Maradhi ya homa ya Uti wa mgongo ni balaa kubwa Afrika Magharibi | Masuala ya Jamii | DW | 13.05.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Maradhi ya homa ya Uti wa mgongo ni balaa kubwa Afrika Magharibi

Barani Afrika, umoja wa bara hilo pamoja na Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS umetoa wito kwa nchi wanachama kuweka mipango ya kukabiliana na mripuko wa maradhi ya homa ya nguruwe iliyoanzia nchini Mexico.

Symolbild Afrika Meningitis

Ramani ya Afrika ikionesha mameneo yanayokabiliwa na homa ya uti wa mgongo

Bado lakini mripuko huo haujapiga hodi kubwa barani humo.Hata hivyo katika nchi nyingi za bara hilo hususani za Afrika Magharibi,zimekuwa kwa miaka mingi zikikabiliwa na mripuko mbaya wa maradhi ya homa ya uti wa mgongo.Mashirika ya misaada yamekuwa katika harakati kubwa za kutoa kinga ya maradhi hayo.


Hapa ni katika jimbo la Kano Kaskazini mwa Nigeria.Kama ilivyo kawaida watoto ndiyo walioko katika nafasi kubwa ya kuathirika na maradhi haya.


Zaidi ya watu elfu mbili wamekufa nchini Nigeria kutokana na maradhi haya ya homa ya uti wa mgongo, na idadi ya vifo imekuwa ikiongezeka katika nchi za Niger, Burkina Faso, Chad na Cameroon.

Ripoti pia zinasema kuwa zaidi ya watu elfu 40 wanaugua maradhi haya ya homa wa uti wa mgongo, ambayo mgonjwa asipowahiwa hufa katika muda wa kipindi cha saa 48 toka alipoambukizwa.


Dr Gbolahan Onyiloye ni mmoja wa madaktari wasio na mipaka Medicins Sans Frontiere wanaohudumia wagonjwa kwenye eneo hili.


´´Tunawatofautisha wagonjwa wetu kwa mujibu wa umri wao.Kwa wagonjwa waliyo na umri kuanzia miaka miwili kwa ujumla huwa tunaangalia dalili kama vile maumivu ya kichwa, shingo na mabaka usoni na mgongoni.Kwa watoto wadogo kabisa, huwa haraka sana tunawapima homa na joto linapofikia kiwango cha nyuzi joto 38 basi hutiliashaka.Na wengine tunaangalia dalili kwa ujumla kama vile misuli ya mwili kuwa tepetepe.´´Maradhi haya ya homa ya uti wa mgongo ambayo hudhuru ndani kwa ndani, yanayosababishwa na virusi na bakteria, yamekuwa mara kwa mara yakiyakumba maeneo ya ukanda wa Saheli kuanzia Mauritania mpaka Ethiopea.

Mwaka huu nchi za Nigeria na Niger ambazo ni kati ya nchi zenye idadi kubwa ya watu barani Afrika zimekumbwa na mripuko wa maradhi hayo ya homa wa uti wa mgongo.


Na hapa ndipo shirika la madaktari wasio na mipaka lilipoanzisha mpango wake mkubwa kabisa wa kutoa kinga ya maradhi haya kwa watu zaidi ya milioni nane.


Madaktari hao wanaogopa kutokea kwa janga kubwa la mripuko wa maradhi hayo kama lile la mwaka 1996 ambapo zaidi ya watu elfu 25 walikufa.


Lakini Sajenti Mark La Force kutoka mradi wa kimarekani wa kupambana na maradhi hayo anasema kuwa tumaini la kukabiliana na hatari ya mripuko kama huo iwapo utatokea ni dogo.


Hiyo inatokana na imani ya dawa dhidi ya maradhi hayo kupungua miongoni mwa wananchi, kufuatia kufa kwa watoto 11 zaidi ya miaka kumi iliyopita Kaskazini mwa Nigeria kulikosababishwa na kunywa dawa aina ya Trovan ya kuzuia maradhi hayo.


´´Hii ni moja kati ya changamoto, na ndiyo maana imekuwa vigumu sana kudhibiti mripuko wa maradhi haya.Kinga ya chanjo inayotumika hivi sasa ni aina ya dawa ambayo huweza kudumu mwili mwa mwanadamu kwa muda mfupi.Kwa hivyo hata kama watu watapatiwa chanjo hiyo, lakini huenda wakawa katika hatari baada ya kipindi cha miaka miwili au mitatu toka kupatiwa chanjo hiyo´´


Sajenti Mark La Force anasema kuwa imekuwa vigumu mwaka hata mwaka kutabiri lini na wapi mripuko huo utatokea, kwasababu maandalizi yanaweza kufanyika kwa ajili eneo ndogo lakini ukakuta eneo lilikabiliwa na mripuko ni kubwa.


Vile vile Sajenti Mark La Force anasema tatizo lingine ni uhaba wa fedha, pamoja na kwamba Umoja wa Ulaya na Shirika la Afya duniani vimetoa mamilioni ya dola kukabiliana na maradhi haya.


´´Hatua ya kupambana na mripuko wa maradhi haya mara zote umekuwa mgumu, kwasababu inahusisha maamuzi katika kuamua nani wapewe, kwani kwa kawaida hakuna dawa za kutosha kuweza kuwapatia watu wote kwa wakati mmoja´´


Lakini Shirika la madaktari wasio na mipaka linajaribu kukimbizana na muda kukabiliana na maradhi haya kwa kusambaza kinga kunusuru maisha ya watu wa eneo hili.


Mwandishi:Aboubakary Liongo/ZPR

Mhariri:Thelma Mwadzaya

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com