkubwa wa kijeshi wa serikali ya Ukraine katika mapigano yake ya miezi mitatu ambayo yameuwa zaidi ya wanajeshi 200 wa Ukraine halikadhalika mamia ya raia na waasi.

Tovuti ya Poroshenko imesema wapiganaji hao wanaotaka kujitenga walikuja kushambuliwa kwa mizinga wakati walipojaribu kushambulia mlolongo wa vikosi vya serikali. Waasi wamepoteza kifaru kimoja na magari mengine ya deraya.

Taarifa kutoka tovuti hiyo imeongeza kusema kwamba majasusi wa jeshi la ulinzi na wanajeshi wa Ulinzi wa Taifa hivi sasa wanafanya shughuli zao Slaviansk.

Waasi wataka msaada wa Urusi

Waasi wanaotaka kujitenga kwenye viunga vya Slaviansk. (15.05.2014)

Waasi wanaotaka kujitenga kwenye viunga vya Slaviansk. (15.05.2014)

Mji wa Slaviansk ulikuwa ukizidi kujiamulia inavyotaka bila ya kutegemea makundi ya waasi yenye kudhibiti Donetsk kitovu cha viwanda mashariki ya Ukraine na mji wa Luhansk na mara nyingi ukiukaji wa waasi wa usitishaji wa mapigano wa serikali uliomalizika muda wake hapo Jumatatu umekuwa ukitokea katika mji huo wa Slaviansk.

Hapo Ijumaa kiongozi wa kijeshi wa waasi katika mji huo Igor Strelkov ametowa wito wa dharura wa kutaka msaada kutoka Urusi nchi ambayo serikali ya Ukraine inailaumu kwa kuchochea ghasia mashariki mwa nchi hiyo.Amesema bila ya msaada wa Urusi eneo hilo linalodaiwa na waasi lijulikanalo kama Novoirossiya (Urusi Mpya) litatekwa na vikosi vya serikali ya Ukraine.

Ameandika katika tovuti ya waasi "Slaviansk itaanguka mapema kabla ya miji mengine".

Serikali ilianzisha mashambulizi mapya dhidi ya waasi wanaotaka kujitenga hapo Jumanne baada ya Poroshenko kukataa kurefusha muda wa kusitisha mapigano uliokuwa umemalizika.

Serikali za Urusi,Ufaransa na Ujerumani zimeitaka serikali ya Ukraine na waasi kuzingatia tena usitishaji wa mapigano.

Mwandishi : Mohamed Dahman /Reuters/AFP/dpa

Mhariri : Bruce Amani

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com