1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mapigano yaendelea Syria

3 Aprili 2012

Mapigano makali baina ya majeshi ya serikali na wapiganaji wa upande wa upinzani yameendelea leo nchini Syria, licha ya Rais Bashar al-Assad kukubali kutekeleza mpango wa amani uliopendekezwa na Kofi Annan.

https://p.dw.com/p/14XCS
Wapiganaji mjini Damascus
Wapiganaji mjini DamascusPicha: AP

Shirika linaloshughulikia haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake makuu jijini London, Uingereza, limeripoti kwamba mapigano yalitokea leo katika maeneo mbali mbali ya Syria ikiwemo mikoa ya Daraa, Idlib, Homs na maeneo yaliyo karibu na mji mkuu Damascus. Katika mkoa wa Daraa, ambao ni moja ya ngome kuu za wapiganaji wanaoupinga utawala wa Assad, mapigano yalizuka jana usiku katika mji wa Inkhel baada ya waasi kushambulia maeneo ya ukaguzi wa jeshi.

Sayyed Mahmud, ambaye ni mwanaharakati aliyeko Daraa, ameliambia shirika la habari la afp kwa njia ya simu kwamba hali ya usalama katika mji wa Dael uliko katika mkoa wa Daraa ni tete kabisa. Mahmud ameeleza kwamba wanajeshi wa Syria jana walichoma moto nyumba 14 pamoja na kukamata watu. Mwanaharakati huyo aliendelea kueleza kwamba utawala wa Syria una mpango wa kuwafanya watu wafe kwa njaa, na hivyo wanajeshi wanaingia kwa nguvu katika nyumba za watu na kuharibu vyakula pamoja na vifaa vya matumzi. Wanajeshi hao huingia pia katika maduka ya kuokea mikate na kuharibu unga.

Watu wakiukimbia mkoa wa Daraa
Watu wakiukimbia mkoa wa DaraaPicha: AP

Shirika la msalaba mwekundu kupewa ushirikiano

Katika mkoa wa Idlib, mapigano makali yalifanyika nje ya eneo la mji wa Taftanaz. Shirika la kutetea haki za binadamu nchini Syria limeripoti kwamba raia wawili pamoja na askari wanne waliuwawa. Mapigano yaliripotiwa pia katika mji mkuu Damascus ambapo majeshi yalivamia nyumba na kukamata watu.

Mapigano haya yametokea wakati ambapo kiongozi wa shirika la msalaba mwekundu, Jakob Kellenberger, yuko ziarani nchini Syria. Hii ni ziara yake ya tatu nchini humo tangu kuanza kwa mapigano ambayo Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 9,000. Nao utawala wa Syria unaripoti kwamba maafisa wa usalama wapatao 3,000 wameuliwa na makundi ya waasi. Waziri wa mambo ya kigeni wa Syria, Wallid Muallem, amemhakikishia Kellenberger kwamba nchi yake itafanya juhudi zote kuziwezesha shughuli za shirika la msalaba mwekundu.

Jakob Kellenberger wa shirika la msalaba mwekundu
Jakob Kellenberger wa shirika la msalaba mwekunduPicha: dapd

Baraza la kitaifa la Syria limeukubali mpango wa Kofi Annan wa kuleta amani wenye vipengele sita. Hata hivyo, baraza hilo halikutoa tamko lolote juu ya lengo la kusitisha mapigano ifikapo tarehe 10 mwezi huu. Baadhi ya wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wameeleza kuwa wanahofia kwamba huenda wapiganaji nchini Syria wakaongeza kiasi cha mashambulizi wiki hii.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/RTRE/AFPE/

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman