Maoni ya wahariri wa magazeti
22 Aprili 2010Sakata linalohusu kunyanyaswa na kuharibiwa watoto wa kiume na makasisi wa kanisa katoliki bado linaendelea. Hapa nchini Ujerumani askofu Walter Mixa amejing'atua.
Wahariri wa magazeti wanatoa maoni yao juu ya askofu huyo.
Wahariri hao pia wanazungumzia juu ya udhaifu uliojitokeza katika umoja wa nchi za Ulaya kufuatia janga lililosababishwa na mlipuko wa volkano,na vile vile wanatupia macho matukio ya kisiasa nchini Poland baada ya kifo cha rais Kaczynski.
Magazeti karibu yote ya hapa nchini leo yanatoa maoni juu ya kujizulu kwa askofu wa dayosisi ya Augsburg, Walter Mixa kutokana na kashfa zinazoendelea kuliandama kanisa katoliki. Askofu huyo amejiuzulu baada ya kukiri kwamba alikuwa na mkono mwepesi katika kuwarudi watoto, yaani alikuwa anawapiga watoto.
Mhariri wa gazeti la Heilbronner anasema hatimaye Askofu Walter Mixa ameng'atuka.Amefikia uamuzi huo baada ya kutambua kwamba ushahidi dhidi yake ulikuwa unaongezeka kila siku, juu ya kuwapiga watoto na juu ya kudokoa fedha kutoka kwenye mfuko wa yatima.Mhariri wa gazeti la Heilbronner anasema majuto aliyoyaonyesha askofu huyo yalikuja aherini sana. Kwa hiyo uamuzi wake wa kujiuzulu ni ukombozi kwa kanisa katoliki ambalo kwa sasa linakabiliwa na mgogoro mkubwa.
Juu ya askofu huyo gazeti la Darmstädter Echo linasema kwa kadri alivyokuwa anaendelea kung'ang'ania kiti, ndivyo alivyokuwa anazidi kuvuruga wajihi wa kanisa.
Na kanisa ndiyo nguzo ya mfumo wa maadili nchini Ujerumani, anasema mhariri wa gazeti hilo la Darmstädter Echo.
Mhariri wa gazeti la Hessische/Niedersächsiche Allgemeine anasema askofu Mixa angeliweza kujiondoa kanisani kwa heshima ,lakini hakuitumia fursa aliyokuwa nayo.
Mhariri huyo pia anasema alichofanya askofu huyo kinawakilisha kilele cha kile kinachoenda kinyume na imani ya waumini.
Magazeti ya Ujerumani leo pia yanazingatia
masuala ya kimataifa ,kwa mfano juu ya
mgogoro uliosababishwa na mlipuko wa
volkano.
Mhariri wa gazeti la Neue Presse anasikitika kwamba Ulaya haikuzungumza na sauti moja juu ya mgogoro huo.Mhariri huyo anaeleza kwamba nchi za Ulaya bado zipo mbali sana na umoja. Lakini mgogoro uliosababishwa na mlipuko wa volkano umeonyesha umuhimu wa kuwapo umoja huo.Gazeti hilo linasema tofauti zilizokuwapo juu ya kukabilliana na hatari ya volkano zimeonyesha kuwa mgawanyiko unaweza kuleta maafa.
Gazeti la Berliner Zeitung linatoa maoni juu ya Poland baada ya kifo cha rais wa nchi hiyo Lech Kazcyinski.
Gazeti hilo linasema,kufuatia kifo cha Kaczynski uchaguzi utakaofanyika utaonyesha iwapo mshindi-yaani rais mpya- atayaunga mkono mageuzi yanayoletwa sasa na waziri mkuu .
Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche
Zeitungen/
Mhariri/Abdul-Rahman