Maporomoko ya ardhi yauwa 300 Afghanistan | Masuala ya Jamii | DW | 04.05.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Maporomoko ya ardhi yauwa 300 Afghanistan

Timu za uokozi zimeachana na shughuli za kuwatafuta wahanga Jumamosi(03.05.2014) baada ya maporomoko ya ardhi kukifukia kijiji kilioko pembezoni mwa mlima kaskazini mwa Afghanistan na kuuwa takriban watu 300.

Watu wakiwa katika harakati za kutafuta wahanga na miili iliofukiwa na maporomoko ya ardhi Afghanistan.

Watu wakiwa katika harakati za kutafuta wahanga na miili iliofukiwa na maporomoko ya ardhi Afghanistan.

Wenyeji wa eneo hilo na wafanyakazi wa uokozi wakitumia sepetu wamejaribu kwa taabu kuwatafuta wahanga waliokwama chini ya vifusi vya maporomoko hayo makubwa ya ardhi ambayo yamekifukia kijiji cha Aab Bareek kilioko katika jimbo la Badakhstan linalopakana na Tajikistan.

Maafisa wanasema idadi ya vifo inaweza kuongezeka na kufikia 500.Gavana wa Badakhstan Shah Waliullah Adeeb amewaambia waandishi wa habari katika eneo la janga hilo kwamba kwa kuzingatia repoti zao,nyumba 300 zimefukiwa na kifusi na kwamba wana orodha ya watu 300 waliothibitishwa kuwa wamekufa.

Amesema hawawezi kuendelea tena na operesheni ya uokozi na kutafuta miili ya watu kutokana na kwamba nyumba hizo zimefukiwa na futi nyingi za matope na kwamba watakachofanya ni kuwaombea dua wahanga na kulifanya eneo hilo kuwa kaburi la pamoja.

Gul Mohammad Bedar naibu gavana wa Badakhshan ameliambia shirika la habari la AFP kwamba idadi iliotangazwa mwanzo ya kuhofiwa kuuwawa kwa watu 2,500 ilitolewa na wenyeji wa eneo hilo na sio kutoka timu yao ya ufundi.Amesema wanadhani idadi ya vifo haitopindukia 500.

Hakuna matumaini kupatikana wahanga

Wanavijiji na askari polisi wachache wakiwa na zana za msingi tu za uchimbaji waliendelea tena na juhudi zao za kuwatafuta wahanga wakati jua lilipochomoza lakini mara moja ilikuja kubainika kwamba hakuna matumaini ya kuwapata wahanga waliofukiwa na matope hadi mita 100.

Muhanga wa maporomoko ya ardhi Afghanistan.

Muhanga wa maporomoko ya ardhi Afghanistan.

Mwanamke mmoja mzee amekaririwa akisema "Ndugu saba wa familia yangu walikuwepo hapa.......watano au wanne kati yao wameuwawa. Mimi mwenyewe niko nusu hai, nifanye nini ?"

Timu ya Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan imesema sasa nadhari inaelekezwa kwa watu zaidi ya 4,000 waliopotezewa makaazi yao aidha kutokana na kuathiriwa moja kwa moja kama matokeo ya maporomoko hayo ya ardhi ya Ijumaa au hatua ya tahadhari kwa vijiji vinavyohesabiwa kuwa katika hatari.

Ari Gaitanis msemaji wa Kikosi cha Usaidizi cha Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan amesema mahitaji yao makubwa ni maji,madawa,chakula na hifadhi ya dharura.

Eneo hilo la kimaskini la vijiji vyenye nyumba za matofali ya udongo vilioko katika mabonde yalioko pembezoni mwa milima isiokuwa na miti mara kwa limekuwa likikumbwa na maporomoko ya ardhi katika miaka ya hivi karibuni.

Kilio cha msaada

Jeshi la Afghanistan likisafirisha misaada kwa wahanga wa maporomoko ya ardhi.

Jeshi la Afghanistan likisafirisha misaada kwa wahanga wa maporomoko ya ardhi.

Sehemu ya mlima juu ya kijiji cha Aab Bareek ilianguka kama saa tano asubuhi hapo Ijumaa wakati watu wake walipokuwa wakijaribu kukusanya vitu vyao na mifugo yao baada ya kutokea kwa poromoko dogo la ardhi masaa machache kabla.

Mamia ya nyumba ziliangamizwa katika maporomoko hayo ya ardhi ambayo yalichochewa na na mvua kubwa.Kuna wasi wasi sehemu nyengine ya mlima huo inaweza kuporomoka wakati wowote ule.

Jeshi la Afghanistan limezisafirisha timu za uokozi kwenye eneo hilo leo hii kutokana na kwamba eneo hilo la milimiani lilioko mbali linaweza tu kufikiwa kwa kupitia barabara mbaya zilizo nyembamba ambazo zenyewe zimeharibiwa kutokana na mvua kubwa iliokuwa ikinyesha kwa zaidi ya wiki.

Tinga tinga la uchimbaji likiwa kazini katika eneo la maporomoko ya ardhi Afghanistan.

Tinga tinga la uchimbaji likiwa kazini katika eneo la maporomoko ya ardhi Afghanistan.

Kanali Abdul Qadeer Sayad naibu mkuu wa polisi katika jimbo la Badakhstan ameliambia shirika la habari la Uingerera Reuters kwamba wameweza kupata tinga tinga moja la kuchimbia katika eneo hilo lakini shughuli hiyo ya uchimbaji ilionekana kukatisha tamaa. Amesema ukubwa wa eneo lililoathirika na kina cha matope inamaanisha kwamba mashine za kisasa tu ndio zitakazoweza kusaidia.

Vikosi vya muungano vinavyoongozwa na Jumuiya ya Kujihami ya NATO vimewekwa katika hali ya tahadhari kutowa msaada lakini wamesema kwamba serikali ya Afghanistan haikuomba msaada.

Mwanaume mwenye umri wa makamo amenukuliwa akitowa wito kwa serikali kwenda na kuwasaidia watu wao kuikwamuwa miili.

Mwanaume huyo aliyekuwa amesimama kwenye mlima unaoanglia mto wa matope ambako ndiko kilichokuwepo kijiji chake hapo awali amesema " Tumeweza kuwatowa watu 10 hadi 15 tu,vijiji vyote viliobakia vimenasa kwenye matope hayo ya udongo".

Mvua za msimu na kuyayuka kwa theluji ya kipindi cha machipuko kumesababisha uharibifu katika sehemu kubwa ya eneo la kaskazini mwa Afghanistan na kuuwa zaidi ya watu 100 kabla ya kuzuka kwa janga hili la karibuni kabisa.

Mwandishi : Mohamed Dahman/ AFP/Reuters

Mahariri : Bruce Amani

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com