1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya magharibi kuisusia Urusi kisiasa

2 Machi 2014

Balozi wa Ukraine katika Umoja wa Mataifa ameomba kikao cha dharura cha Baraza la Usalama ili kufanya kila linalowezekana kuzuwia uvamizi wa Urusi, wakati vikosi vya jeshi la nchi hiyo vikidhibiti jimbo la Crimea.

https://p.dw.com/p/1BI7R
Turtschinow / Jazenjuk / Ukraine
Viongozi nchini UkrainePicha: Reuters

Lakini hatua hazionekani kuwa zinaweza kuchukuliwa na chombo hicho chenye nguvu cha Umoja wa Mataifa. Kama mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama, Urusi ina nguvu za karata ya turufu na inaweza kuzuwia baraza hilo kuidhinisha azimio lolote litakalokosoa ama kuiadhibu nchi hiyo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amemtaka Rais Vladimir Putin katika mazungumzo kwa njia ya simu "kuanza mazungumzo ya ana kwa ana na maafisa wa serikali mjini Kiev."

UN Generalsekretär Ban Ki-moon München Sicherheitskonferenz Bayern 2014
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moonPicha: Reuters

Hali ni ya hatari Ukraine

Akiita hali nchini Ukraine kuwa "ya hatari na inayodhoofisha amani", balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Samantha Power, ameliambia Baraza hilo kuwa "umefika wakati kwa uvamizi wa jeshi la Urusi nchini Ukraine kusitishwa."

Power na wajumbe wengine wa Baraza hilo wametoa wito wa kutumwa kwa wakaguzi wa kimataifa nchini Ukraine haraka iwezekanavyo kuangalia hali nchini humo, na Power ameonya kuwa "hatua za uchokozi za Urusi zinaweza kirahisi kuipeleka hali hiyo kupindukia hali ya kuporomoka kabisa." Pia ametaja kuhusu kazi za ujumbe wa upatanishi wa kimataifa kutumwa nchini Ukraine.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitishwa kwa kikao cha dharura kwa mara ya pili mfululizo kuhusiana na hali ya matukio inayokwenda kasi nchini Ukraine.

Baraza hilo pia lilikutana kwa muda mfupi katika kikao cha wazi, kikao kilichoonyeshwa katika televisheni, licha ya upinzani kutoka Urusi, na baadaye kilifanya tena mkutano wake kwa faragha.

Ukraine Russland Konflikt Krim 1. März 2014
Wanajeshi wa Urusi wakiwa nchini UkrainePicha: REUTERS

Obama aionya Urusi

Wakati huo huo, Rais Barack Obama alimweleza Rais Vladimir Putin wa Urusi jana Jumamosi (01.03.2014) kuwa hatua ya nchi hiyo kutuma wanajeshi nchini Ukraine ni kitendo cha ukiukaji wa sheria za kimataifa na ameonya kuwa anatafakari kuitenga nchi hiyo kisiasa iwapo hatua hiyo ya Urusi itaendelea.

Obama pia ameelezea kuhusu haki ya watu wa Ukraine kuamua hatima yao na kuanza kimsingi kuwaweka pamoja washirika wake wa mataifa ya magharibi dhidi ya Urusi, na kuwapigia simu viongozi wa Ufaransa na Canada.

Ukraine Russland Konflikt Krim 1. März 2014
Wanajeshi katika mzozo huo wa ukrainePicha: REUTERS

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, John Kerry, pia alifanya mazungumzo na mawaziri wengine sita kutoka mataifa ya Ulaya na Canada pamoja na Mkuu wa Sera za Mambo ya Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, pamoja na balozi wa Japan nchini Marekani, kuratibu hatua itakayochukuliwa baadaye.

Rais Obama alimpigia simu Rais Francois Hollande wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Canada, Stephen Harper, viongozi wa mataifa ya upande wa pili wa Bahari ya Atlantic ikiwa ni pamoja na Uingereza ambazo ni uti wa mgongo wa upinzani wa baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia dhidi ya Urusi.

Obama / Telefon / Gespräch mit Putin / Krim / Oval Office
Rais Obama akizungumza na viongozi wengine kwa simuPicha: picture-alliance/dpa

Canada kwa upande wake imesema inamuondoa balozi wake kutoka Urusi kuhusiana na mzozo huo wa Ukraine. Taarifa ya Waziri Mkuu Stephen Harper baada ya kikao cha dharura cha baraza la mawaziri imesema Canada pia itasusia mkutano wa mataifa manane tajiri utakaofanyika mjini Sochi nchini Urusi mwezi Juni.

Harper anashutumu vikali uingiliaji kati kijeshi wa Urusi nchini Ukraine na amemtaka Rais Putin kuondoa majeshi hayo.

Mwandishi: Sekione Kitojo/ape/afpe

Mhariri: Mohammed Khelef