Marekani yarejea kwenye kilele cha maambukizi ya COVID-19 | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.06.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marekani yarejea kwenye kilele cha maambukizi ya COVID-19

Ujerumani imerejesha vikwazo vya kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona kwa miji miwili katika jimbo la North Rhine Westphalia baada ya mripuko wa virusi hivyo katika kichinjio kimoja.

Haya yanajiri wakati ambapo ripoti zinaarifu kuwa Marekani imerudi katika kilele cha maambukizi ya virusi hivyo hatari na Uingereza iko katika hatari kubwa ya kukabiliwa na wimbi la pili la maambukizi wakati ambapo Waziri Mkuu Boris Johnson analegeza vikwazo kwa ajili ya kuunusuru uchumi. 

Waziri wa afya wa Ujerumani Jens Spahn siku ya Jumatano amesisitiza kwamba virusi vya corona vinasalia kuwa hatari kubwa baada ya jimbo la Magharibi mwa Ujerumani la North Rhine Westphalia hapo jana kurudisha vikwazo kwa miji miwili kufuatia idadi kubwa ya watu kuambukizwa virusi hivyo katika kampuni moja ya machinjio.

Miji ya Guetersloh na Warendorf ilikuwa miji ya kwanza Ujerumani kuwekewa tena vikwazo ambavyo vilikuwa vimeondolewa taratibu tangu mwezi Aprili. Na sasa waziri Spahn amesema iwapo kutakuwepo mazingira yanayoruhusu virusi hivyo kusambaa, basi vina uwezo wa kusambaa kwa haraka sana.

Holland | Gesundheitsminister - Jens Spahn nach Besuch in Radboudumc

Waziri wa afya wa Ujerumani Jens Spahn

Maeneo mengine ya Ulaya

Kwengineko Ulaya Uingereza kupitia tangazo la Waziri Mkuu Boris Johnson inajiandaa kufunguwa uchumi wake mnamo Julai 4. Hii ni licha ya nchi hiyo kuwa na mojawapo ya idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na virusi vya corona.

Wataalam wanasema iwapo tahadhari hazitochukuliwa basi Uingereza itajikuta inapambana na wimbi la pili la maambukizi.

Hayo yakiarifiwa ripoti zinaarifu kuwa katika kipindi cha miezi miwili, maambukizi mapya ya virusi hivyo Marekani yameongezeka na kufikia kiwango cha juu Kama ilivyokuwa nchi hiyo ilipokuwa kwenye kilele chake cha maambukizi.

Kulingana na takwimu kutoka Chuo Kikuu cha Johns Hopkins zilizochapishwa Jumatano, Marekani iliandikisha maambukizi mapya 34,700. Visa vipya vya maambukizi Marekani vimekuwa vikiongezeka kwa zaidi ya wiki moja sasa baada ya kupungua kwa zaidi ya wiki sita.

Maeneo ya awali yaliyokuwa ndio kitovu kama New York na New Jersey yameshuhudia idadi ikipungua mno ingawa maeneo ya kusini na magharibi mwa Marekani yamekumbwa na ongezeko kubwa la maambukizi.

Rais Donald Trump aliendelea na mkutano wake wa kisiasa huko Arizonab Jumanne, mojawapo ya eneo lililoathirika mno na virusi hivyo. Mamia ya vijana walikusanyika kumsikiliza katika kanisa moja kusikiliza ajenda yake ya kutaka kuchaguliwa kwa muhula wa pili. Meya wa mji wa Phoenix Kate Gallego alikuwa amemtaka kila mmoja kuchukuliwa tahadhari kwa kuvaa barakoa, akiwemo Rais Trump, ila rais huyo alipuuza, hakuvaa barakoa.

Coronavirus | China Peking Ausbruch im Fengtai-Distrikt

Wataalamu wa afya mjini Peking China

Katika maeneo mengine duniani pia, visa vinaongezeka, kwa mfano India imeripoti rekodi ya ongezeko la maambukizi kwa siku moja baada ya kuandikisha maambukizi 16,000 na Mexico ambayo inasemekana kuwa inapima watu wachache iliweka rekodi pia ya maambukizi ya siku moja baada ya kruipoti maambukizi mapya 6,200.

Ila China inaonekana kufanikiwa kupunguza uwezekano wa mripuko mpya mjini Beijing kwani kwa mara nyengine imeonyesha ulimwengu uwezo wake wa raslimali kwa kufanya vipimo milioni 2.5 katika siku kumi na moja tu. Hii leo China imeripoti visa 12 tu kinyume na hapo jana ilipokuwa na visa 22 huku mji wa Beijing ukiripoti visa 7 tu kutoka visa 13 awali.

Korea Kusini ambayo ilifanikiwa kupambana na wimbi la kwanza la virusi vya corona, sasa inashuhudia ongezeko la visa vipya hasa katika Mji Mkuu Seoul. Uongozi wa nchi hiyo uliripoti visa 51 jana na hii inatokana na kulegezwa kwa vikwazo na hali ya maisha kurudi kama kawaida.

Kulingana na Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, watu milioni 9.2 wameambukizwa kote duniani huku zaidi ya 470,000 wakiwa wamefariki dunia kutoka na virusi vya corona kufikia sasa.