Marubani Lufthansa wakataa pendekezo la malipo
26 Novemba 2016Shirika la Lufthansa limesema hapo mapema limetoa pendekezo kujaribu kuvunja mkwamo katika mzozo wa muda mrefu wa malipo ya nyongeza ya mshahara na marubani wa shirika hilo ambao wamekuwa katika mgomo tangu Jumatano.
Mgomo wa wiki hii, wa 14 tangu mapema mwaka 2014, tayari umesababisha kusitishwa kwa karibu safari 2,600 na kuathiri zaidi ya wasafiri 315,000. Lufthansa imesema hali hiyo ya kuvurugika kwa safari imeanza kuathiri maombi ya safari kwa kipindi cha kati.
Wasi wasi kwa wawekezaji
Marubani walitishia kurefusha mgomo wao kupindukia leo Jumamosi, wakiongeza wasi wasi miongoni mwa wawekezaji kwa kupanda kwa gharama za kampuni hiyo na athari kubwa zaidi katika nchi ya Ujerumani yenye uchumi mkubwa katika bara la Ulaya.
Lakini chama hicho cha wafanyakazi marubani kimesema jioni ya jana Ijumaa kwamba haina mpango wa kuendelea na mgomo kupindukia siku ya Jumamosi.
Haikuondoa hata hivyo uwezekano wa kuchukua hatua nyingine kama hiyo hapo baadaye, lakini chama hicho kimesema mgomo mwingine wowote utatangazwa masaa 24 kabla.
Chama hicho kimepuuzia pendekezo la hivi karibuni la shirika hilo la ndege na kusema ni "hatua ya kimahusiano na umma tu" na kusema si jambo jipya.
Lufthansa imesema imetoa pendekezo la kuongeza mshahara kwa asilimia 4.4 kwa awamu mbili , pamoja na malipo ya mwezi mmoja sawa na mshahara wa mwezi kwa asilimia 1.8.
Lufthansa yaahidi
Shirika hilo pia lilisema limependekeza kutengeneza nafasi za kazi 1,000 kwa marubani vijana na hadi nafasi 600 za marubani wanafunzi katika muda wa miaka mitano ijayo. Shirika limesema linaweza kuingia katika mazungumzo ya upatanishi na chama cha wafanyakazi marubani kuanzia Novemba 29.
Kwa upande wake , marubani watalazimika kukubali kubadilika kwa mpango wa mafao yao ya uzeeni , ambapo Lufthansa itawakikisha malipo ya mchango wao tu.
Wafanyakazi wa kutoa huduma katika ndege pamoja na wafanyakazi wa uwanja wa ndege tayari wamekubaliana na mabadiliko haya. Bettina Volkens , mkuu wa idara ya nguvu kazi katika shirika hilo, amesema mabadiliko hayo yatasaidia shirika hilo kuhifadhi fedha.
Chama cha wafanyakazi kinataka wastani wa ongezeko la mishahara kwa mwaka la asilimia 3.7 kwa marubani 5,400 nchini Ujerumani katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2012.
Lufthansa linasema linabidi kupunguza gharama za uendeshaji ili kuweza kushindana na mashirika mengine kama Ryanair katika njia za safari fupi na Emirates katika safari ndefu, licha ya kupata faida kubwa katika mwaka 2015.
Marubani wa Lufthansa wanalipwa vizuri kwa kiwango cha tasnia hiyo ya safari za anga. Rubani katika shirika la Lufthansa analipwa kiasi cha euro 180,000 kwa mwaka kabla ya kodi , licha ya kuwa rubani katika kiwango cha juu cha malipo anaweza kupata hadi euro 22,000 kwa mwezi kabla ya kodi.
Shirika la Lufthansa limesema hapo kabla kwamba litalazimika kufuta safari nyingine 137 zaidi leo Jumamosi, ikiwa ni pamoja na safari 88 za mbali , na kuwaathiri kiasi ya wasafiri 30,000. Shirika hilo pia limesema baadhi ya safari fupi na za kati pia zitaathirika.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Sylvia Mwehozi