Maoni:Uhuru wa vyombo vya habari utetewe kikamilifu | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.05.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Maoni:Uhuru wa vyombo vya habari utetewe kikamilifu

Uhuru wa vyombo vya habari utetewe kwa nguvu zote anasema mkurugenzi mkuu wa DW Peter Limbourg katika uhariri wake unaomulika pia miaka 65 ya kituo cha matangazo ya kimataifa cha Ujerumani-Deutsche Welle

May tatu ni siku ya uhuru wa vyombo vya habari. Ni vyema kuwa na siku kama hiyo. Angalao mara moja kwa mwaka watu wanaikumbuka haki hiyo ya binaadam. Uhuru wa vyombo vya habari-mada ya kuvutia ambayo watu wanajitambulisha nayo kijuujuu. Siku nyengine 364  za mwaka zilizosalia haziwashughulishi watu sana. Kuna baadhi ya mifano hapa:

 

Kuyanyamazia maovu kwaajili ya masilahi ya kiuchumi

 

Wanasiasa wa kidemokrasi kutoka ulaya wanashindania kujipendekeza nchini China. Uhuru wa vyombo vya habari katika nchi hiyo hakuna na matangazo huru ya Deutsche Welle na vituo vyengine vya matangazo vya kimataifa, yanazuwiliwa moja kwa moja nchi humo. Na wawakilishi wa sekta ya kibiashara pia wanapokuwa China wanafikiria zaidi biashara nono badala ya haki za binaadam. Kwa namna hiyo watu wanajiachia kunasa katika makucha ya uovu na kiu cha madaraka cha Peking.

Kwasababu nchini China hakuna atakaeandamana ikiwa wawekezaji wa kigeni watasumbuliwa. Lawama kuhusu hilo, hazikutikani katika vyombo vya habari.

Idadi kubwa ajabu ya wanasiasa wa Ujerumani na Ulaya wanapigania  watu wamuelewe vyema rais wa Urusi Vladimir Putin. Wasi wasi wake kuelekea jumuia ya kujihami ya NATO na Umoja wa ulaya unabidi uzingatiwe. Hofu za waandishi habari nchini Urusi lakini zinaoneklana kama kero tu na ndio maana hazizingatiwi: hofu zao kuelekea vitisho, mateso au hata vifo. Cha kutia moyo hapo ni kwamba waziri mpya wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Heiko Maas anafuata msimamo mwengine .

Iran pia inayawekea vizuwizi matangazo ya DW na ya vituo vyingi vyengine vya kimataifa na kuwasumbua moja kwa moja wafanyakazi wake. Hakuna anaezungumzia kuhusu waandishi habari 23 wanaoshikiliwa katika jela za mateso za walinzi wa mapinduzi. Hata hivyo kuna wanasiasa wanaootea kujongeleana. Kujongeleana na utawala unaodhamiria kuiteketeza Israel , kuleta vurugu katika eneo lote la Mashariki ya kati na kueneza ugaidi.

Mageuzi Saudi Arabia-Yatamfaidisha lini Raaif Badawi?

 

Mrithi wa kiti cha ufalme wa Saud Arabia anashangiriwa kwasababu amewaruhusu wanawake waendeshe magari na kuruhusu kumbi za sinema zifunguliwe. Wakati huo huo mwanablogi Raaif Badawi bado anashikiliwa jela nchini Saud Arabia kwasababu tu ya kuitumia haki yake ya kimsingi ya uhuru wa mtu kutoa maoni yake.

Watawala wa kimabavu barani Afrika wanadai na kupatiwa misaada zaidi ya maendeleo, lakini wanawapokonya vijana, waandishi habari wenye bidiii , uwezo wa kuendesha ipasavyo shughuli zao kupitia vituo vya kibinafsi vya matangazo.

Nchini Bangladesh na Pakistan wanablogi wanayatia hatarini maisha yao wanapokosoa itikadi kali ya kiislam inayozidi kupata nguvu katika nchi hizo. Uungaji mkono wa dhati kutoka nje, ni tunu licha ya juhudi za wanadiplomasia. Nchini Afghanistan ambako wanajajeshi wa Ujerumani wanawajibika kwa zaidi ya miaka 15 sasa kulinda utulivu, uhuru na  amani, waandishi habari 10 wameuliwa jumatatu iliyopita na magaidi wa itikadi kali.

Mexico ni mshirika wa maonyesho ya mwaka 2018 ya Hannover. Hakuna nchi yoyote nyengine ambako waandishi habari wako hatarini kama huko kwasababu serikali inashindwa kuyadhibiti makundi yanayofanya biashara ya madawa ya kulevya. Mwaka jana waandishi habari 11 waliuliwa-nchini Syria tu ndiko waandishi wengi zaidi waliuliwa. Serikali za nchi za magharibi zinabidi zitambue jukumu lao kwasababu wengi wanaotumia madawa hayo ya kulevya wanakutikana katika nchi zao.

Orodha ni ndefu. Inaweza kutufikisha Uturuki ambayo ni mwanachama wa jumuia ya kujihami ya NATO na pia Poland na Hungary, ambazo ni wanachama wa umoja wa ulaya.

Ni orodha ya kuhuzunisha. Orodha ya nchi zinazojitambulisha kijuu juu tu siku inapowadia.

Wananchi tufanye nini?

 

Zitattafel Limbourg

Mkurugenzi mkuu wa Deutsche Welle Peter Limbourg

Tunabidi tuwatathmini viongozi wa serikali na wanasiasa wetu kuambatana na kile wanachokifanya kupinga visa vya kuendewa kinyume uhuru wa vyombo vya habari. Jee wanawazindua waimla kinaga ubaga kuhusu maadili yetu? Jee wako tayari kuachilia mbali mikataba wanapotambua maadili hayo hayaheshimiwi? Wanafungamanisha utayarifu wa kutoa misaada ya maendeleo na kuheshimiwa haki za binaadam na uhuru wa vyombo vya habari?

Demokrasia inahatarishwa katika kila pembe ya dunia na waimla, utawala wa mtu mmoja na wenye kujitafutia umaarufu. Demokrasia itanusurika tu ikiwa wapenda demokratia watasimama kidete kuitetea.

Leo May tatu Deutsche Welle inaadhimisha siku ilipoanzishwa: Kwa muda wa miaka 65 tunawaeleza walimwengu katika kila pembe ya dunia, habari huru na zisizoelemea upande wowote.Tutaendelea kupigania uhuru wa vyombo vya habari.Tutasema ukweli mtupu.Tunaahidi."

 

Mwandishi: Limbourg,Peter/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com