Mauaji ya wakimbizi Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.10.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mauaji ya wakimbizi Syria

Marekani imefadhaishwa na ripoti kwamba serikali ya Syria imedondosha mabomu ya mapipa kwenye kambi ya wakimbizi katika mji wa Idlib na kuliita shambulio hilo kuwa mauaji makubwa ya kinyama

Wananchi wakiyakimbia mapigano katika mji wa kaskazini magharibi wa Idlib 2012.

Wananchi wakiyakimbia mapigano katika mji wa kaskazini magharibi wa Idlib 2012.

Mkanda wa video uliowekwa kwenye mtandao wa Youtube umeonyesha maiti za wanawake, watoto na mahema yaliokuwa yakiwaka moto wakati watu wakiwa mbioni kuwaokowa wale waliojeruhiwa.

Sauti kutoka kwenye mkanda huo imesikika ikisema hayo yalikuwa mauaji ya wakimbizi na ikitaka dunia ishuhudie mauaji hayo ya raia,ya watu waliopotezewa makaazi yao ambao walikuwa wameyakimbia mashambulizi ya mabomu.

Mtu kwenye mkanda mwengine wa video katika kambi ya Abidin yenye kuhifadhi watu waliokimbia mapigano katika jimbo jirani la Hama amesikika akisema kwamba watu wanaofikia sabini na tano wameuwawa katika shambulio hilo.

Vyombo vya habari vya serikali havikulitaja shambulio hilo katika taarifa zake.Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu lenye makao yake mjini Uingereza ambalo linachunguza umwagaji damu katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria limesema watu 10 wameuwawa.

Marekani yafadhaishwa

Jen Psaki msemaji wa wizara ya Mambo ya nje ya Marekani.

Jen Psaki msemaji wa wizara ya Mambo ya nje ya Marekani.

Marekani imesema imefadhaishwa na repoti hizo lakini haikuweza kuthibitisha undani wake.Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Jen Psaki amesema katika taarifa iwapo itathibitishwa hiyo ilikuwa ni kazi ya utawala wa Assad itakuwa tu ni hatua ya karibuni kabisa ya ukatili unaofanywa na utawala huo dhidi ya raia wake wenyewe.

Takriban watu milioni 10 wamepotezewa makaazi yao kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria ambavyo vilianza na maandamano ya kudai dermokrasia na kuja kugeuka kuwa uasi uliohusisha matumizi ya silaha wakati vikosi vya usalama vilipotumia nguvu kuvunja maadamano dhidi ya serikali.

Zaidi ya watu milioni 3 wameikimbia nchi hiyo na mzozo huo umeuwa takriban watu 200,000 kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Nchi jirani zaemewa

John Ging Mkuu wa Kuratibu Masuala ya Kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa.

John Ging Mkuu wa Kuratibu Masuala ya Kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa.

Mkurugenzi wa operesheni za kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa ameonya kwamba baadhi ya nchi jirani na Syria ziko katika hali ya kuelemewa kupindukia wakati zikiwajibika kuiacha mipaka yake wazi kwa wakimbizi na wakati huo huo kuwajibika kwa wananchi wake wenyewe.

John Ging amesema hapo jana kwamba Lebanone,Uturuki na Jordan yumkini zikaendelea kuwa na wakimbizi kwa miaka mingi ijayo.

Kauli yake hiyo inakuja siku moja baada ya Jordan na Lebanon kuueleza mkutano wa kimataifa kwamba mmiminiko wa wakimbizi nchini mwao unamaliza rasilmali zao na kutishia utulivu wa kisiasa.

Katika kesi ya Lebanon wakimbizi wamesababisha ongezeko la asilimia 25 la idadi ya watu wa nchi hiyo.

Wakati huo huo Australia leo hii imepitisha sheria yenye kulifanya kuwa kosa la jinai kusafiri kwennda kwenye maeneo yenye harakati za kigaidi hiyo ikiwa ni hatua kali kabisa ya kupambana na ugaidi yenye nia ya kuwazuwiya wapiganaji wa jihadi kwenda kupigana nchini Iraq na Syria.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com