1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbeki azuru Darfur

Jane Nyingi/ AFPE..Picha AFP2 Aprili 2009

Mbeki akutana na maafisa wa serikali mjini Khartoum kabla ya kusafiri Darfur

https://p.dw.com/p/HP80
Aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Thabo MbekiPicha: AP

Aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki, na ambae hivi sasa anaongoza jopo la Umoja wa Afrika kuhusu mgogoro wa jimbo la Darfur hii leo yuko nchini Sudan kwa mazungumzo kuhusu mgogoro huo. Mbeki atakutana na maafisa wa serikali mjini Khartoum kabla ya kusafiri Darfur kwa mfululizo wa mikutano. Wakati huo huo mjumbe wa Marekani Scott Gration ameanza ziara yake mjini Khartoum, kwa mwito wa ushirikiano thabiti kati ya Marekani na Sudan.


Bw Mbeki atakutana na maafisa wa serikali mjini Khartoum na baadae kuelekea Darfur kwa mikutano kadhaa pamoja na wawakilishi wa watu walioyakimbia makaazi yao pamoja na viongozi wa ngazi ya juu wa kikosi cha pamoja cha umoja wa mataifa na Afrika cha kusimamia amani darfur-UNAMID.


Sudan iliyafukuza mashirika kadhaa ya kutoa misaada, katika jimbo hilo lililoharibiwa kwa vita, baada ya mahakama ya uhalifu wa kivita kutoa waranti ya kukamatwa rais wa Sudan Omar Hassan al Bashir mwezi uliopita.


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon ameitaka serikali ya Sudan kubatilisha uamuzi wake wa kuyatimua mashirika 13 ya misaada. Umoja wa Afrika, ulipinga vikali hatua ya mahakama hiyo ya kimataifa ilioko mjini The Hague, Uholanzi kuhusiana na warranti huo dhidi ya rais Bashir, ukisema utavuruga juhudi za amani katika taifa hilo kubwa kabisa barani Afrika.


Wakati huo huo mjumbe mpya wa rais Barack Obama wa Marekani, Scott Gration amesema Marekani na Sudan zinataka kuwa washirika, kwa kutafuta nafasi zitakazoujenga uhusiano imara kati ya nchi hizo mbili . Katika siku yake ya kwanza ya ziara yake nchini Sudan, Gration aliwaambia waandishi wa habari kuwa amewasili nchini humo mikono yake ikiwa wazi na litakua jukumu la serikali ya Sudan kuamua inavyotaka kuendeleza uhusiano huo.


Mjumbe huyo wa Marekani aliwasili mapema jana, jumatano kwa ziara ya wiki nzima, ikiwa ni mwezi mmoja baada ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita kutoa waranti ya kukamatwa kwa rais Bashir kwa tuhuma za uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur.


Mjumbe huyo wa Marekani amekutana na afisa wa ngazi ya juu katika wizara ya mambo ya nje nchini Sudan Mutrif Siddiq, na huenda akakutana pia na rais al bashir.Gration anatazamiwa kusafiri Darfur mwishoni mwa juma


Rais Obama baada ya kukutana na Bw Gration jumatatu wiki hii, alielezea matumaini ya kutafuta njia za kuwarejesha wafanyakazi wa mashirika ya misaada katika eneo hilo la mashariki mwa nchi hiyo.


Mashirika ya kimataifa ya kutoa misaada huwahudumia watu wapatao millioni 2.7 ambao waliyakimbia makaazi yao kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe huko Darfur, kwa kuwapa chakula, maji na kutoa huduma za matibabu.



Kwa upande wake Rais al- Bashir wa Sudan amesimama kidete akiutetea uamuzi wake wa kuyatimua mashirika ya kutoa misaada katika jimbo la Darfur.



Jane Nyingi