Mashabiki wa soka Ujerumani wapambana na Corona | Michezo | DW | 04.04.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Mashabiki wa soka Ujerumani wapambana na Corona

Wakati Arminia Bielefeld ilipania kusonga mbele katika Bundesliga mashabiki wa Stuttgart ambao ni wapinzani wao hawakujua hiyo itakuwa mechi yao ya mwisho kabla shughuli za kijamii kupigwa marufuku kutokana na corona.

Nchini Ujerumani wakati klabu ya kandanda ya Arminia Bielefeld ilicheza kuwania kusonga mbele katika ligi ya Bundesliga mnamo mwezi Machi mwaka huu, mashabiki wa timu ya Stuttgart ambao ni wapinzani wao hawakujua kwamba huo utakuwa ni mchezo wao wa mwisho kabla ya shughuli mbalimbali za kijamii kupigwa marufuku kutokana na mripuko wa virusi vya Corona.

Wiki moja baadaye mechi za Bundesliga zilisimamishwa nchini Ujerumani na chama cha mashabiki wa klabu ya Stuttgart walijielekeza zaidi katika kusaidia wazee na walio katika mazingira magumu wakati wa shida ya kiafya iliyotokea kufuatia janga la mripuko wa virusi vya Corona.

"Watu wengi wako tayari kwa ajili ya kuweka umakini wao kwa upande mmoja na kuja pamoja kuisaidia jamii," Clemens Knoedler wa kundi la wanachama wa Stuttgart Schwabensturm aliliambia Shirika la habari la AFP.

"Wiki moja baada ya mchezo wa Bielefeld ilibainika wazi kwamba kuna kitu kitakachobadilika. Tulikutana na kujiuliza wenyewe tutafanya nini."

Pamoja na makundi ya wachangiaji wengine nchini kote Ujerumani, Knoedler na wachama wenzake mashabiki waliamua kuhamasisha jamii yao.

Wakati ambapo aliwaongoza maelfu ya mashabiki wa Stuttgart katika kushangilia timu yao ya soka, Knoedler sasa anaandaa karibu watu wa kujitolea 80 kuchukua mboga na dawa ili kwenda kuwasaidia wale ambao hawawezi kutoka majumbani mwao. 

Fans Zuschauer Mundschutz (picture-alliance/Pressefoto Baumann/Augenblick)

Mashabiki wakiwa wamefunika midomo yao wakitazama mechi kati ya VfB Stuttgart na TSG Hoffenheim wakati wa corona

Mpango huo umekwishaenea ndani ya siku chache na kwa sasa ukitapakaa katika wilaya sita tofauti katika mji wa Stuttgart na maeneo jirani.

"Tunafanya hivi kwa ajili ya jiji letu na mkoa wetu. Hiyo ni moja ya sehemu ya uelewa wetu kama kikundi cha wanachama wa mashabiki, kwamba tupo tayari kusaidia jamii kadri ya uwezo wetu," alisema Knoedler.

Wakijulikana katika uhamasishaji wao wa nguvu na upingaji uwanjani kikundi hicho cha wanachama wamejiweka mbele kama utamaduni wa mashabiki maarufu wa soka nchini Ujerumani.

Mashabiki wabadili matendo yao

Mapema mwaka huu, vikundi vya mashabiki vilishambuliwa kwa maandamano yasiyofaa dhidi ya mmiliki wa klabu ya Hoffenheim, Dietmar Hopp, ambaye alitolewa maneno ya dhihaka kama "mtoto wa malaya" katika viwanja vya soka nchini Ujerumani.

Mkurugenzi mtendaji wa klabu ya Bayern Munich, Karl-Heinz Rummenigge, alisema kuwa vikundi hivyo vya mashabiki vimeonyesha taswira mbaya ya kabumbu la hapa Ujerumani, lakini katika wiki za hivi karibuni wameonyesha utofauti na matendo yao.

Mashabiki katika vilabu vikubwa vya kandanda kama vile Borussia Dortmund na Schalke 04 nao pia wameandaa kujitolea katika huduma za kijamii kama walivyofanya wale wa Stuttgart, wakati mashabiki wa klabu ya Bayern Munich wameitisha bakuli kwa ajili ya kuchangia hazina ya chakula.

Miundo mbinu iliyoshikamana ya vikundi hivyo vya mashabiki wa soka nchini Ujerumani, inafanya iwe rahisi kupanga kwa haraka na kulitekeleza jambo mara moja wakati wa shida, Knoedler aliiambia AFP.

Tangu mwaka 2013, kikundi chake mwenyewe kimekwishakutoa michango ya kila mwaka kwa ajili ya kuisaidia jamii kama vile watoto na vituo vya kuwasaidia watu wanaoishi katika mazingira magumu. 

1. FC Union Berlin steigt in 1. Fußball-Bundesliga auf (picture-alliance/dpa/Bildfunk/A. Gora)

Mashabiki wa Union Berlin wakishangilia baada ya klabu yao kupanda daraja 27.05.2019

Kwingineko nchini Ujerumani wapenzi na mashabiki wa kandanda wamekuwa wakichangia michango midogo midogo kwa ajili ya mapambano dhidi ya mripuko wa virusi hatari vya Corona.

Katika majiji mbalimbali nchini kote Ujerumani vikundi vya wanachama mashabiki wa soka wamekuwa wakishika mabango nje ya hospitali na maduka makubwa.

Mara nyingi walitumika kushika mabango na kuonyesha kupinga masuala ya kisiasa au mambo mengine ambayo hawakubaliani nayo, lakini kwa sasa mabango yao yakibeba ujumbe wa kuwasaidia walioko mstari wa mbele kupambana na janga hatari la mripuko wa virusi vya corona ambavyo hadi hivi sasa vimekwishaua zaidi ya watu 40,000.

Wakati hayo yakichomoza klabu ya soka ya Union Berlin, imewapatia mashabiki nafasi ya kununua bia na soseji za mtandaoni ili kuweza kuchangia katika masuala ya kijamii, wazo ambalo pia limeenea kwenye vilabu vingine nchini humu.

Na watani wa jadi wa Union Berlin, BFC Dynamo wamekwenda mbali zaidi. Timu hiyo inayocheza katika daraja la nne inauza tiketi za kutizama mechi tu ya kifikra dhidi ya "klabu inayochukiwa zaidi hapa Ujerumani": timu fulani inayoitwa "FC Corona Covid-19".

Mwandishi: Deo Kaji Makomba/AFP

Mhariri: Josephat Charo