Marianne Birther akosolewa | Magazetini | DW | 14.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Marianne Birther akosolewa

Patashika baada ya kufichuliwa hati inayoruhusu risasi zifyetuliwe katika Ujerumani Mashariki ya zamani.

Mada moja tuu ndio iliyohanikiza magazeti ya Ujerumani hii leo:mjadala uliozuka baada ya kugunduliwa hati inayoruhusu watu kufyetuliwa risasi katika Ujerumani mashariki ya zamani.

Tuanzie kusini mwa Ujerumani ambako gazeti la mjini München SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linaandika:

„Hakuna tena haja ya kujua kitovu cha utawala wa GDR.Kimefichuliwa katika kesi mia kadhaa.Ilijulikana na bado inajulikana nini kimetajwa na kimeamuliwa ndani ya hati hiyo inayoruhusu risasi zifyetuliwe.Ilikua msingi wa hukmu zote zilizohusiana na kadhia hizo.Lakini hata kama nakala ya aina pekee iliyogunduliwa hivi karibuni ina maelezo ambayo hakuna aliyekua akiyajua hadi sasa:amri yenyewe haina umuhimu, mamoja, imetolewa kimaandishi au kwa mdomo.Cha muhimu ni ile hali kwamba katika mipaka ya Ujerumani mashariki- GDR watu wameuliwa kutokana na amri hiyo inayoruhusu risasi zifyetuliwe“.


Hayo ni maoni ya SÜDDEUTSCHE ZEITUNG la mjini München.LÜBECKER ZEITUNG limeandika:

„Pengine moyo mtu humdunda na kupigwa na bumbuwazi nyaraka mpya zinapofichuliwa na kubainisha uhabithi na ukatili wa utawala wa Ujerumani mashariki ya zamani .Amri bayana ya kufyetua risasi,bila ya kujali dhidi ya nani,wanawaké na watoto pia hawakusalimika-ni ukatili wa hali ya juu.Hata hivyo kufichuliwa na kuchapishwa hati hiyo hakubadilishi pakubwa.Hoja za kuitumia hati hiyo kisheria zimesutwa saa 48 tuu baada ya kufichuliwa.Nani ametoa amri hiyo,nae pia hajulikani.Hakuna pia kinachobadilika panapohusika na suala la makosa ya kimaadili na nani hasa ameamuru risasi zifyetuliwe.Watu kati ya 700 na 1200 wameuliwa kinyama kabisa katika eneo la mpakani la Ujerumani ya mashariki ya zamani-chanzo walitaka kuihama nchi hiyo ya wafanyakazi na wakulima.Hiyo pekee ni aibu,mamoja,pametolewa amri ya kufyetua risasi au la.“

Mhariri wa gazeti la LANDSHUTER ZEITUNG anahisi:

„Sio pekee patashika iliyosababishwa na kugunduliwa waraka huo,inamfanya Marianne Birthler abainike kazi imemshinda.Patashika hizo hizo ndio sababu ya unga kuzidi maji.Marianne Birther anasema hati hiyo ni mpya,ingawa hati sawa na hiyo ilikwisha gunduliwa na maafisa wa idara yake tangu mwaka 1997.Si hayo tuu:Badala ya kujibebesha dhamana ya makosa yaliyotokea,anataka kujitoa kimaso maso,akififiisha mambo na kudai wahusika wataandamwa kisheria.Kiroja chengine ni pale naibu spika wa bunge la shirikisho Wolfgang Thierse anapoingilia kati na kujaribu kumtetea Marianne Birther na idara yake.Makubwa haya.“

Tuufunge ukurasa wetu wa magazetini kwa kutupia jicho kilichoandikwa na gazeti la ALLGEMEINE ZEITUNG la mjini Mainz.Gazeti linaandika:

„Patashika iliyozuka kuhusiana na waraka unaoamuru risasi zifyetuliwe inabainisha umuhimu uliopo wa kufafanuliwa yote yale yaliyofanyika katika jamhuri ya kidemokrasi na ya kipumbavu katika kipindi kizima cha miaka 50 tangu ilipotangazwa.Inaonyesha hadaa na unyama uliokuwepo.Wote wale ambao kwa miongo kadhaa na kwa sababu tofauti walikua wakiupigia upatu kuusifu utawala huo,wanastahiki hivi sasa kuzama katika bahari ya aibu.“

 • Tarehe 14.08.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHS9
 • Tarehe 14.08.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHS9
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com