1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Milio ya risasi yasikika karibu na Ikulu Conakry

Saumu Mwasimba
5 Septemba 2021

Wanajeshi wamemwagwa kuzunguuka eneo la Ikulu katika mji wa Kalouma ulioko jirani na mji mkuu Conakry

https://p.dw.com/p/3zwLi
Guinea Ausschreitungen nach Bekanntgabe der vorläufigen Ergebnisse in Conakry
Picha: John Wessels/AFP

Milio ya risasi imesikika katika mji mkuu wa Guinea,Conakry Jumapili asubuhi kwa mujibu wa shahidi wa  shirika la habari la Reuters na vidio zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Duru za jeshi zinasema daraja pekee linalounganisha upande wa eneo kubwa la nchi na mji wa Kalouma ambako kuna makaazi ya mawaziri wengi pamoja na ikulu ya rais limefungwa na wanajeshi chungunzima wengine wakiwa na silaha wamepelekwa katika eneo linalozunguka makaazi ya rais.

Afisa wa ngazi ya juu serikalini, amefahamisha kwamba rais Alpha Conde hakujeruhiwa lakini hakutoa maelezo zaidi ya hayo.Ingawa vidio ambayo haijathibitishwa inasambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha rais Conde amekamatwa na kikosi maalum cha jeshi. Kituo cha Televisheni ya taifa kimepiga muziki na kuonesha vipindi lakini hakikutangaza habari yoyote kuhusu mashambulizi yaliyotokea. Shahidi mmoja wa shirika la habari la reuters amesema aliona raia waliokuwa na majeraha ya kupigwa risasi. Ufyetuaji risasi huo karibu na makaazi ya rais umeibua wasiwasi wa kiusalama katika nchi hiyo ambayo ina historia ya muda mrefu ya jeshi kutwaa madaraka na majaribio ya mapinduzi.

Guinea Präsidentschaftswahlen | Alpha Conde
Picha: John Wessels/AFP

Haikufahamika haraka ikiwa rais Conde alikuwa nyumbani wakati mashambulio hayo ya risasi yalipoanza katika mji wa Kaloum ulioko nje ya Conakry.

Rais Conde amekuwa akikabiliwa na hatua za kumkosoa tangu alipoamua kugombea muhula wa tatu mwaka jana akisema kifungu cha katiba kinachoweka ukomo wa muhula hakimgusi. Ikumbukwe Conde alichaguliwa tena lakini hatua hiyo ilichochea vurugu kubwa za maandamano mitaani na upinzani ulisema watu chungunzima waliuwawa.

Conde aliingia madarakani mwaka 2010 katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini humo tangu ilipojipatia Uhuru kutoka kwa wafaransa mnamo mwaka 1958.

Wengi waliuona uongozi wake kama mwanzo mpya wa taifa hilo ambalo kwa miongo lilifunikwa na rushwa,na utawala wa kimabavu.Ingawa wapinzani wanasema ameshindwa kuimarisha maisha ya Waguinea ambao wengi wanaishi kwenye umasikini mkubwa licha ya nchi yao kuwa na utajiri mkubwa sana wa madini. Mwaka 2011 alinusurika jaribio la kumuua baada ya wanajeshi waasi kuishambulia ikulu.

Mwandishi: Saumu Mwasimba