1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani inalaani ghasia mashariki mwa DR Kongo

18 Februari 2024

Marekani imelaani hali ya kuongezeka kwa ghasia zinazofanywa na waasi wa M23 katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://p.dw.com/p/4cXfh
Sake, North Kivu Province, DR Kongo
Picha: Benjamin Kasembe/DW

Marekani imelaani hali ya kuongezeka kwa ghasia zinazofanywa na waasi wa M23 katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikisema wafuasi wa kundi hilo lenye kuungwa mkono na Rwanda lazima waondoe makombora ya kisasa ya ardhini hadi angani ambayo yanatishia maisha ya watu mashariki mwa nchi hiyo.Taarifa ya msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Matthew Miller inasema ongezeko hilo la machafuko limengeza hali ya hatari kwa mamilioni ya watu, na kutoa wito kwa M23 kusitisha mara moja uhasama na kujiondoa katika maeneo wanayoyadhibiti katika viunga vya karibu na Sake na Goma. Mapigano yamepamba moto katika siku za hivi karibuni karibu na mji wa Sake, umbali wa kilomita 20 kutoka Goma, kati ya waasi wa M23 na vikosi vya serikali ya Kongo. Idadi kadhaa ya wanajeshi na raia imeripotiwa kuuwawa au kujeruhiwa katika mapigano hayo katika muda wa siku 10 zilizopita.Aidha kwa mapigano hayo ya hivi karibuni yamesukuma maelfu ya raia kukimbia makazi yao kuelekea Goma, ambayo iko katika eneo la kati ya Ziwa Kivu na mpaka wa Rwanda.